Ndege 3 za Serikali zaenda kwa Milioni 1.5/-

(picha: MillardAyo.com)

Waziri wa Kilimo na Chakula na Ushirika, Christopher Chiza ameelezwa kuwa ndege ndogo tatu za Taasisi ya Serikali kupitia Wizara ya Kilimo zilizokuwa zikitumika kunyunyizia dawa ya wadudu zimeuzwa kwa jumla ya shilingi milioni moja u nusu kutokana na ukosefu wa vipuri.

Waziri alipokea taarifa hiyo iliyowasitusha watu wengi wakiwemo viongozi alioongozana nao alipokwenda kukagua shughuli za taasisi hiyo katika karakana iliyopo Arusha.

Afisa Mfawidhi wa taasisi hiyo Gideon Magusi alisema ndege hizo aina ya 5H-MRP Piper Super Cable na Cessna 145 zilianguka kwa nyakati tofauti.

Alisema ndege moja ilianguka Sitalike, Mpanda mwaka 1986 na nyingine ilianguka katika kiwanja cha ndege Mwanza 1992 ikiwa katika safari ya kikazi ya kudhibiti ndege aina ya Kweleakwelea, na ndege nyingine ilianguka Igunga, Tabora wakati wa operesheni ya kudhibiti nzige.

Baada ya kufanya utaratibu wa kulipwa fidia na shirika la bima la Taifa, NIC. Hata hivyo NIC kupitia kwa Katibu mkuu wa Wizara ya Kilimo, ililipa fidia ya shilingi laki tano kwa kila ndege na kuchukua mabaki, hivyo Serikali ilipata shilingi milioni moja na laki tano kwa ndege zote tatu.

Kutokana na taarifa hiyo, Chiza aliyeonesha kuchukizwa, aliagiza kuwa ndege zote zinazomilikiwa na taasisi hiyo zikiwepo mpya na zitakazonunuliwa, kukatiwa bima kubwa na inayokidhi.

Alisema ni jambo la kushangaza kuwa kampuni zilizokuwa zikikodi ndege hizo zilipwa fedha nyingi kupitia NIC huku Serikali ikiambulia shilingi laki tano.
 

Post a Comment

Previous Post Next Post