Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda leo Jumamosi, Machi 2, 2013 amezindua Tume maalum
aliyoiunda ili ifanye uchunguzi wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne
yaliyotangazwa Februari 18, mwaka huu na kuwataka wajumbe wa Tume hiyo
watafute kiini cha mserereko wa kushuka kwa ufaulu kuanzia mwaka 2010
hadi 2012.
Waziri Mkuu amezungumza na wajumbe wa Tume hiyo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni, jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa.
Amesema kwa mujibu wa hadidu za rejea, wajumbe wa tume hiyo watatakiwa kuangalia ni sababu zipi zimechangia kuwepo kwa matokeo hayo mabaya, mserereko wa kushuka umekuwa ukiongezeka kwa sababu gani, usimamizi katika Halmashauri ukoje, ukaguzi wa elimu na uhamishiwaji wa sekta ya elimu kwenye Wizara ya TAMISEMi umechangiaje kushuka kwa kiwango cha ufaulu.
Vilevile, watatakiwa kuangalia mitaala na mihutasari ikoje, kuangalia uwiano uliopo kwenye mitihani inayotungwa ikiwa ni pamoja na uhakiki wa mitihani hiyo; kuangalia mazingira ya kufundishia, mfumo wa upimaji, usimamizi na uendeshaji, na kutokuwepo kwa chakula shuleni kunachangiaje kushuka kwa utendaji mbaya wa wanafunzi katika masomo yao.
Tume hiyo yenye wajumbe 15, imepewa muda wa wiki sita kuanzia Machi mosi iwe imekamilisha kazi hiyo na kuwasilisha taarifa yao kwa Waziri Mkuu.
Tume itaongozwa na Prof. Sifuni Mchome wa Tume ya Vyuo Vikuu, na Makamu wake atakuwa Bi. Bernadetha Mushashu (Mbunge wa Viti Maalum – Kagera).
Wajumbe wengine ni Bw. James Mbatia (mbunge wa Kuteuliwa), Bw. Abdul J. Marombwa (Mbunge wa Kibiti), Prof. Mwajabu Possi (Chuo Kikuu - UDSM), Bibi Honoratha Chitanda (CWT), Bibi Daina Matemu (TAHOSSA) na Bw. Mahmoud Mringo (TAMONGSCO).
Wengine ni Bw. Rakhesh Rajani (TWAWEZA), Bw. Peter Maduki (CSSC), Mwl. Nurdin Mohamed (BAKWATA), Bw. Suleiman Hemed Khamis (Baraza la Wawakilishi, Zanzibar), Bw. Abdalla Hemed Mohamed (Chuo Kikuu – SUZA), Bw. Mabrouk Jabu Makame (Baraza la Elimu Zanzibar na Bw. Kizito Lawa (Taasisi ya Kukuza Mitaala)
Post a Comment