Kampuni 1,000 kuhudhuria mkutano wa nishati Arusha


Na Baltazar Nduwayezu,EANA
Zaidi ya watu 1,000 kutoka Afrika Mashariki na sehemu nyingine duniani wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa wa siku tatu wa Nishati ya Petroli na Maonyesho utakaofanyika mjini Arusha, kati ya Februari 6 na 8, 2013.

‘’Lengo kuu la Mkutano na Maonyesho ni kukuza uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi kwa kuionyesha dunia rasilimali ya nishati hiyo iliyopo katika kanda na kubadilishana taarifa juu ya hali ya uendelezaji wa sekta hiyo katika kila nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),’’ Dk. Nyamajeje Weggoro,Mkurugenzi wa Tija na Sekta ya Jamii wa EAC aliwaambia waandishi wa habari hapa juzi. 

Aliongeza kwamba mkutano huo utatoa mada mbalimbali za kiufundi zinazoonyesha maendeleo ya sekta ya mafuta ya petrol na gesi katika EAC na duniani kwa ujumla wake.

‘’Hii ni nafasi ya kipekee kwa Afrika Mashariki kuonyesha ugunduzi wa hivi karibuni wa uwepo wa mafuta na gesi na kuona ni namna gani bora ya kuweza kuchimba rasilimali hiyo katika nchi wananchama,’’ alisema Dk. Weggoro. Mkutano huo unatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais Jakaya Kikwete.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni : ‘’Kanda ya Afrika Mashariki,eneo linaloibukia kwa uwekezaji na upatikanaji wa mafuta na gesi kwa siku za usoni kwa maendeleo endelevu. 

‘’Tumechagua kauli mbiu hiyo kwa sababu upo ugunduzi mkubwa wa mafuta na gesi katika miaka miwili iliyopita Magharibu mwa Uganda na katika maeneo mengine,ugunduzi wa gesi Kusini mwa Tanzania na ukanda wa Pwani, ugunduzi mkubwa wa mafuta Kaskazini mwa Kenya na gesi pia ukanda wa Pwani wa Kenya,’’ alieleza Dk. Weggoro na kuongeza ‘’hali hii imeifanya kanda hii kuwa na mvuto wa aina yake kwa wawekezaji kutoka duniani kote.’’

Wajumbe waliothibitisha kushiriki katika mkutano huo ni pamoja na viongozi wa biashara katika sekta ya nishati,mawaziri wa shughuli za EAC, mawaziri wanaoshughulikia nishati, fedha na mipango toka nchi tano za EAC na sekta nyingine muhimu, wawakilishi toka sekta binafsi, bodi mbalimbali za kitaaluma, vyuo vikuu na kampuni kubwa za uchimbaji petroli na gesi.

Mkutano huo wa Afrika Mashariki wa Nishati ya Petroli unaofanyika kila baada ya miaka miwili ulizinduliwa rasmi mwaka 2003 na unafanyika kwa mzunguko miongoni mwa nchi wanachama.

Post a Comment

Previous Post Next Post