DAR DAMU TUPU - SOMA ZAIDI HAPA

Na Waandishi Wetu
JIJI la Dar es Salaam wiki iliyopita lilikumbwa na matukio ya kutisha yaliyosababisha lionekane ni la damu baada ya majambazi kufanya uhalifu wa kutisha sehemu mbalimbali kwa kuwapiga risasi watu huku wakipora fedha na mali.
Zwahili Miraji.
Gazeti hili lilipita maeneo mengi na kubaini yafuatayo:
DENTI CHUO KIKUU ALIVYOMIMINIWA RISASI
Lilikuwa ni kundi la majambazi sita waliovamia Chuo Kikuu cha Dar es salaam usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita na kufanikiwa kuwapora wanafunzi waliokuwa wakijisomea vitu kadhaa na kummiminia risasi mmoja wao.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea saa 9.00 usiku katika ukumbi ujulikanao kwa jina la Yombo 1 ambapo mwanafunzi Alex Robert, 26, alipigwa risasi.
Kwa mujibu wa taarifa za kiuchunguzi, majambazi waliingia katika ukumbi huo wakiwa  na silaha za jadi pamoja na bunduki aina ya shortgun.
Samwel Michael.
Chanzo makini cha gazeti hili chuoni hapo kilisema kuwa majambazi hayo yalipofika ukumbini yaliwaamuru wanafunzi hao kulala chini na kukabidhi kila walichokuwa nacho, amri ambayo wanafunzi hao walitii kwa kuwapa kompyuta mpakato, simu na fedha.
Hata hivyo, mwanafunzi mmoja aliamka na kuwaomba wamrejeshee flashi yake, ambapo jambazi mmoja aliichomoa na kumtupia ndipo Alex alipoomba kurudishiwa kitambulisho kwa madai kuwa asingeweza kuingia ndani ya chumba cha mtihani bila kuwanacho.
Alex Robert.
 Kitendo cha kuomba kitambulisho ndiyo chanzo cha kupigwa risasi mwanafunzi huyo wa kitivo cha sheria.
Mwanafunzi huyo alipigwa risasi mbele ya wenzake Joseph Hansi, Lunura Masalu na Kitojo Karani na baada ya tukio hilo wanafunzi hao walimchukua mwenzao na kumpeleka kituo cha afya chuoni hapo na baadaye alikimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Mara baada ya kitendo hicho, baadhi ya wanafunzi waliandamana kuelekea Kituo cha Polisi Chuo Kikuu kutaka msaada zaidi baada ya kuona askari walioajiriwa na chuo hawakutokea kupambana na wahalifu hao.
Wanafunzi waliliambia gazeti hili kuwa kwa hivi sasa usalama wa maisha na mali zao unatia shaka kutokana na askari wa chuo kutowajibika ipasavyo.
   Beatus Kisanga.
“Siku ya tukio Ukumbi wa  Yombo 1 haukuwa na mlinzi yeyote hadi tulipoomba msaada kutoka polisi makao makuu, huu ni uzembe,” alisema mwanafunzi mmoja kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.
Makamu Mkuu wa Chuo,Utawala, Yunus Mgaya aliliambia gazeti hili kuwa uongozi wa chuo hicho unasikitishwa na tukio hilo na akaahidi kuimarisha ulinzi.
Afisa Habari Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,  Aminieli  Aligaeshi alisema mwanafunzi huyo amefanyiwa upasuaji na kutolewa risasi tumboni na hivi sasa yuko chini ya uangalizi wa madaktari katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, CP Suleiman Kova amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na akasema majambazi hayo yalikuwa na silaha ikiwemo bunduki na upelelezi unaendelea.
Akizungumzia maandamano yaliyotokea chuoni hapo alisema: “Wanafunzi chuoni hapo walikuwa na lengo la kushinikiza ulinzi. Jeshi la polisi kanda maalum kwa kushirikiana na  makamanda wa mikoa wanaendelea na msako mkali dhidi ya wahalifu hao.”

MFANYABIASHARA APIGWA RISASI, APORWA
Wakati huohuo, Ijumaa iliyopita saa 8 mchana majambazi yakiwa na pikipiki na bastola yalimpiga risasi na kumpora kiasi kikubwa cha fedha wakala wa magazeti ya makampuni mbalimbali nchini.
Wakala huyo aliyejulikana kwa jina la Zwahili Miraji Mrutu akizungumza na gazeti hili akiwa Hospitali ya Muhimbili alisema, alikuwa maeneo ya mitaa ya Kipata na Swahili jijini Dar akiwa anapeleka fedha benki ghafla alijikuta akipigwa risasi kifuani na kuporwa pesa.
 Akizungumza kwa shida katika Wodi ya Kibasila, Mrutu alisema: “Majambazi hayo yalikuwa na pikipiki na wakaniambia niwape fedha, nilipozing’ang’ania, walinipiga risasi moja kifuani na mbili hewani kwa lengo la kutawanya watu.”
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, ACP Marietha Minangi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. 
“Tukio hilo kweli limetokea na majeruhi huyo yupo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili akiendelea na matibabu huku nasi tukiendelea na upelelezi,” alisema Kamanda Minangi.

ANYONGWA KIKATILI
Naye mwendesha pikipiki ya miguu mitatu maarufu kama Bajaj ambaye kituo chake kilikuwa maeneo ya Sayansi, Beatus Kisanga, mkazi wa Makumbusho, Dar, ameuawa kinyama kwa kunyongwa na kamba na majambazi.
Tukio hilo lilitokea ndani ya Baa ya Serengeti iliyopo maeneo hayo huku kaka yake ambaye ni mlinzi wa baa hiyo aitwaye Batlista Kisanga alikutwa akiwa hoi hajitambui.
Akizungumza na Uwazi, mmiliki wa baa hiyo, Venancy Lyimo alisema kuwa marehemu aliuawa saa 11 alfajiri naye alipewa taarifa hizo kwa njia ya simu na kijana ambaye anafanya usafi mishale ya saa moja asubuhi.
“Kijana huyo aliniambia kuwa alimkuta mlinzi  akiwa kaunta hajitambui huku vinywaji vikiwa vimetolewa nje na kuzagaa chini. Nilitoka nyumbani kuja hapa kazini,” alisema.
Aliongeza kuwa baada ya kufika alimkuta marehemu akiwa amefungwa kamba mikononi na miguuni huku mdomoni amefungwa kitambaa na mwili wake ukiwa umetupwa kwenye jiko la kuchomea nyama.
“Kinachoonekana ni kwamba wale majambazi waliwapa sumu hawa jamaa,’’ alisema Lyimo.
Aliongeza kuwa, aliwapigia simu polisi waliofika na kuuchukua mwili wa marehemu huku mlinzi akipelekwa Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu.
Kaka wa marehemu aitwaye Yesse Peter akizungumza na Uwazi, alisema kwamba mwili wa marehemu ungesafirishwa wakati wowote kwenda Mbeya kwa mazishi.

KACHERO WA POLISI ANUSURIKA KUUAWA
Wakati hayo yakitokea, askari wa upelelezi aliyefahamika kwa jina la Samwel Michael usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita alinusurika kuuawa na wananchi waliomhisi kuwa ni jambazi baada ya kupata ajali ya bodaboda.
Askari huyo alihisiwa na wananchi kuwa ni muhalifu baada ya kukutwa na bastola huku akiwa amepoteza fahamu.
Tukio hilo lilitokea karibu na Kituo cha Drive Inn, Msasani jijini Dar ambapo mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema: “Nilianza kupata mashaka baada ya kumuona jamaa akiendesha pikipiki aina ya Bajaj Boxer kwa kasi.
“Nikiwa namshangaa ghafla nilimuona akilivaa hili greda ambalo limeegeshwa hapa baada ya kumaliza kufanya ukarabati wa hii barabara.”
Akiwa eneo la tukio mwandishi wetu alimshuhudia askari huyo akitapatapa kutaka kuamka huku baadhi ya wananchi wakisema huenda ni jambazi na kutaka kummaliza. 
Wakati wananchi hao wakitaka kummaliza ghafla alitokea askari wa kikosi cha usalama barabarani na kuchukua bastola iliyokuwa pembeni ya majeruhi huyo na kuanza kumpekua.
Baada ya kumkagua alimkuta na kitambulisho chake cha kupigia kura pamoja na cha kazi kilichoonesha alikuwa  askari wa upelelezi pia alimkuta na pingu pamoja na nyaraka zingine. 
Baada ya kupata vielelezo hivyo afande huyo aliwaondoa hofu wananchi waliokuwa wakitaka kummaliza majeruhi huyo na kuwaambia kuwa  alikuwa ni askari wa upepelezi aliyekuwa kazini.
Baada ya kutulizwa wananchi hao waligeuka wasamaria wema na kuanza kumsaidia majeruhi huyo mpaka walipofika askari wengine ambao walimuwahisha hospitali kupata matibabu.
Habari hii imekusanywa na Makongoro Oging’, Haruni Sanchawa, Richard Bukos na Mwaija Salum GPL

Post a Comment

Previous Post Next Post