ADAI HAWATAFUTI UMAARUFU BALI WANAPINGA DHULUMA
KATIBU Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa,
amesema suala la gesi asili linaleta mvutano kwa sababu ya maslahi ya
watu wachache.
Watu
wanaoendekeza mgogoro katika sakata hilo ni wale waliofilisika kifikra,
hawajui Katiba na hawajui kuwa wananchi ndio walinzi wa kwanza wa
rasilimali zao.
Alisema kuwa
wanaokuja na hoja ya kusema ni siasa, wanakurupuka kwani wao kama
wanasiasa ni lazima kupiga kelele kupinga dhuluma inayotaka kufanywa na
serikali dhidi ya wananchi hao.
Akizungumza
na Tanzania Daima juzi, Dk. Slaa, alisema Katiba ya nchi pamoja na
udhaifu iliyonao, imeainisha vema misingi ya kusimamia rasilimali za
taifa kwa usawa bila ubaguzi wala dhuluma.
Alisema kuwa
katika suala hilo hawatafuti umaarufu wowote wa kisiasa, na hivyo
kuhoji ni nani anaweza kutafuta umaarufu katika shida za watu?
Dk. Slaa
aliongeza kuwa Mtwara ni sehemu tu ya Tanzania, hivyo wananchi wa huko
na Lindi wana haki ya kunufaika na rasilimali iliyopatikana kwao.
“Serikali
inasisitiza kujenga mitambo Kinyerezi kwa kuwa wanataka kuleta gesi hiyo
Dar es Salaam ili kunufaika wao kwanza, jambo ambalo ni la kiubaguzi,”
alisema.
Kwa mujibu
wa katibu huyo, serikali ingekuwa wazi kwa kuwaambia wananchi inalinda
Katiba ipi; maana iliyopo inawapa wananchi haki ya kulinda rasilimali
zao na kunufaika nazo.
Alifafanua
kuwa mkazo unaopaswa kuwepo kwa maendeleo ya taifa, unazungumzia kuondoa
maadui watatu yaani ujinga, maradhi na umaskini.
“Wananchi wa
Mtwara ni maskini, mkoa wao umetelekezwa muda mrefu, wamekopwa korosho
yao, sasa wamepata gesi na wanayo haki ya kudai wanufaike nayo ili nao
wapate viwanda, shule na hospitali nzuri,” alisema.
Dk. Slaa
alisema mikoa hiyo haijawahi kuwa na hospitali ya rufaa, hivyo wanaionya
serikali isiendeshe shughuli za uchumi kwa maslahi ya watu wachache.
Alisisitiza
kuwa hakuna sababu za kutokuwekeza mitambo ya gesi Mtwara na Lindi ili
isaidie ukuaji wa maeneo hayo kiuchumi na kwamba jambo hilo wala halina
siasa.
Alisema ni
jukumu la kila mwananchi kulinda utajiri wa taifa lake kwani wao ndio
wamiliki, hivyo hawapaswi kutegemea hisani ya serikali na badala yake
serikali inapaswa kuwajibuka kwao.
Kauli hiyo
ya Dk. Slaa inakuja siku chache baada ya Waziri wa Nishati na Madini
kuwabeza wananchi wa Mtwara walioandamana wakiongozana na baadhi ya
wanasiasa kupinga usafirishwaji wa gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es
Salaam.
Desemba 27,
wananchi wa Mtwara waliandamana kupinga hatua ya serikali kutaka
wasafirishe gesi hadi Dar es Salam na kuwaacha wao wakiwa hawana kitu.
Januari 2,
Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, akizungumza na
waandishi wa habari alipinga hatua hiyo ya wananchi na kusema jambo hilo
limevamiwa na wanasiasa.
“Hiyo gesi
inayowafanya wanasiasa wawashawishi wakazi wa Mtwara kuandamana haiko
Mtwara wala Lindi, bali iko katika mipaka ya Tanzania ndani ya kina
kirefu cha bahari na kwa hilo kila Mtanzania ana haki ya kutumia,”
alisema.
Waziri
Muhongo alisema ni jambo la kusikitisha kuona wakazi wa Mtwara
wakiandamana kwa ajili ya gesi wakati walipa kodi wa Tanzania
hawajaandamana kwa ajili ya rasilimali zinazotoka maeneo mengine kwenda
kutumika Mtwara.
Alikwenda mbali na kulaumu kile alichokiita wanasiasa kujiingiza katika sakata hilo na kuwahimiza wananchi waandamane.
Post a Comment