Watu Afrika Kusini wanamuenzi sana kiasi cha kutoweza kutafakari maisha bila rais huyo mstaafu
Lakini ndani ya mioyo yao, mamilioni ya watu wanaompenda wanajua vyema kuwa jambo hilo haliwezi kuepukika.
Mandela amekuwa akiugua mara kwa mara katika siku za hapo nyuma, raia wa Afrika Kusini ndio sasa wanaanza kuona dalili na kukubali kuwa Mandela naye ni binadamu kama watu wnegine popte duniani.
Hata hivyo mada hii bado ni jambo ambalo haliwezi kuzungumziwa hadharani nchini Afrika Kusini.
Somadoda Fikeni, mkuu wa shirika la hifadhi za Afrika Kusini, anasema hatuna mtu tunayeweza kumfananisha na Mandela hapa Afrika Kusini na kote duniani.
"watu wanamuona kama tiba kwa maradhi yaliyo katika jamii au maovu yanayotokea katika jamii . Na ndio maana watu hawataki kukubali kuwa Mandela atawaaacha hata siku moja. ''
Kulingana na utamaduni wa Afrika Kusini, wale walio wagonjwa sana hawafi hadi familia 'inapowaachilia' kiroho.
Raia wa Afrika Kusini wanamuona Mandela kama gundi ambayo inashikilia jamii pamoja na wanaamini kuwa mabadiliko katika jamii, umaskini, ufisadi na ukosefu wa ajira yanaweza kuangamizwa ikiwa tu Mandela atasalia kuwapa muongozo viongozi wa wengine nchini humo.
Hii inaweza kuwa ni ndoto kubwa kumwekea mtu mmoja , lakini machoni mwa wengi, Mandela sio binadamu wa kawaida.
Hata hivyo, kwa mara ya kwanza inaonekana kuwa kilio kinachomzingira Mandela anapougua mara kwa mara kinaanza kubadilika kwa sauti.
Jarida la Sunday Times mwishoni mwa wiki, lilikuwa na kichwa: Ni wakati kumruhusu aende zake.''
Ni kauli ambayo inazua hisia kwa familia ya Mandela na watu wengi Afrika Kusini.
Kawaida wito ambao hujitokeza hasa afya ya Mandela inapoendelea kuzorota ni watu wamuombee.
Lakini haya hayakuwa maneno ya mtu wa kawaida kuhusu sura anayotoa Mandela kwa jamii.Yalikuwa maneno ya rafiki yake na mfungwa mwenzake katika gereza la Roben Island, Andrew Mlangeni, baada ya kupokea habari kuwa Mandela amelazwa tena hospitalini.
"familia yake lazima imwache aende zake, ili Mungu afanya atakalo naye...Pindi familia itakapofanya hivyo, nao watu wa Afrika Kusini wataweza kumruhusu aende zake,'' alinukuliwa akisema bwana Mlangeni.
Wengi wanafahamu fika kuwa hali mbaya ya kiafya ya Mzee Mandela, inaendelea kuzorota, lakini kwa hali hiyo hiyo wanamtaka aweze kuishi maisha marefu.
Ni uhusiano wa kipee walio nao Mandela.
''Huenda ikawa mzozo katika familia yake ndiyo inampa wasiwasi na hilo linahitajika kusuluhishwa wakati akiwa bado hai. Huenda asipokelewe vyema, upande huo wa pili hadi mambo haya yatakaposuluhishwa,'' alisema Mlangeni
Mtu yeyote ambaye amewahi kumpenda baba au babu yake anaweza kushuhudia kuwa yeye kawaida hataki mtu yule kuondoka...watu nchini Afrika Kusini wanamuona Mandela kama baba yao asiyekuwa na kifani.
Mandela alizuia kutokea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, alipotoa wito wa waafrika weusi na wazungu kuungana pamoja na kusameheana baada ya vita alivyoongoza dhidi ya ubaguzi wa rangi, wakati ambapo Afrika Kusini kama nchi ilionekana karibu kuporomoka.
Lakini nchi hiyo ingali inakabiliwa na mgawanyiko, ubaguzi wa rangi kujitokeza mara kwa mara na chama wa ANC kimegawanyika kuliko wakati wowote ule.
Mandela alichiliwa baada ya miaka 27 gerezani kufuatia vita vyake dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Ukabila unaanza kujitokeza nchini humo, baadhi ya wataalamu wanasema kuwa hii ni kutokana na kukosekana kwa uongozi thabiti.
Migawanyiko hii inawalazimisha raia wa Afrika Kusini kuitizama upya ndoto ya Nelson Mandela ya nchi ya mshikamano licha ya rangi ya watu na ikiwa ndoto hiyo itawahi kutimizwa.
Baadhi wangali wanaamini kuwa Afrika Kusini inaweza kujikwamua na kujipa hadhi ya juu zadi kama iliyokuwa ndoto ya Mandela. SOURCE: BBC SWAHILI.
Post a Comment