NAIROBI, Kenya
KAMPUNI ya Grandpa Records ya Kenya imevunja mkataba wake na mwanamuziki Lucas Nkenda 'Mr. Nice'.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Refigah Slams amelieleza gazeti la Daily Nation la Kenya wiki hii kuwa, amefikia uamuzi huo baada ya Mr. Nice kukiuka makubaliano kati yao.
Mr. Nice, ambaye amehamishia makazi yake nchini Kenya, aliingia mkataba na kampuni hiyo miezi miwili iliyopita kwa ajili ya kusimamia kazi zake.
"Tumeamua kumwondoa Mr. Nice katika udhamini wa Grandpa Records kutokana na kukiuka makubaliano yetu," alisema Slams.
Slams amemwelezea Mr. Nice kuwa ni mtu asiye na ushirikiano na ni mgumu kufanya naye kazi.
Alisema tangu walipoingia naye mkataba, mwanamuziki huyo wa kitanzania amesababisha matatizo mengi katika kampuni yake, ambayo hakuwa tayari kuyataja.
"Kwa kifupi, Mr. Nice alikuwa ameingia mikataba na Sallam Sharaf na Lamar wa Tanzania na hakutueleza wakati anaingia mkataba na Grandpa Records,"alisema.
Mr. Nice alitarajiwa kufanya uzinduzi wa albamu yake mpya ya Chali wa Kibera hivi karibuni chini ya udhamini wa kampuni hiyo.
Katika hatua nyingine, mwanamuziki nyota wa Uganda, Jose Chameleone amezindua albamu yake mpya inayojulikana kwa jina la Badilisha nchini Marekani.
Chameleone alifanya uzinduzi wa albamu hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya wiki mbili nchini Marekani.
Mtandao wa Msn uliripoti juzi kuwa, tayari mwanamuziki huyo tajiri wa Kiganda ameshafanya maonyesho katika miji ya Seattle na Los Angeles.
Kwa mujibu wa mtandao huo, Chameleone anatarajiwa kufanya maonyesho mengine katika miji ya Dallas na Texas kabla ya kurejea Uganda mwezi ujao
Post a Comment