Mipasho, rusha roho, vijembe ndio taarabu - Jokha.



Kwa ufupi
Changamoto kubwa ni kuwepo kwa bendi nyingi zinazopiga aina hiyo ya muziki, huku mashabiki wengi wakiwa wanaamini kuwa bendi fulani yu ndio inayofanya vizuri. Hivyo kazi iliyopo kwa wasanii wa bendi mpya kama yetu, ni kufanya mambo makubwa, ili kupata mashabiki wa kudumu.
Kalunde Jamal

HATA angeamua kugombania mashindano ya urembo angeshinda, kutokana na kuwa na mwili uliojengeka vema kulingana na vigezo vya mashindano hayo, licha ya kuwa ni mama wa mtoto mmoja.

Miongoni mwa wasanii wa muziki wa taarabu wenye mvuto wa sauti na maumbile, huku ikiwa ngumu kuamini kuwa ana mtoto basi si mwingine ni binti mwenye macho yenye mvuto kutoka katika kundi la muziki huo lijulikanalo kama T.Moto,  Bi Jokha Kassim.

Wiki hii amekaa chini na Starehe, kwa  mahojiano mafupi kuhusiana na tasnia hiyo ya muziki unaopendwa na watu wengi hususan wanawake ili kuapata mawili matatu.

Baada ya salamu na mengineyo, mambo yalinoga...

Starehe: Tangu umeingia kwenye muziki huu unaonaje na wewe umebadilika kwa kiasi gani.

Jokha: Muziki huu unazidi kuchanua na kujipatia mashabiki kila uchao, licha ya kuwepo kwa changamoto nyingi.

Starehe :Changamoto zipi hizo tena mnazokumbana nazo.

Jokha: Changamoto kubwa ni kuwepo kwa bendi nyingi zinazopiga aina hiyo ya muziki, huku mashabiki wengi wakiwa wanaamini kuwa bendi fulani yu ndio inayofanya vizuri. Hivyo kazi iliyopo kwa wasanii wa bendi mpya kama yetu, ni kufanya mambo makubwa, ili kupata mashabiki wa kudumu.

Starehe: Kwa maana hiyo, unatamanai siku moja bendi zote zife ibaki T.Moto tu?

Jokha: Hapana, kwanza kwa upande wangu ukiachilia mbali changamoto ya kugawana mashabiki lakini uwepo wa bendi nyingi ndio unafanya muziki huu ukue na kufika mbali zaidi na zaidi. Hivyo uwepo wa bendi nyingi za muziki huu ni chachu pia ya kukua kwa muziki wenyewe.

Starehe: Turudi kwenye aina ya muziki na maudhui ya mashairi yake, nyimbo nyingi mnazoimba ni za mipasho na vijembe vingi labda kwa nini?

Jokha: Mipasho na vijembe ndio hasa ilivyo taarabu kilichobadilika ni mipasho navijembe vya sasa vipo wazi tofauti na vya zamani ambavyo vilikuwa ni vya kuzunguka sana na mafumbo.

Starehe: Kwa nini vya sasa vipo wazi wakati muziki wa taarabu ni wa heshima na ndio mana hata asili ya kucheza kwake ni kwa heshima?

Jokha: Hapo hapo tofauti hata wewe umeiona zamani hata kucheza ilikuwa ni kutingishika na muziki wenyewe ulikuwa ni wa ma mwinyi wa pwani lakini sasa hadi wachaga wanacheza taarabu>
Na dunia imebadilika hakuan anayetaka kuumiza kichwa kwa maswali kama ilivyokuwa zamani kuku na yai kilianza nini sijui njiwa peleka salamu, uwazi umezidi na muziki ni biashara na ukitaka kufanikiwa kwenye biashara yoyote ni lazima usome alama za nyakati na waimba taarabu tumezisoma na ndio maana muziki umebadilika kulingana na wakati na soko liantaka nini?

Starehe: Kumekuwepo na kundi la wasanii chipukizi ambao wakitoa wimbo mmoja au miwili hawaonekani tena kwa mtazamo wako tatizo nini?

Jokha: Wengi wao wanaingia kwenye fani wakiwa na mawazo ya kuwa watu maarufu kwa muda mchache matokeo yake wanakuta soko gumu na ndio  wanakata tamaa na kuachana kabisa na muziki au kuwa wavimba macho kwenye bendi.

Starehe:Wavimba macho?

Jokha: Ndio wavimba macho!
Msanii yupo kwenye bendi miaka miwili mitatu na hajawahi kuimba wimbo ukafanya vizuri zaidi ya kuitikia nyimbo za wenzake si mvimba macho ni nani sasa huyo?

Starehe:unawaambia nini wasanii kama hao.

Jokha: Mawaambia kuwa kama Khadija Kopa, Mwanahawa Ally na wengine wengi wakongwe ni kazi na ndio maana mimi nimeendelea kuwepo siku zote kwa kufuata misingi ya kazi na sio kukurupuka hivyo wasikurupuke kuvamia fani wajipange na hatimae wanaweza kufikia malengo yao.

Starehe: mashabiki wategemee nini kutoka kwako?

Jokha: Kwanza nawashukuru kwa kuniamini na kuniona ni mwanamuziki na nimelipima hilo kutokana na shoo tunazofanya kuwa na mashabiki wengi, nawaahidi kwa niaba ya wenzangu hatutowaangusha hata kidogo wakae mkao wa kuendelea kula ambivu baada ya mbivu.....T.Moto hakuna mbichi wala kusubiri.

www.mwananchi.co.tz/

Post a Comment

Previous Post Next Post