NEWZ:- MKUU WA WILAYA YA TANGA HALIMA DENDEGO AMEWAJIA JUU BAADHI YA ASKARI

Mkuu wa Wilaya ya Tanga HALIMA DENDEGO amewajia juu baadhi ya Askari wa Kitengo cha Usalama Barabarani ambao wamekuwa wakishawishi na kupokea rushwa huku wakijua kwamba kufanya hivyo ni makosa.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema tabia ya Askari wa Usalama barabarani kupokea rushwa kutoka kwa madereva na wamiliki wa vyombo hivyo ni ukiukwaji wa sheria na maadili ya kazi hivyo wanapaswa kushughulikiwa mapema kwa maslahi ya Taifa.
DENDEGO ambaye aliyasema hayo katika semina ya Madereva na wamiliki wa vyombo vya moto aliwataka pia madereva kuondokana na tabia ya kutoa rushwa na badala yake wafuate taratibu zilizopo kisheria ikiwemo kulipa faini badala ya kutoa fedha hizo kwa ajili maslahi ya watu fulani.
Akizungumzia suala la madereva kutokuvaa sare Mkuu huyo wa Wilaya alitoa siku kumi kwa madereva wote wa daladala kuhakikisha wanabadilika na katika kusisitiza hilo aliahidi kufanya msako akishirikiana na kamati yake ya ulinzi na usalama kuhakikisha madereva wanabadilika.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani(RTO), ABDI ISSANGO amesema hatakuwa tayari kuwafumbia macho baadhi ya askari wachache wanaokiuka misingi na maadili ya kazi wanaoifanya na kwamba dawa yao ipo jikoni.
Baadhi ya Wamiliki wa vyombo vya usafiri waliomba jeshi la Polisi kupitia kitengo cha usalama barabarani kusamehe makosa yale yanayoonekana ni madogo kwa kisingizio kwamba biashara wanayoifanya ni ngumu,ombi ambalo RTO alilikataa kwa kuwa halikubaliki kisheria.

MUSSA OMARI Dereva wa Daladala zinazopitia njia ya Kange yeye alilalamikia baadhi ya askari wa usalama barabarani kutembea na magari binafsi na hatimaye kuwasimasisha madereva kwa haraka katika mazingira ambayo yanaweza kusababisha ajali.
Chanzo:-  http://www.cloudsfm.co

Post a Comment

Previous Post Next Post