WIVU KWA WALIOFANIKIWA UTAKUFANYA NAWE UFANIKIWE!


Stori:Amrani Kaima
Neno wivu katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, limeelezewa kama hali ama tabia ya mtu kusononeka au kukasirika muda amuonapo mpenzi au rafiki yake ana uhusiano wa mapenzi na mtu mwingine.

Kamusi hiyo pia imeeleza kuwa neno hilo hilo wakati mwingine hutumika kama ngoa ama kijicho. Ngoa ni hali ya kuona uchungu, vibaya au chuki kwa kukosa kitu ambacho mwingine amekipata. Kijicho nalo limeelezwa kuwa ni tabia ya mtu kutopenda mwingine apate mafanikio.

Sasa hali ambayo leo napenda kuizungumzia haitahusiana na masuala ya kimapenzi kama kamusi hiyo ilivyoelezea. Naizungumzia ile ya kuona uchungu, vibaya na kuumia kutokana na mtu mwingine kupata mafanikio. Watu wengi wanaposikia neno wivu masikioni mwao huona ni kitu kibaya na hata siku moja hakiwezi kuwa kizuri.
Ni sawa wivu ni kitu kibaya sana kama isipoangaliwa lakini pia ni tabia ambayo ikitumika vilivyo inaweza kuleta faida katika maisha ya binadamu. Wivu ni kitu cha asili ambacho kila binadamu anacho.
Hakuna hata binadamu mmoja ambaye hana tabia ya wivu, achilia mbali binadamu hata wanyama pia wana wivu kiasi kwamba hakuna sababu za wazi kwa nini binadamu ana wivu. Hiyo ni hali ya kawaida ambayo kila mtu anazaliwa nayo.

Ni wivu wa aina gani ambao unakubalika na una faida? Kwa wale ambao wako mashuleni wivu unahitajika ili uweze kufanya vizuri katika masomo yako. Usipokuwa na wivu unaweza kuona kwamba mwenzako kupata 100% wewe ukapata 30% ni kitu cha kawaida tu. Lazima uwe na wivu na huyo aliyepata alama nzuri ili uweze kufanya jitihada za dhati kuhakikisha unamfikia kama siyo kumpita kabisa.

Kama unaishi na mtu ambaye amekuwa na mafanikio makubwa siyo vibaya kama utakuwa na wivu juu yake kwa kujiuliza kwa nini yeye kafanikiwa. Lazima ikuume na wivu huo ukufanye kuwa na juhudi katika kuhakikisha na wewe unafanikiwa kama yeye. 

Kama uko kazini na mwenzako kapandishwa cheo, kuwa na wivu kwa kujiuliza kwa nini mwenzako amepandishwa cheo wewe umeachwa? Je, ni kutokana na kufanya kazi kwake kwa bidii au ni nini? 

Itaendelea wiki ijayo.
GPL

Post a Comment

Previous Post Next Post