Hatma ya Joseph Mbilinyi mikononi mwa DPP


ImageHatma ya kufikishwa mahakamani kwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘’Sugu”( Chadema), iko mikononi mwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema jana kuwa jeshi lake limekamilisha upelelezi kuhusu tuhuma zinazomuhusu Sugu na kwamba wanasubiri maelekezo ya kumfikisha mahakamani. Mbilinyi alikamatwa juzi mchana akiwa mjini Dodoma anakohudhuria vikao vya bunge na habari zilisema anatuhumiwa kutoa maneno ya kashfa na uchochezi dhidi ya Waziri, Mkuu Mizengo Pinda.  Inadaiwa kuwa mbunge huyo amefanya hivyo kupitia mtandao wa kijamii. Kamanda huyo alisema jana Mbilinyi aliripoti katika Kituo cha Polisi Kati kama alivyotakiwa na jeshi hilo na kuongezewa dhamana hadi leo anapotakiwa kurudi tena kusikiliza hatma yake. Misime alisema “jeshi hilo liliamua kumkamata mbunge huyo baada ya kugundulika kuandika maneno ya kumtukana Waziri Mkuu kuhusu utendaji wake na kumdhalilisha katika siku ambayo hakuitaja.” Taarifa zisizo rasmi zinaonyesha kuwa, mbunge huyo anatuhumiwa kuandika maneno hayo ya kashfa kufuatia kauli ya Pinda hivi karibuni kuhusu kuwataka polisi kuwapiga raia wasiotii sheria. 
       Alikuwa akijibu swali la papo kwa papo ndani ya Bunge wiki iliyopita ambapo alisema Serikali imechoshwa na vitendo vya watu kutotii sheria na kutoa mfano wa matukio ya Mtwara na Arusha. Huko Mtwara polisi walitumia nguvu zaidi kuwadhibiti wananchi waliokuwa wakikataa gesi isisafirishwe kwa njia ya bomba kwenda Dar es Salaam, wakati huko Arusha, walifanya hivyo katika kuwatawanya wafuasi wa Chadema, waliokuwa wakishiriki katika tukio la kuaga maiti. Baadhi ya watu wakiwamo wanaharakati walisema kauli hiyo inaweza kuleta chuki kati ya polisi na wananchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post