CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimehofia machafuko na umwagaji damu
unaoonekana kuendelea kwa sasa maeneo mbalimbali nchini na kusema hali
hiyo inatokana na nchi kukabiliwa na ombwe kubwa la uongozi.
Kauli hiyo
imetolewa jana na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, wakati alipokuwa
akifungua kikao cha Baraza la Viongozi wa CHADEMA Kanda ya Ziwa
Magharibi, kilichofanyika jijini Mwanza, kisha kuhudhuriwa na wajumbe
kutoka kanda hiyo inayoundwa na mikoa ya Geita, Mwanza na Kagera.
Alisema hali
ya nchi kwa sasa si shwari ikilinganishwa na enzi za nyuma za utawala
wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kwamba kuna bomu
linaloweza kulipuka muda wowote kutokana na baadhi ya mambo, likiwamo
suala la matokeo mabovu ya mitihani pamoja na dhana potofu ya udini
inayoonekana kuchafua hali ya hewa.
"Tanzania
bado inakabiliwa na tatizo kubwa la ombwe la uongozi. Hali ya nchi kwa
sasa si shwari...na Watanzania wote bila kujali itikadi zetu za kisiasa
tunapaswa kuungana pamoja kuinusuru nchi na machafuko yoyote yanayoweza
kutokea kwa kuiondoa CCM madarakani mwaka 2015,” alisema Mbowe katika
hotuba yake hiyo.
Aidha,
aliwahakikishia wananchi kwamba CHADEMA ni chama makini, chenye sera
thabiti na zinazotekelezeka kwa wakati tofauti na CCM, hivyo chama chake
kimejiandaa kuongoza halaiki ya Watanzania katika safari ya kuingia
Ikulu kupitia Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015, kwani nguvu ya umma
kamwe haishindwi.
Sera ya majimbo
Mwenyekiyio
huyo wa CHADEMA taifa, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai, mkoani
Kilimanjaro, alisema sera ya majimbo iliyoanzishwa na chama chake
imelenga kushusha madaraka ya kiuongozi ngazi ya chini, badala ya
madaraka hayo kubaki juu kama ilivyo kwa CCM.
Alisema
mbali na sera hiyo kulenga kushusha madaraka ngazi ya chini, pia chama
hicho kimeweka mikakati maalumu ya kuhakikisha kila kijiji na kaya 30
zinakuwa wa uwakilishi ndani ya chama, na kwamba kanda zote 10 zikiwamo
nane za Tanzania Bara na kanda mbili za Visiwani Zanzibar, ni kitanzi
kikubwa kitakachoiangamiza CCM kwenye chaguzi zijazo.
"Mkakati na
sera hii ya majimbo ni nzuri sana katika mapambano ya kusaka maendeleo
na kushusha madaraka ya uongozi ngazi ya chini. Sera hii na nyingine
kadhaa ni ya kutokea CHADEMA, na hata kama majeshi zaidi ya 1,000
yajipange vipi hayataweza kuzuia nguvu ya umma kuiingiza CHADEMA
madarakani uchaguzi ujao.
"Tunaposema
CHADEMA imejiandaa kukamata uongozi tupo kwenye mstari wa ukweli kabisa.
Tumejiandaa vizuri na Tanzania kwa sasa inahitaji tiba maalumu ambayo
ni kuing'oa CCM madarakani,” alisema mwenyekiti huyo wa CHADEMA.
Alisema
chini ya sera hiyo, chama kitaunda kamati za utekelezaji ngazi hizo za
chini, kuwa na waratibu wa kila kanda husika watakaowajibika kuratibu
shughuli zote na ukusanyaji wa rasilimali watu, kuwa chombo cha maamuzi
ngazi hizo na baadaye rufaa yake kuwasilishwa makao makuu pale
inapobidi.
Hata hivyo
alionya kwa kusema kwamba kamwe hawatakubali uendawazimu wowote ule
kuona CHADEMA inadondoka katika jukwaa la kisiasa, kwani kwa sasa
asilimia kubwa ya Watanzania wanaitegemea na kuiunga mkono, kwani
ikishuka itawagharimu wananchi kwa miaka 20 kutafuta chama kingine
chenye nguvu kama CHADEMA.
Vyombo vya habari
Katika
hotuba yake hiyo ya ufunguzi wa Baraza la Viongozi wa Kanda ya Ziwa
Magharibi, Mbowe alivishukia baadhi vyombo vya habari na waandishi wake
hapa nchini, ambapo alisema vipo baadhi yake vikiwamo vinavyomilikiwa na
serikali au CCM vimekuwa vikificha ukweli wa mambo hata pale jamii
inapohitaji kupata uelewa wa jambo fulani.
Alisema
ukwepeshaji wa ukweli huo kwa umma ni sawa na kuwadhulumu au kuwanyima
haki wananchi kupata habari kwa mujibu wa katiba ya nchi, na alivitaka
vyombo hivyo kuhakikisha vinawatendea haki wananchi kwa kueleza ukweli
wa jambo, ikiwa ni pamoja na kuwakosoa watawala pale wanapokwenda
kinyume cha matakwa halisi ya wananchi.
"Waandishi
wa habari ni watu muhimu sana katika maendeleo ya nchi. Lakini kuna
baadhi ya waandishi wa habari na vyombo vyao wamekuwa wakipindisha
ukweli kwa kusema uongo! Na hata kwenye uongo waandishi na vyombo hivi
wanadiriki kuwaaminisha wananchi kwamba ni jambo la kweli.
"Suala hili
si zuri hata kidogo. Najua vipo baadhi ya vyombo vinavyomilikiwa na
wanasiasa au na serikali vinaegemea upande wa watawala kisha kushindwa
kufanya kazi zake vizuri za kuuhabarisha umma habari njema na zenye
ukweli mtupu. Vyombo hivi tunavitaka navyo vibadilike, muda ndio huu
CHADEMA inaelekea Ikulu,” alisema Mbowe.
Hata hivyo,
Mbowe alitoa wito kwa wanachama, viongozi wa chama pamoja na wananchi
wote kwa ujumla, kuunganisha nguvu pamoja katika kusaka mabadiliko ya
kisiasa yatakayowakomboa Watanzania kutoka katika umaskini unaoonekana
kushindwa kuondolewa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Post a Comment