Waziri Mkuu wa Syria Wael al-Halaqi ambaye ametangaza utayari wa serikali yake kutumia mazungumzo kumaliza umwagaji wa damu |
Na Nurdin Selemani Ramadhani
Waziri Mkuu wa Syria Wael al-Halaqi ametangaza utayari wa nchi yake
kuketi kwenye meza ya mazungumzo kuangalia njia muafaka ambazo zinaweza
zikamaliza miezi ishirini na moja ya umwagikaji wa damu unaoendelea
kushuhudiwa katika Taifa hilo.
Waziri Mkuu Halaqi ametoa kauli hiyo wakati anahutubia Bunge na kusema
hawapo tayari kuona masuala ya nchi hiyo yanaingiliwa na mataifa mengine
ya kimagharibi kama ambavyo imeanza kushuhudiwa sasa.
Tamko la Waziri Mkuu wa Syria linakuja baada ya Mpatanishi wa Mgogoro
huo Lakhdar Brahimi kuonesha nia yake ya kutumia mazungumzo katika
kufikia suluhu ya machafuko yanayogharimu uhai wa watu wasio na hatia.
Brahimi amenukuliwa akisema iwapo pande zinazokinzana zitashindwa kuketi
mezani ni wazi kabisa nchi ya Syria itaelekea kubana na itakuwa moja ya
mataifa ambayo yameshindwa kwa sasa.
Halaqi ameeleza utayari wa serikali yake kutumia njia ya mazungumzo
ikitafsiriwa kama jibu kwa Mpatanishi Brahimi aliyezuru Syria na
kukutana na Rais Bashar Al Assad aliyesema yupo tayari kutumia njia
yoyote kuleta suluhu lakini si kwa yeye kuondoka madarakani.
Waziri Mkuu wa Syria ameenda mbali zaidi na kusema wapo tayari wa
maridhiano ambayo yanashirikisha nchi za kikanda pamoja na mataifa
yanayoguswa na kile kinachoendelea lakini si yale ambayo yamejiegemeza
kwa upinzani.
Halaqi akihutubia Bunge la Syria amesema mambo ya nchi hiyo yanastahili
kupatiwa suluhu na wananchi wenyewe na si kutegemea mataifa ya nje ndiyo
yalete suluhu ndani ya Taifa hilo.
Waziri Mkuu Halaqi ameyataka mataifa yote ambayo yanaingilia mgogoro wa
nchi hiyo uliosababisha vifo vya watu wanaokadiriwa kufikia elfu
arobaini na tano kuheshimu sheria za kimataifa kwenye hili.
Machafuko nchini Syria yalianza mwezi March mwaka 2011 kwa maandamano ya
amani yakishinikiza kuondoka madarakani kwa Rais Assad lakini baadaye
ghasia zikatawala na ndipo mapigano baina ya wapinzani na wafuasi wa
Kiongozi huyo yakazuka.
Source-kiswahili.rfi.fr
Post a Comment