Uchambuzi Wa Olle Mjengwa

 Kunradhi,kuna tatizo la kiufundi kwenye kamera ya msaidizi wa mwenyekiti,ndiyo maana makala haiwezi kusomeka vizuri kwenye gazeti.isome hapa chini

Cazorla wa Arsenal angefungiwa mechi tatu
Na Olle Bergdahl Mjengwa,
KATIKA mchezo wa mpira kuna wachezaji wengi  wanaopenda kujiangusha bila kuguswa. Wachezaji hawa wanaharibu mchezo wa mpira. Nitawapa mfano uliotokea wiki mbili zilizopita. Arsenal walicheza mechi dhidi ya Westbrom. Katika kipindi cha kwanza Cazorla alipata mpira ndani ya 18 ya Westbrom. Jonas Olsson,  beki wa Westbrom alienda kumkaba Cazorla. Olsson alijaribu kupiga mpira, lakini, Cazorla aliupeleka mpira kushoto, Olsson aliukosa mpira na ilionekana kama Olsson aliupiga mguu wa kulia wa Cazorla. Cazorla alianguka na Arsenal walipata penalti.
Marudio yalionyesha kwamba Olsson aliukosa mpira, lakini, pia marudio yalionyesha kwamba Olsson hakugusa mguu wa Cazorla na Cazorla alianguka bila kuguswa.
Inasikitisha kwamba mchezaji mzuri kama Cazorla anajiangusha makusudi ili timu yake ipate penalti. Katika mpira kwa sasa timu inaweza kushinda mechi kwa sababu mchezaji wao anajiangusha ndani ya 18 na refa anaamua ipigwe penalti.
Msimu huu FA kwa kweli wamejaribu kuwapunguza wachezaji wanaojiangusha katika ligi ya Uingereza. Msomaji utakuwa unajua, kwamba wachezaji wengi katika ligi ya Uingereza msimu huu wamepata kadi ya njano kwa sababu wamejiangusha.
Mara nyingi katika ligi ya Uingereza  marefa wamefanya vizuri kuwapa kadi za njano wachezaji wanaojiangusha. Lakini, mara kwa mara,  na hasa katika msimu huu, marefa wamekosea na wametoa kadi ya njano kwa wachezaji ambao kweli wamechezewa  faulo na hawakujiangusha. Kwa mfano,  Torres alipata kadi njano ya pili katika mechi dhidi ya Manchester United msimu huu. Lakini, marudio yalionyesha kwamba Torres kweli alichezewa faulo na Johny Evans.
Marefa wengine pia wamefanya kosa la kuwapa mipira ya adhabu kuelekea timu za upinzani  wachezaji ambao wamejiangusha kwa makusudi. Mwezi huu fainali za Kombe la Dunia la vilabu zinafanyika nchini Japan.
Na kwa mara ya kwanza katika historia ya mpira wa miguu ‘Goal line technology’- teknolojia ya mstari wa goli  itatumiwa. Bado hatuna teknolojia ambayo inaweza kuona kama mchezaji amejiangusha kwa makusudi. Lakini,  mimi nafikiri , kama mchezaji anajiangusha ndani ya 18 au nje ya 18, na refa anampa penalti au faulo, na marudio yanaonyesha kwamba mchezaji huyo kweli alijiangusha, basi, nafikiri  mechi ikiisha , mchezaji huyo angepata kadi nyekundu na angefungiwa mechi 3.
Kama mchezaji anamwambia mchezaji mwingine neno la kibaguzi katika mechi,  na refa haoni, mchezaji huyo bado atafungiwa mechi kadha kama timu ya upinzani inawasilisha rasmi malalamiko. Kwa mfano, msimu uliopita Suarez alimwambia Evra neno la kibaguzi katika mechi dhidi ya Man U katika FA cup. Mechi ilipoisha,  Evra alilalamika rasmi, na marudio yalionyesha kwamba Suarez kweli alimwambia Evra neno la kibaguzi. Suarez alifungiwa mechi 8.
Naamini kwamba kama wachezaji wangepata kadi  nyekundu kama wanajiangusha makusudi , na kama wanaweza kufungiwa hata kama refa hajaona,  lakini, marudio yameonyesha kwamba wamejiangusha,  basi,  wachezaji wachache sana wangeendelea na tabia huyo ya kujiangusha makusudi.

Post a Comment

Previous Post Next Post