HATIMAYE WABUNGE WAKIRI KUTOA RUSHWA KWA WAPIGAKURA..

Moja ya vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma.
Wabunge wameelezwa kuwa, vita dhidi ya rushwa inatishia nafasi zao kisiasa kwani wengi huitumia ili waendelee kuwepo madarakani, huku baadhi ya wabunge wakikiri kufanya hivyo kutokana na madai ya kushinikizwa na wapigakura.


Kutokana na hali hiyo, wabunge wameshauri jamii ielimishwe kazi na majukumu ya mbunge, kwani vinginevyo wataendelea kushinikizwa kutoa rushwa hasa wakati wa uchaguzi.
Akiwasilisha mada kwenye semina ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bajeti, Hesabu za Serikali (PAC) na Serikali za Mitaa (LAAC) kwenye Ukumbi wa African Dream juzi kuhusiana na mapambano dhidi ya rushwa na nini kifanyike, Mkuu wa Skuli ya Sayansi za Jamii ya Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe alisema mwingiliano wa kisiasa ni changamoto kubwa katika vita dhidi ya rushwa.
"Vita dhidi ya rushwa inatishia nafasi za wabunge kisiasa kwani wengi wenu huitumia ili waendelee kuchaguliwa na ina namna na rangi nyingi sana. Pia mfumo wa Bunge nao una walakini, kwa mfano Mbunge anatoa hoja nzuri kuhusiana na mambo ya rushwa, lakini kwanza tunamuangalia kichama badala ya kijamii," alisema Prof. Mwamfupe.
Pia alisema baadhi ya wabunge wametokana na rushwa katika uchaguzi, hivyo hawawezi kupiga vita rushwa na kwamba suala la kuambiwa mtu ana ushahidi katika mambo ya rushwa ni tatizo lingine linalowafanya baadhi ya watu kuzungumza chinichini kwa vile hawana ushahidi wa kutosha kuhusu rushwa.
Alisema pia kwenye baadhi ya mamlaka zinazohusika na kupiga vita rushwa nazo zina matatizo kwa kuwa sehemu nyingi nako kumeoza.
Alizitaja baadhi ya taasisi ambazo zinatakiwa zishiriki kwenye mapambano dhidi ya rushwa, lakini nazo zina watuhumiwa wa rushwa kuwa ni Ofisi ya Rais ambapo ndipo ilipo Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Wabunge, Polisi na Mahakama.
"Wabunge wapo watuhumiwa wa rushwa, polisi wapo, mahakama wapo, afya wapo na walimu pia wapo, sasa kuna changamoto kubwa kwa jamii," alisema.
Hata hivyo, alisema uwezekano wa kudhibiti rushwa upo mkubwa kwa jamii kutakiwa kujitambua na mamlaka husika kila moja ikatekeleza wajibu wake inavyotakikana kwa kila mtu kuhakikisha hatoi wala hapokei rushwa.
"Rushwa zote ni mbaya, lakini inayoumiza zaidi ni ile ya makubaliano, mfano kule Ukerewe umepanda lifti ya mgongo wa mamba anakuvusha ziwani, sasa mnafika katikati ya maji anakuuliza vipi mimi mzuri wa sura au?
"Hapo wewe mara moja utamwambia wewe ni mrembo na nashangaa kwa nini umechelewa kushiriki mashindano ya urembo.  Au rushwa ya mtu unampa halafu unamwambia usiende kusema hii ni hatari sana," alisema Prof Mwamfupe na kuongeza kuwa tatizo la rushwa si yatima ana wazazi, mjomba, shangazi na majirani, hivyo kumuangamiza kunahitaji nguvu kubwa kwa jamii yote, lakini msingi mkubwa wa vita umejikita katika utashi wa kisiasa.
Hata hivyo, alisema dhiki na ulafi ndiyo tatizo kubwa la rushwa pia kwani wapo wanaolipwa vizuri, lakini kwa tamaa zao wanataka kuendelea kupata mambo makubwa.
Wakichangia mada hiyo na nyingine zilizowasilishwa na Mbunge wa Magu Mjini, Dk. Festus Limbu (CCM) na Naibu Mkuu wa Takukuru mkoani Dodoma, Sostheness Kibwengo, baadhi ya wabunge walitoa malalamiko yao kwamba wakati mwingine utamaduni wa kijamii wa kuwakarimu wageni unatafsiriwa kuwa rushwa, huku wengine wakitaka wapiga kura wapewe elimu wasiwashinikize wabunge wawape rushwa.
Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere (Chadema), alisema wabunge wanashinikizwa kutoa rushwa na wapiga kura na hivyo kuomba Bunge, Ofisi ya Rais Utawala Bora, iweke utaratibu wa kuanza kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na majukumu ya Mbunge angalau kuanza kupunguza tatizo  hilo.
"Wapo wapiga kura wanaweza kukufuata wanataka karo za shule za watoto wao na mambo mengine mengi," alisema.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Zarina Mabadiba (CCM) akichangia alisema unatumika muda mwingi kupiga vita rushwa badala ya kupiga vita sababu za kuwepo rushwa na kutolea mfano wa muuguzi ambaye anakwenda kazini, lakini mshahara wake ni mdogo hivyo kama akitokea mtu anataka  kumpa rushwa anachukua.
Pia alisema inaweza kutokea unaenda hospitali na mgonjwa yupo mahututi, hivyo mpo tayari kutosa rushwa kwa nia ya kupata huduma bora kuokoa maisha yake.
Aliomba kuwepo na tafsiri pana kuhusiana na rushwa kwani inaweza kutokea umekaa na wapiga kura wako nyumbani mkabadilishana mawazo kisha mnapata chakula lakini baadaye mnakamatwa kwamba ulikuwa unatoa rushwa.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy (CCM) alisema ili kumfahamu mla rushwa ni kuangalia mshahara wake na mali alizo nazo na kushauri watu wanyang'anywe mali zao na kufilisiwa na kuomba taasisi zinazohusika ziache kukimbizana na wala rushwa wadogo ya Sh 2,000 au Sh 50,000 badala yake ipambane na wala rushwa wakubwa.
Mbunge wa Viti Maalumu, Moza Abeid alitaka Takukuru ijisafishe yenyewe kwani haina siri na alitolea mfano yeye aliwahi kwenda kutoa taarifa ya kutakiwa rushwa mahali, lakini akashangaa taarifa zikamfikia muhusika.
Waziri Mkuchika akijibu baadhi ya hoja alisema tayari sekretarieti ya maadili imeshawasilisha mapendekezo ya marekebisho ya namna ya kuiboresha Takukuru ili iwe na nguvu zaidi na kwamba pia watapendekeza katiba ya sasa itajwe Takukuru na majukumu yake.
Semina hiyo iliandaliwa na Mtandao wa Wabunge katika vita dhidi ya Rushwa (APNAC) na kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Post a Comment

Previous Post Next Post