MTWARA HAKIJAELEWEKA.


Kwa kile kinachoonekana kushindikana kwa suluhu juu ya mgogoro wa gesi, hali inaonekana kuwa bado ni tete mbali na jitihada za Waziri Mkuu kuja kutatua mgogoro hou. Baada ya taarifa yake ya majumuisho aliyoitoa juzi jioni hapa Mtwara inaonekana bado kuacha maswali mengi miongoni mwa Wananchi. Hali asubuhi ya jana imekuwa ni tofauti kidogo kulinganisha na juzi. Jana kila unapopita majadiliano na mazungumzo yao ni juu ya hotuba ya juzi ya majumuisho juu ya hoja za mgogoro wa gesi. Inaonekana watu bado wanamashaka na msimamo wa serikali.

Nimebahatika kuongea na wananchi wachache juu ya jambo hili lakini wote wameonekana kutosadiki msimamo wa Serikali kwa kile wanachodai ni propaganda za kisiasa na uhalisia wa mambo. 

Wakisisitiza katika hili walihoji; “Hivi wewe ndugu yangu, kama msimamo wa serikali ilikuwa ni kusafirisha gesi iliyosafishwa, je kipi kilkistahili kuanza kujengwa kati ya kiwanda cha kusafisha na bomba la kusafirishia gesi?” 

Mwingine akahoji; “Unawezaje kukubali kusafirisha umeme kupelekwa Songea ambako ni mbali na kushindwa kupelekwa Dar es salaam ambako ni karibu? Wapi kutakuwa na gharama kubwa zaidi? Tunajuwa janja yao ilipo kwa hiyo, msimamo wetu uko palepale kwamba kama shida yao ni umeme basi usafirishaji wa gesi kwa bomba haiwezekani. Ni kipi kinachowafanya kung’ang’ania usafirishaji huo kama si wizi?”

Kwa hakika inaonekana bado kuna jambo serikali inapaswa ilifanye zaidi ya hiki kinachoaminika ni suluhu inayotangazwa tangu juzi, kwani nadhani bado suluhu hiyo haijaingia masikioni mwa watu. Mikanganyiko ni mingi, wengi wanahoji pia juu ya sababu hasa ya Waziri Mkuu na jopu lake kubwa kuja huku; je ilikuwa ni kusikiliza hoja na misimamo ya Wanakusini au kutoa msimamo wa Serikali kwamba lazima gesi isafirishwe kwa bomba? Bado hoja ni nyingi kwa kweli.

Wananchi wamekwenda mbali zaidi na kuponda hoja kuhusu kuchelewa kumalizika kwa ujenzi wa barabara, maeneo ya Somanga. Kwani kwa mujibu wa Waziri Mkuu ni kwamba; barabara imechelewa kukamilika ujenzi wake kwa sababu ya kufariki kwa Mkandarasi. Hoja hii inapingwa kwa kuhoji kipindi tangu barabara hiyo ilipoanza kujengwa na kifo cha Mkandarasi huyo, kwamba hakuna uhusiano wowote. Wanatole mfano hapa kwamba itawezekanaje msiba ushindwe kumaliza ujenzi wa barabara kipande cha Kilometa 60 ndani ya zaidi ya miaka kumi?

Ni wazi kabisa kwamba, mbali ya taarifa zinazotolewa juu ya kumalizika kwa mgogoro huu lakini ukweli ni kwamba hali bado ni tete na kunahitajika busara zaidi kutafakari jambo hili zaidi ya kusimamia misimamo ambayo itatuletea matatizo. Inatupasa tutafute suluhu ya kudumu ili hata kile kinachotegemewa kufanywa kiweze kuleta tija kwa nchi yetu na si machafuko.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Wabariki Watanzani.

Hassani Samli,
Mtwara.
+255717340671

Post a Comment

Previous Post Next Post