


HATUA ya
mwanazuoni wa siku nyingi nchini, Profesa Issa Shivji kupinga hukumu ya
Mahakama ya Rufani Tanzania iliyomrejeshea ubunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema imemtia matatani na baadhi ya watu wanasema gwiji huyo wa
sheria “huenda amenukuliwa vibaya au hajasoma hukumu husika.”
Jana
Wakili wa Lema, Tundu Lissu, alimkosoa Profesa Shivji pamoja na Rais wa
Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, Francis Stolla akisema wanasheria
hao wamepotoka katika matamshi yao ya kupinga hukumu ya Mahakama ya
Rufani.
Matamshi ya
Shivji pia yaliiteka mijadala katika mitandao ya kijamii ya Jamii
Forums, Mabadiliko na Facebook ambako wachangiaji walikuwa wakivutana
huku baadhi yao wakisema wazi kwamba msomi huyo amekosea huku wengine
wakimtetea kwamba yuko sahihi.
Akizungumza
na gazeti hili jana kutoka Songea mkoani Ruvuma, Lissu alipinga vikali
hoja zilizotolewa na Profesa Shivji pamoja na Stolla, akisema kuwa
hazina mashiko na zinaweza kutolewa tu na mtu ambaye hakufuatilia
mwenendo wa kesi hiyo.
Juzi Profesa
Shivji na Stolla walinukuliwa wakiikosoa hukumu ya Mahakama ya Rufani,
iliyomrejesha bungeni Lema wakisema hukumu hiyo iliyotolewa na majaji
watatu Salum Massati, Bernard Luanda na kiongozi wao Nathalia Kimaro,
inapingana na sheria.
Lissu katika
maelezo yake alisema uamuzi wa mahakama katika kesi ya Lema umejenga
upya msingi bora wa matumizi ya vyombo vya uamuzi, kwani kesi nyingi za
kupinga matokeo ya ubunge, zimekuwa zikifunguliwa na watu ambao wamekuwa
wakitumwa na vigogo wa kisiasa na watu wenye fedha.
Akizungumza
na Mwananchi, Lissu alisema hoja hizo hazina mashiko na kuwa ile
iliyotolewa na Profesa Shivji inatokana na msomi huyo kuzungumza
kitaalamu bila kuangalia mazingira halisi ya siasa za Kitanzania.
Lissu
alisema mahakama ya rufani haikupiga marufuku wapiga kura kufungua kesi
za kupinga ila iliwataka tu kufanya hivyo pale haki zao zinapokiukwa.
“Kwanza siyo
kweli kwamba mahakama imepiga marufuku wapiga kura kufungua kesi,
ilisema watafanya hivyo pale ambapo haki zao zimevunjwa, haki zenyewe ni
kupiga kura, kura zao kutohesabiwa ama suala jingine litakalomnyima
kupiga kura, hizo ndiyo haki za mpiga kura,” alisema na kuongeza:
“Sasa
mwalimu wangu, Profesa Shivji yeye anatazama tu kwa jicho la kitaalamu
na kusema haki za binadamu zimekiukwa, kwa muda wanasiasa, matajiri na
CCM wamekuwa wakiwatumia wananchi kuwapinga wabunge wa upinzani.”
Uchambuzi wa Lissu
Alitoa
mfano akisema katika uchaguzi wa 1995, Dk Willibrod Slaa alishinda
ubunge na watu wanaojiita wananchi walifungua kesi kupinga ushindi huo,
mwaka 2000 wakampinga tena na hata 2005.
Alisema 1995
Makongoro Nyerere aliposhinda ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini
kupitia NCCR- Mageuzi, watu wanaojiita wananchi walifungua kesi ambayo
matokeo yake yalikuwa mbunge huyo kupoteza kiti chake.
Lissu
alisema 2005 aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Marehemu Chacha Wangwe
alifunguliwa kesi na watu waliojiita wananchi ambao mwisho wake
walishindwa.
“Hawa
wananchi ambao wanafungua kesi zenye mawakili wanaolipwa mamilioni ya
fedha ni watu ambao hata fedha za kununua viatu hawana, hawa waliokuwa
wakimpinga Marehemu Wangwe nikiwa mahakamani niliwauliza kama wanawajua
mawakili waliokuwa wanawatetea, walikuwa hawawajui.
Nikawauliza kama wamewahi kufika Dar es Salaam wakasema hapana, sasa sijui waliwapataje wale mawakili,” alisema na kuongeza:
“Wote hawa
wanakuwa ni watu wanaotumiwa. Mwaka huu kati ya wabunge wote 25 Chadema
tulioshinda, 14 tulifunguliwa kesi na kati ya hizi 12 zimefunguliwa na
watu wanaojiita wananchi, hii ni kutumiwa,” alisema.
Alisema mara
baada ya uchaguzi mwaka 2010 aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf
Makamba, aliandika waraka kuwataka makatibu wa chama hicho kufungua kesi
kwa majimbo yote ambayo chama hicho kiliangushwa jambo alilosema ndilo
liliwasukuma kuwatumia wananchi.
Kuhusu hoja
kuwa mahakama hiyo ya rufani imeingilia kazi ya kutunga sheria badala ya
kuzitafsiri na kuwa imepingana na sheria ya Bunge na Mahakama Kuu
katika kesi ya Chediel Mgonja ya mwaka 1980, Lissu alisema hazina
mashiko.
“Hiyo ni
hoja ya kipuuzi. Hiyo sheria ya kuwa mwananchi yeyote ana haki ya
kufungua kesi kuwa imetenguliwa na Mahakama ya Rufani, hata mwanafunzi
wa mwaka wa kwanza wa sheria ukimuuliza atakwambia kuwa, amri ya
Mahakama Kuu wala ya Mahakama ya Rufani yenyewe haiwezi kuizuia mahakama
hiyo ya juu kabisa nchini kufanya uamuzi wake,” alisema.
Akizungumzia
hoja ya Stolla kwamba mahakama iliibua jambo jipya la kuhoji kama
wajibu rufani walikuwa wapiga kura ama la, alisema Rais wake huyo hana
hoja, kwani wakili wa walalamikaji aliibua hoja kama hiyo na alipoulizwa
na mmoja wa majaji kuwa “Hata sisi hatuwezi kulizungumzia suala hili,
alishindwa kujibu akawa anajikanyaga tu,” alisema.
Aliongeza:
“Kwenye rufaa ya kwanza mahakama inaruhusiwa kuibua chochote, sasa hizo
ni hoja zinazotolewa na watu ambao marafiki zao wa CCM wameshindwa sasa
wanavaa joho la utaalamu kutoa hoja kama hizi zisizo na mashiko.”
Shivji na Stolla
Profesa
Shivji kwa upande wake alieleza kushangazwa na maelezo ya Mahakama ya
Rufani kuwa mpiga kura hana haki ya kufungua kesi ya kupinga matokeo ya
uchaguzi na kusema hiyo ni sawa na kutunga sheria mpya na si kutafsiri
zilizopo.
“Sheria ya
Bunge na Mahakama Kuu katika kesi ya Mgonja (Chediel ya mwaka 1980),
vinampa haki mpiga kura kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo.
Sijaona hoja nzito ya Mahakama ya kufuta haki hiyo ya mpiga kura,”
alisema Profesa Shivji.
Kwa upande
wake, Stolla alisema: “Nimesikiliza hata maoni ya wanasheria mbalimbali
wakizungumzia kutopendezwa na tafsiri ya Mahakama ya Rufani kuhusu haki
ya mpiga kura ‘ku-challenge’ (kupinga) matokeo ya uchaguzi mahakamani.
Aliongeza:
“Katika uamuzi wa kisheria, inaonekana Mahakama imetunga sheria mpya na
wengi tunajiuliza kama siyo, ni sababu gani nyingine inampa haki mpiga
kura kupinga matokeo?”
Stolla
alisema Sheria ya Bunge ya Uchaguzi ya tangu mwaka 1985, ambayo
ilifanyiwa marekebisho mwaka 2002, kabla ya kutungwa upya mwaka 2005,
inampa haki mpiga kura kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani.
Kesi ya Lema
Lema alivuliwa ubunge na Mahakama Kuu
Kanda ya Arusha, Aprili 5, mwaka huu kutokana na kesi iliyofunguliwa na
makada watatu wa CCM, Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel,
wakipinga ushindi wake.
Walikuwa
wakidai kuwa katika kampeni zake alikuwa akitumia lugha ya matusi,
kejeli na ubaguzi wa kijinsia dhidi ya aliyekuwa mgombea wa wadhifa huo
kwa tiketi ya CCM, Dk Batilda Buriani.
Mahakama
Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibarila ilimtia
hatiani kwa kutumia lugha ya matusi na kutengua matokeo yaliyompa
ushindi.
Hata hivyo, alikata rufaa Mahakama ya
Rufani kupitia kwa mawakili wake, Method Kimomogoro na Tundu Lissu
ambayo Desemba 21, mwaka huu ilimrejesha tena bungeni baada ya kukubali
rufaa yake.
Katika uamuzi wake, Mahakama hiyo
ilisema kwa kuwa kisheria hayo ni masilahi ya umma kufikishwa mahakamani
chini ya Ibara ya 26 (2) ya Katiba na kwamba mlalamikaji anapaswa
kuonyesha haki zake au masilahi ambayo yameingiliwa na athari
alizozipata.
Habari na Fredy Azzah
Chanzo - Mwananchi
Post a Comment