(A) Mkutano Mkuu
KAMATI
ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania
(TASWA), iliyokutana katikati ya wiki jijini Dar es Salaam imekubaliana
na mapendekezo ya baadhi ya wanachama kuomba isogeze mbele kwa wiki moja
Mkutano Mkuu wa chama hicho.
Awali mkutano huo ulipangwa kufanyika Desemba 21 na 22 mwaka huu Kiromo View Resort Hotel, Bagamoyo mkoani Pwani, hivyo sasa utafanyika Desemba 28 na 29 mahali hapo hapo.
Hatua
hiyo ya kusogeza mbele inatokana na baadhi ya wanachama kuomba iwe
hivyo kutokana na Jumamosi ya Desemba 22 kutakuwa na mchezo wa kirafiki
wa kimataifa kati ya timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na
ile ya Zambia ‘Chipolopolo’ kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa
msingi huo tumekubaliana na hoja kwamba mchezo huo kwa kiasi fulani
ungeathiri umakini wa wajumbe kwenye mkutano kwa namna moja au nyingine,
hivyo kupunguza tija.
Tunaamini
idadi kubwa ya wanachama waliothibitisha kushiriki ni ishara kwamba
wengi wanataka kujumuika kwa asilimia kubwa katika kukijenga chama chao,
hivyo hatuoni sababu ya kufanya mkutano kwa kukurupuka.
Hadi
kufikia Desemba 15 ambayo ilikuwa siku ya mwisho ya wanachama
kuthibitisha ushiriki wa mkutano zaidi ya asilimia 95 ya wanachama
walikuwa wamethibitisha kushiriki.
Kutokana
na hali hiyo wote waliothibitisha ushiriki huo na ni hai watajulishwa
kwa barua rasmi, ambazo zitaeleza utaratibu wa namna ya kufika Bagamoyo
na mambo mengine muhimu yatakavyokuwa.Barua zitaanza kutoka wakati
wowote kuanzia Jumatano ijayo baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya
TASWA kinachotarajiwa kufanyika siku hiyo.
Pia
tayari TASWA imewaalika wadau mbalimbali wakiwemo wahariri wakongwe
ambao wamethibitisha kushiriki kwenye mkutano huo wa aina yake.TASWA
baada ya kupata udhamini wa Zantel kwa
ajili ya mkutano huo bado inaendelea na mazungumzo na wadhamini
mbalimbali na inatarajia kuwatangaza wakati wowote mambo yatakavyokuwa
mazuri.
(B) Pongezi
TASWA
inawapongeza viongozi wapya wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC)
walioingia madarakani Desemba 8, mwaka huu mkoani Dodoma, ambapo Ghullam
Rashid alichaguliwa tena kuwa Rais, huku Filbert Bayi akichaguliwa tena
kuwa Katibu Mkuu.
Tunaahidi
kuendelea kushirikiana na uongozi wa TOC kama ilivyokuwa wakati
uliopita na kuwatakia kila la kheri katika kutekeleza majukumu yao na
tuna imani watafanya vyema.
(C) Msiba:
Tumepokea
kwa masikitiko makubwa taarifa ya msiba wa mwandishi wa zamani wa
habari za michezo, Amina Singo kilichotokea usiku wa kuamkia leo.
Tunaungana
na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu kwani wakati wa uhai
wake alikuwa mdau mkubwa wa TASWA wakati huo akiwa mtangazaji wa habari
za michezo wa Redio Times FM, hivyo kifo chake ni pengo kubwa kwa tasnia
ya uandishi wa habari hapa nchini.
Kwa mujibu wa marafiki za marehemu msiba upo Mbezi na mipango ya mazishi inaendelea. Tukipata taarifa zaidi tutajulishana.
Nawasilisha.
Amir Mhando
Katibu Mkuu
16/12/2012.
Post a Comment