Mwajiriwa akifanya kazi katika Kiwanda kipya cha Karatasi AADCO huko Hargeisa. [Na Barkhad Dahir/Sabahi]
|
Na Barkhad Dahir, Hargeisa
Kiwanda ambacho huzalisha karatasi, maboksi na madaftari ya wanafunzi --
kiwanda cha kwanza kama hicho kufanyakazi nchini Somalia kwa miongo
miwili -- kilifunguliwa huko Hargeisa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kuanzisha Kiwanda cha Karatasi cha AADCO kumekuwa kukishughulikiwa tangu
mwaka 2009, mmiliki wake Aden Barado alisema katika sherehe za ufunguzi
siku ya Jumamosi (tarehe 5 Januari).
"Ilichukua muda mkubwa kwa sababu tulikuwa katika nchi iliyoharibiwa,"
Barado alisema, na kuongeza kuwa ni shida kuanzisha kiwanda nchini
Somalia ambako kuna msaada mdogo wa kurahisisha mchakato.
Kiwanda kilianza kujengwa mwezi Januari 2012 na kumalizika mwezi Disemba.
Kiwanda ina wafanyakazi 50, wakiwemo wanawake, na watu zaidi wataajiriwa
hivi karibuni, kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Teknolojia Mohamud Abdullahi
Ahmed, aliyesema kuwa baadhi ya wafanyakazi walipewa mafunzo huko
China.
Kila saa 16, kiwanda huzalisha vitabu 70,000 ambavyo viko tayari kuuzwa
sokoni, aliiambia Sabahi. Kiwanda hakiharibu mazingira kwani kinatumia
mfumo unaoweka kikomo cha kelele na moshi ya kupita kiasi, alisema.
Waajiriwa hukusanya vitabu, karatasi za
ofisini na maboksi ya ufungaji katika Kiwanda cha Karatasi cha AADCO.
[Na Barkhad Dahir/Sabahi]
Hiki ni kiwanda cha kwanza cha aina yake kufunguliwa nchini Somalia
tangu kuanguka kwa serikali kuu miongo miwili iliyopitaa, Meneja Mkuu
Hassan Nur alisema. Gharama kamili za mradi zilikuwa dola milioni 5.
Katika awamu ya kwanza, kiwanda kinapangiwa kuchapisha vitabu vya
mazoezi kwa wanafunzi, Nur aliiambia Sabahi. Katika miezi michache ya
kwanza ya mwaka 2013, pia kitazalisha karatasi za ofisi zenye ukubwa wa
A4, madaftari na maboksi ya kufungia vitu, alisema.
Katika juhudi za kuacha uagizaji wa vifaa vya kiwanda kutoka nje,
kampuni hiyo mwishoni mwa mwaka huu itazalisha malighafi zake yenyewe za
kutengenezea karatasi. "Tunaataka tujitosheleze kwa kuchapisha vifaa
ambavyo uzalishaji wetu unahitaji, ambavyo kwa sasa tunanunua kutoka
China," Nur alisema.
"Dhamiri yetu ni kuuza bidhaa zetu Somalia yote na nchi za jirani kama vile Djibouti na Ethiopia," alisema.
Kuimarika kwa hali za viwanda vya ndani
Kiwanda hiki kipya cha karatasi kitawasaidia watu katika eneo hili
kuokoa pesa nyingi ambazo wanatumia katika kuagiza vitabu na karatasi za
ofisini, alisema Mohamed Shukri Jama, mwenyekiti wa Chama cha Biashara,
Viwanda na Kilimo.
"Kitaongeza upatikanaji wa kazi, ujuzi na uwekezaji, na hayo tunayakaribisha," alisema.
Kutoka mwaka 2000 hadi 2012, alisema kuwa shirika lake lilisajili
viwanda 58 huko Somaliland ambavyo huzalisha vitu kadhaa, lakini ni 18
tu kati yao ambavyo kwa sasa vinafanya kazi. Alisema kuwa viwanda
vilivyokufa kila kimoja kilipata baina ya dola milioni 1 na 5 kutoka
wawekezaji binafsi, lakini vikashindwa kuwa vya faida na hatimaye
kufungwa.
Alisema hali hasi, kama vile ukosefu wa msaada wa serikali, upatikanaji
mikopo na msaada wa kiteknolojia, kunaweza kukwamisha uzalishaji wa
ndani. Ili kusaidia uzalishaji wa ndani, kodi zinapaswa kuongezwa kwa
vitu vinavyoagizwa kutoka nje ili watu wanunue bidhaa zilizozalishwa
ndani, alisema.
Waziri wa Biashara, Viwanda na Utalii Abdirizak Khalif Ahmed, ambaye
alihutubia sherehe za ufunguzi, alisema kuwa wizara yake inapanga
kufanya hivyo. Ahmed alisema kuwa karibuni alipeleka kwa Wizara ya Fedha
mpango wa kuongeza kodi kwa bidhaa za kuagizwa ambazo ni sawa na bidhaa
zilizotengenezwa ndani ili kusaidia na kulinda utengenezaji.
Rais wa eneo la Somaliland Ahmed Mohamed Silanyo alikata utepe katika
sherehe hizo, na kuahidi kuwa utawala wake imejitolea kukuza uwekezaji
katika eneo hilo na kuongeza upatikanaji wa kazi kupitia msaada wa sera
na ufundi.
Chanzo: sabahionline.com
Post a Comment