
ASEMA KAULI ZA WAZIRI MUHONGO NI HATARI
NAIBU Katibu
Mkuu wa Chadena, Kabwe Zitto, na wenyeviti wa vyama vya CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba, na James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, wameishukia serikali
wakisema inaweweseka kutokana na kauli ya Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo, kukinzana na mkakati wa serikali.
Hatua hiyo
inakuja siku moja tangu Waziri Muhongo akutane na waandishi na
kuwakejeli wananchi wa mikoa ya kusini hususan Mtwara kuwa hawakupaswa
kuandamana kupinga mpango wa serikali kusafirisha gesi kutoka huko
kwenda Dar es Salaam kwa kuwa rasilimali ni za Watanzania wote.
Waziri
Muhongo alidai kuwa wananchi wa Mtwara wanashawishiwa na wanasiasa ili
kufanya vurugu ilhali gesi nyingi haiko kwao bali iko kwenye mipaka ya
nchi baharini kwenye kina kirefu na kuongeza kuwa hata wao wamekuwa
wakinufaika na rasilimali za mikoa mengine.
Katika
taarifa yake, Zitto alisema kuwa mkuu wa mkoa wa Mtwara aliwaita
Watanzania wa mkoa huo wahaini, wapuuzi na watu hatari huku Rais wa
Jakaya Kikwete naye akiingia kwenye mjadala huo kwa kuonya watu
wanaowaunga mkono wawanachi hao akiwaita watafuta umaarufu wa kisiasa na
wanataka kuigawa nchi.
“Siku moja
baada ya hotuba ya Rais, Waziri Muhongo alifanya mkutano na waandishi wa
habari kueleza suala lilelile ambalo bosi wake alilielezea usiku wa
kuamkia Mwaka Mpya 2013. Hii ni dalili ya serikali kuweweseka,” alisema.
Alisema kuwa
katika kauli ya serikali, ambayo haikuwa na jipya zaidi ya wimbo uleule
wa ‘kugawa nchi’ ‘umaarufu wa kisiasa’ serikali ilitaka kuonyesha umma
kuwa watu wa Mtwara hawana shukurani.
Kwamba miaka
yote toka Uhuru watu wa Mtwara wamekuwa wakilishwa na pamba, kahawa,
chai, tumbaku na sukari na hivyo watu wa Mtwara na Lindi hawakuchangia
hata kidogo kwenye hazina ya taifa.
“Hivyo wao
kupigia kelele gesi yao ni uchoyo na roho mbaya na kukosa shukurani.
Kauli ya serikali ni kauli ya chombo kinachoendelea kukosa uhalali wa
kuongoza taifa. Ni kauli ya kukata tamaa. Ni kauli hatari sana dhidi ya
Watanzania waliojitolea damu kulinda uhuru wa nchi yao.”
Zitto
alifafanua kuwa serikali katika kauli yake haitaji kabisa kwamba toka
Uhuru watu wa Mtwara na Lindi wamekuwa wachangiaji wakubwa sana katika
uchumi wa taifa kupitia zao la korosho.
Alisema
takwimu za uzalishaji wa korosho zinaonyesha kwamba kuanzia mwaka 1965
mpaka 2011 zimeliingizia taifa fedha za kigeni jumla ya dola za
Kimarekani bilioni 4.58.
Katika mwaka
wa uchumi unaoishia Novemba 2012, korosho imeliingizia taifa jumla ya
dola za Kimarekani 151 milioni. Katika mwaka 2011 zao hili liliingiza
dola milioni 130 wakati pamba iliingiza dola 53 milioni tu.
Zitto
alihoji kuwa tunaipima kwa fedha? Uroho wa gesi asilia kuzalisha umeme
wa kufurahisha walalaheri asilimia 14 nchini ndio inaifanya serikali
kusahau kabisa kujitoa muhanga kwa watu wa Mtwara katika kulinda uhuru
wa taifa letu?
Kwamba
serikali kusema lazima bomba lije Dar es Salaam kwa sababu ndiyo
inazalisha asilimia 80 ya mapato ya serikali ni uongo na aibu serikali
kujitetea kwa uongo.
“Dar es
Salaam ni kituo tu cha kukusanyia mapato ya serikali. Uzalishaji mkubwa
wa nchi yetu wenye kuzalisha kodi unafanyika nje ya Dar es Salaam.
Walipa kodi wakubwa wengi ofisi zao kuu ziko Dar es Salaam lakini
uzalishaji wao unafanyika nje ya Dar es Salaam.
Serikali itoe orodha ya walipa kodi wakubwa 100 tuone uzalishaji halisi wa mapato hayo unafanyika wapi,” alihoji.
Zitto
alisistiza kuwa maandamano ya watu wa Mtwara ni kielelezo tosha kwamba
watu wa mikoa ya Lindi na Mtwara wamechoshwa na longolongo za serikali.
Alisema kuwa
watu wa Mtwara na Lindi wameona historia ya bomba la Songosongo. Hata
kodi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa (asilimia 0.3) ilikuwa inalipwa
na Halmashauri ya Manispaa Ilala na kampuni ya Pan Africa Energy.
Lipumba, Mbatia wanena
Akizungumza
na gazeti hili, Profesa Lipumba alisema anashindwa kumwelewa Waziri
Muhongo, hajui hali halisi ya maeneo ya Watanzania, kama hawezi kusema
gesi iko maeneo gani katika mikoa ya Tanzania, basi ni profesa wa ajabu
kidogo.
Alifafanua kuwa anashindwa kumwelewa kwani anapingana na sera ya serikali ambayo yeye mwenyewe ni waziri.
Alisema kuwa
kama gesi ilipoanza kuchimbwa Songosongo likajengwa bomba dogo la nchi
12 kusafirisha gesi chini ya bahari toka Songosongo hadi Somanga na
bomba la nchi 14 lilijengwa toka Somanga hadi Dar es Salaam.
“Uwezo wa
mabomba haya ni mdogo ukilinganisha na gesi inayopatikana Songosongo na
mahitaji yake kwa shughuli ya kufua umeme na kutumia viwandani,”
alisema.
Alisema kuwa
mpango huu ulikubaliwa na serikali na ukaingizwa katika Mpango Kabambe
wa Taifa wa kufua na kusambaza umeme, kwamba mradi huo wa kufua umeme MW
300 Mtwara ulipangwa uwe umekamilika mwaka huu wa 2012.
Lipumba
aliongeza kuwa wananchi wa Mtwara wanahitaji kujua kwa nini serikali
haikutafuta njia mbadala ya kugharamia mpango wa kufua umeme na
kuiunganisha Mtwara na gridi ya taifa.
Naye Mbatia
akizungumza na waandishi wa habari alisema kuwa anashangazwa na viongozi
wa CCM wanaposhindwa kuwa na sauti moja ya kusimamia rasilimali za
taifa na hivyo kuparaganyika na kupishana kauli katika suala la gesi.
“Hatuhitaji
viongozi wa kuuliza Watanzania tunataka nini, Watanzania wote tunataka
kushirikishwa hasa katika masuala ya rasilimali ya gesi, maumivu ya
mikataba mibovu katika sekta ya madini na sekta nyingine
imetuchosha,”alisema.
Naye
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Helen Kijo-bisimba,
pamoja na Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania, Ussu Mallya,
walisema wananchi hawana tatizo isipokuwa serikali haijawashirikisha
kwani wanajua kuwa mikoa yao imeachwa nyuma muda mrefu bila maendeleo.
Post a Comment