Ndugu zangu,
Miongoni mwa viongozi
waliopata kuongoza dola ya Kiislam, hususan baada ya Mtume Muhammad
(SAW) , na baada ya masahaba, ni Amir Muuminina Khalifa Umar bin
Abdulaziz.
Wanazuoni wa Kiislam
wanatwambia, kuwa utawala wa Khalifa Umar bin Abdulaziz ulijaa uadilifu.
Si kwa viongozi tu, hata kwa raia wake.
Inasemwa, kuwa moja ya
mafanikio makubwa ya utawala wa Khalifa Umar bin Abdulaziz ni kukusanya
zakka. Katika Uislam, zakka ni ibada ya lazima kwa mwenye nacho kuwapa
masikini, yatima, wajane, wasafiri, raia na wengineo wenye kuhitaji.
Watu walijengewa imani
kubwa, kiasi hakuna aliyethubutu kukwepa kutoa zakka. Hata wale
waliopokea zakka walikuwa waadilifu, hawakupokea zakka mara mbili kama
walishapokea kabla. Wote waliostahili kupata zakka , walipata zakka.
Hakika, zakka zilitolewa zikajaa mabohari.
Siku moja raia mmoja
alikwenda kwenye ofisi ya Khalifa Umar bin Abdulaziz. Wakati wa maongezi
yao, Khalifa Umar alikuwa akihangaika kuupuliza na kuuzima mshumaa
mmoja na kuwasha mwingine.
Alikuwa na mishumaa miwili
mezani. Kadri mazungumzo yalivyoendelea, Umar aliendelea kufanya hivyo.
Alipuliza mshumaa mmoja ukazimika, kisha akawasha mwingine.
Jambo hilo lilimstaajabisha sana mgeni wa Khalifa Umar bin Abdulaziz. Akauliza;
“Je, ni kwa nini unazima mshumaa huu na kuwasha mwingine, kisha huo nao unauzima na kuwasha ule wa kwanza?
Khalifa Umar bin Abdulaziz akamjibu;
“Mshumaa huu ni wa
Serikali, wewe unaponiuliza habari za Serikali nauwasha. Lakini, naona
mara unauliza habari za familia yangu, ndio maana nauzima wa Serikali na
nauwasha mshumaa wangu mwingine nilioununua kwa pesa za mfukoni mwangu.
Nachelea nisije fanya dhuluma kwa mali ya nchi.”
Ndugu zangu,
bila shaka, hicho ni kisa chenye kutupa mafundisho muhimu juu ya dhana nzima ya Maadili katika Utumishi wa Umma.
Tafakari.
Tafakari.
Na hilo ni Neno La Leo.
Post a Comment