| Kiongozi wa Kisiasa wa Kundi la Waasi la M23 Jean-Marie Runiga akishuka kwenye gari tayari kwa kuzungumza na waandishi wa habari huko Bunagana |
Na Nurdin Selemani Ramadhani
Kundi la Waasi la M23 ambalo linapambana na Serikali ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo DRC limetishia kujiondoa kwenye mazungumzo ya
kusaka suluhu ya mgogoro ambao unaendelea Mashariki mwa Taifa hilo iwapo
serikali itashindwa kusaini makubaliano ya kuweka silaha chini.
Waasi wa M23 wamemtaka Rais Joseph Kabila wa Kabange kusaini makubaliano
hayo ili ujumbe wao urejee kwenye meza ya mazungumzo ambayo
yanatarajiwa kuanza hii leo nchini Uganda baada ya kusitisha kwa majuma
mawili kupisha sherehe za mwishoni mwa mwaka.
Kiongozi wa Kisiasa wa Kundi la Waasi la M23 Jean-Marie Runiga Lugerero
ndiye ametangaza msimamo wao wa huenda wakajitoa kwenye mazungumzo ya
huko Kampala kama serikali haitasaini makubaliano na Kundi hilo ya
kusitisha mapigano katika eneo la Mashariki.
Runiga amewaambia wanahabari kwenye mkutano wake ambao umefanyika eneo
la Bunagana kwenye mpaka wa DRC na Uganda watakuwa tayari kupeleka
ujumbe wao kampala iwapo serikali itakubaliana na pendekezo lao kinyume
na hapo hawatoshiriki.
Kiongozi huyo wa M23 akizungumza kwa kujiamini amesema serikali ya
Kinshasa ndiyo inayokwamisha mazungumzo hayo kuweza kufikia muafaka
kutokana na kutokuwa tayari kusaini makuabaliano hayo ya kusitisha
mapigano.
Runiga amekiri kundi lake lina nia ya dhati ya kuhakikisha mazungumzo
hayo yanafanikiwa lakini serikali ndiyo kikwazo kwa sasa na kama
iataendelea na msimamo wao ni wazi wanaweza wakauchukua tena Mji wa Goma
kama walivyofanya mwezi Novemba.
Msemaji wa Serikali ya Kinshasa Lambert Mende ametupilia mbali madai ya
Kundi la Waasi la M23 huku akisema wamekosa hoja za msingi na badala
yake wameanza kutafuta sababu za kujiondoa kwenye mazungumzo hayo.
Hii ni mara ya pili kwa serikali ya Kinshasa na Kundi la M23 kurejea mezani kwa mazungumzo baada ya mazungumzo ya awali yaliyoandaliwa huko Kampala kugonga mwamba kutokana na kila upande kung'ang'ania agenda zao.
Kundi la M23 linaongozwa na Bosco Ntaganda ambaye anasakwa na Mahakama
ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita ICC limekuwa kitisha cha usalama
katika eneo la Mashariki mwa DRC na kusababisha watu 800,000 kuyakimbia
makazi yao.
Chanzo: kiswahili.rfi.fr
Post a Comment