Mume wa aliyekuwa Ofisa Uchunguzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia
Rushwa (Takukuru), marehemu Bhoke Ryoba ambaye aliuawa juzi kwa kupigwa
risasi amesema kifo cha mkewe kimegubikwa na utata mwingi.
Akizungumza na Mwananchi mumewe huyo, Charles Gibore, pamoja na
mambo mengine alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah na
Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo kubaini
ukweli.
“Mke wangu aliuawa na mfanyakazi mwenzake na tukio hilo limegubikwa
na utata ambao Takukuru na Polisi ndiyo pekee wanaoweza kutupa ukweli,”
alisema Gibore nje ya chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam. Kusoma zaidi bofya
Gibore alieleza kuwa mkewe huyo aliuawa usiku wa kuamkia Jumapili
katika tafrija ya kuagana na kupongezana na baadhi ya wafanyakazi
wenzake wa Takukuru waliokuwa wamepandishwa vyeo, tafrija ambayo Bhoke
alipewa zabuni ya kupika chakula.
Alisema pia mkewe aliombwa pia awapatie wenye sherehe hiyo, vijana
wawili wa kuwachomea nyama… “Vijana hao walikwenda asubuhi ukumbini ili
kuandaa eneo la kuchomea nyama, huku Bhoke akiwa bado nyumbani akiandaa
chakula,” alisema Gibore na kuongeza:
“Wale vijana walinieleza kwamba baadaye saa 8:30 mchana, Bhoke na
wenzake walifika ukumbini na kuwakuta vijana wawili wanaofanya nao kazi
wakinywa pombe, huku wakichezea silaha aina ya bastola kujaribu
shabaha.”
“Vijana hao walifyatua risasi juu na ndipo muuaji alipompiga kichwani marehemu katika jicho na mauti yalimfika muda mfupi,” alisema.
“Vijana hao walifyatua risasi juu na ndipo muuaji alipompiga kichwani marehemu katika jicho na mauti yalimfika muda mfupi,” alisema.
Alisema baada ya hapo muuaji huyo alitoweka kisha kujisalimisha
mwenyewe katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Temeke, Chang’ombe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Engelbert Kiondo
alithibitisha mtuhumiwa huyo kujisalimisha na kisha kushikiliwa kituoni
hapo na kueleza kuwa amekuwapo hapo Jumamosi iliyopita.
Kamanda Kiondo alisema pamoja na mtuhumiwa huyo kujitambulisha kuwa
ni mfanyakazi wa Takukuru, polisi wanaendelea kuchunguza ili kubaini
ukweli wa taarifa hizo.
“Tunaendelea kumshikilia hapa na uchunguzi utakapokamilika tutamfikisha mahakamani kwa taratibu nyingine za kisheria,” alisema Kiondo.
“Tunaendelea kumshikilia hapa na uchunguzi utakapokamilika tutamfikisha mahakamani kwa taratibu nyingine za kisheria,” alisema Kiondo.
Marehemu Bhoke Ryoba alizaliwa Juni 18, 1978 katika Kijiji cha
Kiterere, Wilaya ya Tarime mkoani Mara na anatarajiwa kuzikwa kesho
kijijini kwao.
Ameacha watoto watatu; Doloresy (10), Dolrisy (4) na Dolrick Gibore ambaye ana mwaka mmoja.
CHANZO:Mwananchi.

Post a Comment