
WAZIRI wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, juzi alimuokoa Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, dhidi ya makombora ya
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA).
Busara za Sitta ndizo zilizomfanya Lissu abadilishe nia yake ya kuondoa shilingi kwenye bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Hatua hiyo
ilikuja wakati Bunge limekaa kama kamati kupitia vifungu vya wizara
hiyo, ambapo Lissu alitaka Waziri Nchimbi afafanue serikali
imetekelezaje mapendekezo ya tume yake iliyoongowa na Jaji Ihema pamoja
na ile ya Haki za Binadamu zilizoshauri Jeshi la Polisi kusukwa upya ili
lifanye kazi bila kufuata matakwa ya wanasiasa wa chama tawala.
Lissu alitoa
taarifa kwa Mwenyekiti wa kikao hicho, Anne Makinda, kuwa anakusudia
kuondoa shilingi kwenye mshahara wa Waziri Nchimbi endapo majibu yake
yataendelea kuwa mafupi na mepesi.
Hata hivyo,
kama alivyokuwa amejibu mapema wakati akihitimisha hoja za wabunge,
Nchimbi alisema ni kweli kwamba Jeshi la Polisi halipaswi kufanya kazi
kwa maelekezo ya wanasiasa na kwamba ndiyo sababu Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, anaendelea kuwa kazini.
Nchimbi
aliongeza kuwa ripoti hizo wamezisoma lakini wanajipa muda kuzifanyia
kazi, kwani endapo watakurupuka pasipo kuangalia mazingira mwisho wake
unaweza kuwa mbaya.
“Unajua
ukikutana na mtu aliyetoka kuombwa rushwa na trafiki halafu ukamuulizia
utendaji wa jeshi hilo, atakwambia hakuna watu wabaya kama hao. Lakini
ukikutana na dereva aliyepata ajali akakatika mguu halafu akaokolewa na
trafiki, ukimuuliza kuhusu utendaji wa jeshi hili, atasema hakuna watu
wazuri kama hao,” alisema.
Hivyo, Dk.
Nchimbi alisema ripoti hizo hawawezi kuzifanyia kazi moja kwa moja bali
wanapima kuona wakati zinafanyiwa kazi wajumbe waliegemea kwenye nini.
Majibu hayo
yalimwinua tena Lissu na kutoa hoja ya kuondoa shilingi akisema Waziri
Nchimbi ametoa maelezo ya mzaha wakati tume aliyoiunda yeye na ile ya
Haki za Binadamu iliyoundwa na rais ni kwanini wameshindwa kuzifanyia
kazi.
Hoja hiyo
iliungwa mkono na wabunge wengi wa upinzani ambao walianza kuichangia
wakidai jeshi hilo linafanya kazi kwa maelekezo ya wanasiasa, hata
kufikia hatua ya kushindwa kuwachukulia hatua vigogo wa CCM kwa amri za
wakuu wa mikoa na wilaya.
Kabla ya
Waziri Nchimbi kujibu hoja hizo, Makinda alimuita Waziri Sitta ambaye
alikuwa akikaimu nafasi ya waziri mkuu ili aweze kutoa maelezo kuhusu
sakata hilo.
Sitta
alisema wanasiasa wanapaswa kuwatendea haki wananchi, akifafanua kuwa:
“Hapa kuna tuhuma nzito dhidi ya Jeshi la Polisi, kuna tuhuma nzito
dhidi ya serikali ya CCM na zinatolewa na wenzetu wabunge tunaowaheshimu
kutoka upande wa upinzani.
“Nataka
kushauri mheshimiwa mwenyekiti, kanuni ya 103 si mahala pake kuzungumza
jambo zito namna hii, kwa sababu inahitaji hoja ikae vizuri, iwe na
ushahidi, majibu yawepo.”
“Sasa wakati
wa kuondoa shilingi tuzungumze suala la polisi kutumiwa na wanasiasa,
na pande zote ziweze kupeana taarifa kulingana na mujibu na pengine
upande wa serikali wana jambo la kusema, maana tunakerwa na kauli za
viongozi wa vyama vingine wanaotoa eti saa 24 fulani aondoke,” alisema.
Alisema kuwa kuna wanasiasa wanataka kuonesha serikali haifai, ni goigoi, kwamba hakuna serikali inayoendeshwa hivyo.
“Sasa haya
ukiyachanganya ni furushi kubwa kwa wananchi wetu, ningemshauri
Mheshimiwa Lissu atumie kanuni nadhani ya 53, apewe nafasi kwenye
mkutano ujao alete hoja binafsi kwa mujibu wa kanuni, tuwe na muda wa
kuijadili vizuri na tutoe majibu yanayostahili,” alisema Sitta.
Hoja hiyo
ilikubaliwa na Lissu akisema kuwa Sitta ametoa majibu yanayoeleweka,
ambayo si ya kuokoteza kama ya Dk. Nchimbi, maelezo ambayo baadaye
yaliruhusu kikao kuendelea na kupitisha vifungu na hatimaye kuipitisha
bajeti ya wizara hiyo.
Chadema blog
Post a Comment