UTAFITI mpya wa kitabibu umebaini kuwa saratani ya shingo ya
kizazi, inasababishwa pamoja na mambo mengine na ngono kama ilivyo kwa
ugonjwa wa Ukimwi, madaktari bingwa wa magonjwa ya maradhi hayo
wamesema.
Hayo yalielezwa na daktari bingwa wa uchunguzi wa
magonjwa katika Kitengo cha Patholojia katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili, Dk Henry Mwakyoma na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani
katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk Crispin Kahesa.
Madaktari hao wametaja mambo mengine yanayoweza
kusababisha saratani ya shingo ya kizazi kuwa ni kujiingiza kwenye
mapenzi katika umri mdogo, kuolewa mara nyingi, kuwa na wapenzi wengi,
kusafisha sehemu za siri kwa bidhaa zenye kemikali na kuzaa mara nyingi.
Katika kiwango cha kimataifa, wastani wa mwanamke kuzaa bila kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa wa saratani, ni watoto wanne.
Dk Mwakyoma alisema saratani ya shingo ya kizazi
inatokana na aina 40 ya virusi, aina mbili ikiwa ni virusi vinavyosambaa
kwa njia ya ngono... “Human papilloma virus (HPV) Squamos cell
carcinoma kirusi namba 16 na Adenocarcinoma namba 18, ni kati ya virusi
40 vinavyosababisha saratani ya kizazi na vyenyewe vinachangia tatizo
hilo kwa asilimia 70.”
Alisema saratani ya uzazi ndiyo inayoongoza
ikilinganishwa na nyingine nchini na asilimia 80 ya wagonjwa,
wameambukizwa kwa ngono.
“Saratani hiyo husambaa kwa ngono kutoka mwanamke
mmoja kwenda kwa mwingine. Mwanamke mwenye saratani ya kizazi akifanya
ngono, mwanamume huchukua virusi na kumwambukiza mwingine atakayefanya
naye ngono,” alisema na kuongeza:
“Wagonjwa wengi na wale ambao tayari wana
maambukizi, wamekuwa wakikutwa na virusi hawa wa aina mbili ambao
wamekuwa wakienezwa zaidi kwa njia ya zinaa. Inawezekana mwanamume akawa
ametoa kirusi kwa mwanamke mmoja kwenda kwa mwingine.”
“Hata hivyo, kuna wanaume ambao tayari wameshakuwa
na maambukizi ya HPV wanatembea na virusi, hawa tunawaita (high risk
sexual male patner) wanaume hawa utakuta kila akioa mke anakufa kwa
saratani ya shingo ya uzazi, lakini kamwe virusi hao hawawezi kumwathiri
yeye.”
Alisema kuanza ngono mapema nako kunachangia kwa
kiasi kikubwa maambukizi ya saratani hiyo, kwani binti anakuwa katika
hatari zaidi ya kupata maambukizi mapema na hivyo kuweza kumwathiri
mapema zaidi, tofauti na yule aliyeanza baadaye.
“Idadi kubwa ya wanawake wamekutwa na saratani
mapema sana, ukilinganisha na umri wao, lakini wengi wao wamekuwa
wakikutwa na ugonjwa huu kuanzia umri wa miaka 35 kwenda juu. Hii
inamaanisha kuwa walipata maambukizi hayo walipokuwa na miaka 20-25.”
Dk Mwakyoma alisema licha ya hivyo mgonjwa anaweza
asitambue tatizo hilo mpaka miaka 10 hadi 15 baadaye ambapo tatizo
linajitokeza hadharani.
Chanzo: Mwananchi.
Chanzo: Mwananchi.
Post a Comment