
Askofu
Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini, Dk Valentino Mokiwa(pichani),
amevamiwa na majambazi nyumbani kwake, Mbezi kwa Yusufu, Kimara jijini
Dar es Salaam usiku wa uamkia jana. Katika
tukio hilo, mlinzi wa askofu, amejeruhiwa kwa kukatwa mapanga sehemu
mbalimbali za mwili ikiwa ni katika kumshinikiza aonyeshe alipo Askofu
Mokiwa.
Kwa
mujibu wa Askofu Mokiwa, tukio hilo lilitokea jana saa 8:45 usiku ambapo
watu hao walikata uzio na kufanikiwa kuingia kwenye uwanja wa nyumba
yake.
Alisema
baada ya watu hao ambao idadi yake haifahamu kuingia ndani ya uzio,
walikutana na mlinzi na kumshinikiza awaonyeshe alipo yeye (askofu).
Aliongeza kuwa, mlinzi huyo baada ya kuwaeleza watu hao kuwa, askofu
hayupo, walianza kumcharanga mapanga sehemu mbalimbali za mwili.
“Wamemjeruhi
mshipa wa mguu wa kushoto, sehemu za kichwani na kukata kidole, wakati
haya yakiendelea mlinzi wangu alipiga kelele ambazo ziliwezesha kumshtua
mke wangu na mlinzi mwingine wa jirani yangu,” alisema.
Mokiwa
alisema baada ya mke wake kusikia kelele hizo, alimuamsha na baada ya
watu hao kubaini hilo, walikimbia kusikojulikana. Alisema walitoa
taarifa kituo cha polisi Mbezi Luis ambapo polisi walitoa ushirikiano.
“Baada
ya polisi kutupa PF3 tulimpeleka majeruhi hospitali ya Tumbi, Kibaha
ambapo hapo alitibiwa na kuruhusiwa, hali yake sio mbaya ingawa
analalamika anamaumivu makali maeneo yenye majeraha,” alisema.
Askofu
Mokiwa akizungumzia kuhusiana na kauli za watuhumiwa hao kumtaka yeye
baada ya kuingia kwenye nyumba yake, alisema anafiriki watu hao watakuwa
wametumwa na mtu.
“Nadhani
wametumwa lakini sijui ni nani amefanya hivyo, kiukweli sina chuki,
uadui wala kinyongo na mtu yeyote, ninaishi na watu wangu vizuri, sijui
haya yanayotokea yanalenga nini,” alisema.
Alisema katika maisha yake tukio la kuvamiwa ni la kwanza na kwake amesema ni la aina yake.
Aidha,
wakati akizungumza na NIPASHE Jumapili kwa njia ya simu majira ya saa
8: 15 mchana, Askofu Mokiwa alisema polisi wamewasili nyumbani hapo kwa
ajili ya mahojiano zaidi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, analifuatilia.
Post a Comment