Hatima ya Redondo Simba leo


HATIMA ya mchezaji Ramadhani Chombo ‘Redondo’ wa Simba itajulikana leo baada ya Kamati ya Utendaji ya timu hiyo kukutana.

Redondo hajaichezea Simba kwa karibu nusu msimu uliopita baada ya kusimamishwa kwa utovu wa nidhamu akiwa na wachezaji wengine wa timu hiyo Haruna Moshi ‘Boban’ na Juma Nyoso.

Hata hivyo Boban na Nyoso wameshaachana na Simba baada ya kusajilia Coastal Union kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu. Akizungumza kwa simu na mwandishi wa gazeti hili, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ alisema hatima ya Redondo na mambo mengine ya Simba itajulikana baada ya kikao cha leo cha uongozi.

“Tunajua tunachokifanya, tutafanya maamuzi baada ya viongozi kukutana kesho (leo),” alisema. “Kitakachojadiliwa sio suala la Redondo tu, watajadiliwa mambo mengi ikiwemo wachezaji wote wa Simba pamoja na mipango mingine ya kuelekea kwenye Ligi,” alisema Kinesi.

Wachezaji wengine ambao Simba imeachana nao ni Juma Kaseja na Amir Maftaha waliomaliza mikataba yao huku ikivunja mikataba ya Abdallah Juma na Paul Ngalema. Hivi karibuni Redondo alikaririwa akilalamikia uongozi wa Simba kumuacha bila kujua lolote.

Redondo aliitaka Simba iamua lolote juu yake hata kama ikibidi kumpeleka kucheza kwa mkopo katika klabu yoyote kwani anapata tabu kutunza familia yake kwa vile anategemea soka.

Post a Comment

Previous Post Next Post