NI YANGA NA PRISONS, SIMBA NA LYON J'PILI

TIMU kongwe za soka nchini, Simba na Yanga zimepangwa kuanza mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara kwa kumenyana na African Lyon na Prisons.

Wakati Simba itashuka dimbani Jumamosi kumenyana na Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga itashuka dimbani siku inayofuata kwenye uwanja huo kuvaana na Prisons.

Ratiba ya mzunguko huo iliyotolewa jana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inaonyesha kuwa, mechi zingine zitakazochezwa Jumamosi ni kati ya Mtibwa na Polisi (Manungu), Coastal Union na Mgambo Shooting (Mkwakwani), Ruvu Shooting na JKT Ruvu (Mlandizi), Azam na Kagera Sugar (Chamazi) na Oljoro JKT na Toto African (Sheikh Amri Abeid).

TFF imetangaza ratiba hiyo baada ya timu zote zinazoshiriki ligi hiyo kufuta mgomo wa kususia mechi za mzunguko wa pili kutokana na kutolipwa fedha za nauli na wadhamini, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom.

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, klabu zote 14 zimekubali kuendelea na mzunguko huo baada kufanyika kwa kikao cha pamoja na Kamati ya Ligi ya TFF.

Wambura alisema kikao hicho kilifanyika Januari 21 mwaka huu na kamati iliweka masharti kadhaa kabla ya kuendelea na ligi hiyo.

Alisema masharti hayo yanatokana na fedha za nauli kwa ajili ya klabu zilizotolewa na Vodacom kuchukuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Fedha hizo ni sh. milioni 157.

Wambura alisema masharti hayo yatawasilishwa na Kamati ya Ligi kwa maandishi kwa Katibu Mkuu wa TFF na nakala kupelekwa kwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Awali, klabu zilitishia kutoshiriki mzunguko wa pili wa ligi hadi fedha hizo zitakaporejeshwa na TRA.

Katika hatua nyingine, mzunguko wa pili wa michuano ya ligi daraja la kwanza unatarajiwa kuanza kutimua vumbi Februali 2, huku timu ya Small Kids ya Rukwa ikiondolewa na kushushwa daraja.

Wambura alisema timu hiyo imeshushwa daraja kwa mujibu wa kanuni baada ya kushindwa kucheza mechi mbili katika mzunguko wa kwanza na matokeo yote ya mechi, ambazo ilicheza katika mzunguko huo wa kwanza yamefutwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post