Fifa yaigomea Yanga

 

By MWANDISHI WETU  


IN SUMMARY
  • Yanga kupitia kwa Katibu Mkuu wao, Lawrence Mwalusako waliandika barua Fifa Aprili 8, mwaka huu wakitaka shirikisho hilo liiamuru TFF kuwarudisha fedha hizo.
YANGA wamekaa wakafikiria weee wakaona hakuna jinsi wanaweza kuzuia Simba isilipwe deni la Mbuyu Twite. Unajua walichofanya? Wakaandika barua Fifa kuomba TFF ishinikizwe iache kuwakata fedha za Mbuyu Twite inazowalipa Simba.
Unajua Fifa wamefanyeje? Wameisoma barua weee halafu wakaikunjakunja wakaiweka kwenye kapu wakasema; “Sisi inatuhusu nini!”  Fifa ikaitolea nje Yanga.
TFF kwa vipindi tofauti ilikuwa ikikata mapato ya mechi za Yanga msimu uliomalizika ili kuilipa Simba fedha ambazo walimpa Mbuyu Twite katika usajili uliokwama mwaka 2012.
Yanga kupitia kwa Katibu Mkuu wao, Lawrence Mwalusako waliandika barua Fifa Aprili 8, mwaka huu wakitaka shirikisho hilo liiamuru TFF kuwarudisha fedha hizo.
“Tunaomba Fifa muiamuru TFF irudishe fedha (Sh74 milioni) ambazo wametukata kwa ajili ya kuilipa Simba,” inasema sehemu ya barua ya Yanga.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Sheria wa Fifa, Marco Villagar amewajibu Yanga na kuwaambia kuwa suala hilo linapaswa kushughulikiwa na TFF wenyewe.
“Baada ya kupitia shauri lenu, tumeona suala hilo lipo chini ya TFF, kwa hiyo tunashauri suala hilo lishughulikiwe na shirikisho lenu,” inasema sehemu ya barua hiyo ya Fifa.
Simba ilimpa Mbuyu Twite Dola za Marekani 32,000 (Sh 52 milioni), lakini katika barua yao Mwalusako ameandika kuwa wamekatwa na TFF jumla ya Sh74 za Tanzania.
Simba iliingia mkataba na Twite mwaka jana nchini Rwanda na kumpa dola 30,000 ingawa Simba waliongeza Dola 2,000 za nauli na malazi ya mjini Kigali.
Hata hivyo Yanga ilizunguka na kwenda kufanya mazungumzo na FC Lupopo ya Congo, ambayo ilimwidhinisha beki huyo kuchezea Yanga.
Simba ilishtaki TFF ambayo iliamuru suala hilo limalizwe kiungwana kwa Yanga kuilipa Simba fedha zake, lakini kutokana na klabu ya Jangwani kupiga danadana, shirikisho la soka nchini lilianza kuikata fedha Yanga katika kila mechi iliyokuwa inafanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
http://www.mwanaspoti.co.tz

Post a Comment

Previous Post Next Post