MBUNGE wa
Ubungo Jijini Dar es Salaam (Chadema), John Mnyika amemtaka, Rais Jakaya
Kikwete kutosaini marekebisho ya sheria mpya ya mabadiliko katika
Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya 2008.
Mnyika pia
anakusudia kukata rufaa juu ya uamuzi wa Spika wa Bunge, Anne Makinda
kwa kutumia vibaya kanuni za Bunge kutokana na kitendo chake cha
kuzivunja kamati tatu za Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu za
Serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu za Serikali Kuu (PAC).
Akizungumza
na Mwananchi Jumapili, jana, Mnyika alisema Rais Kikwete kabla ya
kusaini marekebisho hayo ambayo yanaonyesha dalili za kuwalinda
mafisadi, ajitokeze na kuwaeleza Watanzania faida na hasara ya
mabadiliko ya sheria hiyo.
Wiki hii
Serikali iliwasilisha bungeni mapendekezo ya mabadiliko katika Sheria ya
Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya 2008, huku ikiongeza vifungu ambavyo
vinapunguza nguvu ya Bunge katika kushughulikia taarifa ya Ofisi ya
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Marekebisho
hayo yamo kwenye Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria, namba tatu
wa mwaka 2012 uliowasilishwa bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Jaji Frederick Werema.
Marekebisho
hayo yanapendekeza kubadili utaratibu mzima wa kushughulikia taarifa
hiyo, kwani yanaongeza vipengele, vinavyoliwajibisha Bunge kwa Serikali.
Serikali
imeongeza vipengele vya ziada ambavyo vinazitaka kamati za Bunge
zinapofanya uchambuzi wa ripoti ya CAG, kupeleka maazimio yake kwa
Serikali ili yatafutiwe majawabu badala ya utaratibu wa sasa wa kupeleka
hesabu zake bungeni.
Mnyika
ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Nishati na Madini alisema marekebisho
hayo hayana tija kwa taifa ambalo linapigania kuwakomboa wananchi huku
likiacha mianya ya wajanja kuendelea kutumia mali za umma bila
kuchukuliwa hatua.
“Rais ndiye
mwenye uamuzi wa mwisho hivyo anatakiwa kutambua kuwa marekebisho hayo
ambayo yako mikononi mwake hapaswi kuyasaini hadi pale atakapowaeleza
ukweli wananchi nia ya mabadiliko ya sheria hiyo,” alisema Mnyika.
Mnyika
amesema amemwandikia barua Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilila akimtaka
kumpatia mtiririko wa uamuzi wa Spika Makinda wakati alipotangaza
kuvunja kamati tatu za Bunge ili aweze kukata rufaa.
Alisema
amekuwa akitaka kufanyika kwa mabadiliko ya kanuni ya Bunge ya 152 (3)
inayompa mamlaka Spika kuchukua uamuzi peke yake pasipo kushirikiana na
mtu mwingine.
“Spika
Makinda amezivunja kamati tatu kwa kutumia kanuni ya Bunge 152 (3),
wakati huo huo licha ya kwamba amezivunja lakini bado zinatambulika
katika kaununi hiyo hiyo ya Bunge ya 114 (11). Sasa sijui Spika ameliona
hili au la,” alisema Mnyika.
Alisema
atatumia sheria za kanuni za Bunge 5 (4) inayompata uhuru Mbunge kukata
rufaa kama hajaridhika na uamuzi wa Spika ili hatua zaidi zichukuliwe.
Juzi Spika
Makinda alitangaza mabadiliko ya kamati za kudumu za Bunge, huku Kamati
ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) iliyokuwa ikiongozwa na Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kufutwa.
Kutokana na
mabadiliko hayo, shughuli za POAC sasa zitaendelea kufanywa na Kamati ya
Hesabu za Serikali (PAC) ambayo itaendelea na jukumu lake la msingi la
kuchambua taarifa ya CAG pia kwa Serikaki Kuu.
Mwananchi
Post a Comment