Serikali ya Nigeria inamsaka kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau |
Serikali ya Nigeria imeyaharamisha makundi mawili ya wapiganaji wa kiisilamu ikionya kuwa yeyote atakayetoa msaada kwao atakabiliwa na kifungo cha miaka ishirini jela.
Rais Goodluck Jonathan, ametangaza makundi ya Boko Haram na Ansaru kuwa makundi ya kigaidi.
Wapiganaji wa kiisilamu wamewaua takriban watu 2,000 tangu kuanza kwa vita vyao mwaka 2009.Jeshi limekuwa likifanya harakati dhidi ya makundi hayo katika eneo la Kaskazini mwa nchi tangu serikali kutangaza hali ya hatari mwezi jana.
Rais Goodluck amesema kuwa harakati za makundi hayo sasa zitachukuliwa hatua za kisheria chini ya sheria ya kuzuia vitendo vya kigaidi
Ina maana kuwa mtu yeyote ambaye kwa kujihusisha na mpango wowote wa Boko Haram au kutoa msaada kwa vyovyote kwa kundi la Ansaru atafungwa jela miaka ishirini au zaidi ikiwa atapatikana na hatia.
Mnamo siku ya Jumatatu, Marekani ilitangaza zawadi ya dola milioni saba kwa yeyote mwenye taarifa kuhusu kiongozi wa Boko Haram Abubakar Shekau na viongozi wengine wa makundi ya wapiganaji wa kiisilamu.
Kundi la Boko Haram, lilizindua harakati zake mwaka 2009 kwa kufanya mashambulizi ya mabomu na mauaji ya kupangwa Kaskazini na Katikati mwa Nigeria.
Nalo kundi la Ansaru, linalosemekana kuwa na uhusiano na Boko Haram,lilijiunga na harakati hizo mwaka 2012, kwa kuwateka nyara raia wa kigeni nchini humo.
Lilisema kuwa liliwaua raia saba wa kigeni na wa kutoka Mashariki ya Kati ambao waliwateka nyara mwezi Februari mwaka 2012 katika jimbo la Bauchi.
Mwezi jana Rais Jonathan, alitangaza hali ya hatari katika majimbo ya Borno, Yobe na Adamawa , ambayo ni ngome kuu za makundi ya kiisilamu.
Hali iliyofuatia ilikuwa jeshi kuanza harakati dhidi ya makundi hayo kwa kutumia ndege za kijeshi kufanya mashambulizi ya angani ili kuwaangamiza wapiganaji hao.
Makundi ya kutetea haki za binadamu, yamekuwa yakituhumu majeshi ya serikali kwa kuwalenga watu wasio na hatia baada ya kudai kuwa wanaunga mkono makundi ya wapiganaji.
Jeshi hata hivyo limekanusha madai hayo.
- BBC SWAHILI.
Post a Comment