SERIKALI imeingilia kati sakata la uchaguzi wa Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) kwa kuamuru kufutwa kwa katiba ya sasa ya shirikisho hilo
na badala yake kuamuru itumike katiba ya zamani (mwaka 2006) baada ya
kubaini kuwa iliyopo ina kasoro nyingi.
Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari leo, Wizara ya Habari,
Utamaduni, Vijana na Michezo imeeleza kuwa katiba ya sasa ya TFF si
halali. Imeelezwa vilevile kuwa msajili wa vyama vya michezo aliyedaiwa
kuipitisha katiba hiyo ameondolewa.
Mchakato wa uchaguzi mkuu wa TFF umesimamishwa kutokana na mgogoro
mzito uliotokana na kuenguliwa kiutata kwa wagombea kadhaa, wakiwamo
Jamal Malinzi anayewania urais na Michael Wambura anayetaka kugombea
nafasi ya makamu wa rais.
Kamati ya rufani ya TFF inayoongozwa na Iddi Mtiginjola ndiyo
iliyozua balaa lote la sasa baada ya kuwaengua kina Malinzi na mwishowe
kumuacha makamu wa sasa wa rais, Athumani Nyamlani abaki kuwa mgombea
pekee.
Hata hivyo, tayari mchakato wa uchaguzi huo uliozua mabishano makali
umeshasimamishwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na maafisa wa
chombo hicho cha juu cha mchezo wa soka duniani wameshaanza kuwasili
kufuatilia kinachotokea nchini.
Uamuzi wa serikali wa kufuta katiba ya sasa na kutaka itumike ya 2006
unampa ahueni kubwa Wambura ambaye alishasema hadharani kuwa
ataiburuza TFF mahakamani kama isipoachana na katiba mpya na kufuata ya
zamani; huku akitoa sababu kadhaa za kupinga matumizi ya katiba mpya,
mojawapo ikiwa ni kupitishwa kwake kwa njia ya waraka wa barua pepe
(e-mail) kwenda kwa wajumbe badala ya kufuata maelekezo ya katiba
yanayotaka mabadiliko kufanywa na wajumbe kupitia mkutano mkuu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taratibu za FIFA, ni marufuku kwa shughuli
za soka kuingiliwa na serikali au mahakama na nchi yoyote inayokwenda
kinyume na taratibu hizo hujikuta ikifungiwa kama ilivyowahi kutokea
nchini Kenya.
(CHANZO: straikamkali.blogspot.com)
Post a Comment