Hali ya usalama Darfur, Gordofan yazikimbiza Simba, Yanga, Falcon


Ujenzi ulipokuwa ukiendelea kwenye Uwanja mpya wa Kaduguli uliopo kusini mwa mji wa Gordofan. Uwanja huo umekamilika na utatumiwa katika mashindano ya Kombe la Kagame yanayoanza kesho

Mashindano ya soka ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati maarufu Kombe la Kagame kwa msimu huu yanaanza kesho mpaka Julai 2 katika miji ya Darfur na Gordofan, Sudan.

Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) linalosimamia mashindano hayo limeamua kuyapeleka mashindano hayo katika miji ya Darfur na Gordofan kwa mtazamo wa kuwakusanya watu pamoja ili kurejesha amani katika maeneo hayo ambayo yalikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu.

Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye amezihakikishia nchi shiriki kuwa maeneo ya Darfur na Gordofan ni salama kwa ajili ya kufanyika kwa mashindano hayo.

Hata hivyo Serikali ya Tanzania ilionyesha wasiwasi wa usalama katika miji hiyo ya Darfur na Gordofan na hivyo kuzizuia Simba, Yanga na Super Falcon ya Zanzibar kushiriki mashindano hayo kwa mwaka huu.

Uamuzi huo wa Serikali umechukuliwa kufuatia mjadala ulioibuka bungeni, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema miji hiyo siyo salama huku akishangazwa na uamuzi wa Cecafa kuamua kuandaa mashindano hayo katika miji hiyo ya Sudan.

Tayari Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Bin Kleb na Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage wameungana na kauli ya Serikali kuhusu hali ya usalama ya miji ya Gordofan na Darfur.

Lakini hata hivyo mwishoni mwa wiki iliyopita Serikali ya Tanzania ilitoa tamko kwamba inaziruhusu Simba, Yanga na Super Falcon kwenda kushiriki katika mashindano, Cecafa waliikatalia Tanzania kwani tayari timu nyingine zimepewa nafasi za timu za Tanzania.

Darfur

Wakati mvutano huo ukiendelea, Mei 13 mwaka huu, wanachama wa Ujumbe wa Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa Darfur (UNAMID) wameungana na kiongozi wa pamoja wa Muungano huo Mohamed Chambas kulaani shambulio la kinyama la Mei 12 lililosababisha kifo cha Mohamed Bashar ambaye alikuwa kiongozi wa kundi la Justice and Equality Movement-Sudan (JEM/Bashar) na washirika wenzake.

Chambas anasema kundi hilo lilikuwa na nia kutafuta suluhu ya amani katika mgogoro huko Darfur. Kuuawa kwa kiongozi huyo kunatokana na hatua ya kusaini makubaliano ya amani ya Doha (DDPD) April 6 mwaka huu.

Mpaka sasa kuna baadhi ya vikundi hatari ambavyo vinaendeleza vuguguvu la machafuko mjini Darfur hususani vikundi vya kijeshi ambavyo havitaki kabisa kutia saini ya makubaliano ya amani au kuheshimu sheria ya kimataifa ya haki za binadamu katika kushiriki kurejesha amani.

Mbali na hatua hiyo, Aprili 29 mwaka huu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitangaza kuwa tangu kuanza kwa mzozo huo mpaka sasa bado suluhu ya kisiasa haijapatikana na hali ya usalama kwa watendaji wa Umoja wa Mataifa inatia wasiwasi. 

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani ndani ya Umoja wa Mataifa, Herve Ladsous anasema ripoti iliyoandaliwa juu ya hali ya utendaji kazi kati ya Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika huko Darfur (UNAMID) inabainisha kuwa majukumu ya chombo hicho yamekuwa yakikwamishwa na hali ya kupungua kwa usalama katika eneo hilo.

Katika tukio lingine la kusikitisha, Aprili 20 mwaka huu Jopo la mawakili wa utetezi katika mahakama ya ICC liliripoti kuwa Saleh Mohammed Jerbo Jamus ambaye alikuwa ni mmoja wa waasi wa Sudan aliuawa wakati wa mapigano huko Darfur Kaskazini.

Mpaka sasa msimamo wa mahakama hiyo ni kufanya uchunguzi wa kifo chake kabla ya kufuta kesi yake. Jerbo aliuawa wakati wa shambulio kwenye makazi yake lililofanywa na wapiganaji wa kundi lililojitenga kutoka kundi la Justice and Equality Movement linaloongozwa na Gibril Ibrahim.

Chanzo cha Machafuko,Darfur

Mzozo wa Darfur ulianza miaka 10 iliyopita baada ya waasi kuanza kushambulia maeneo ya Serikali, wakiishutumu Khartoum kwa kuwakandamiza Waafrika na kuipendelea jamii ya Kiarabu. Kundi la wanamgambo wa Kiarabu la Janjaweed, wakati huo lilishutumiwa kwa kuendesha mauaji ya kikabila dhidi ya raia Waafrika wa Darfur

Post a Comment

Previous Post Next Post