RIWAYA: ROHO MKONONI
MTUNZI: George Iron Mosenya
SIMU: 0655 72 73 25
SEHEMU YA KUMI NA MOJA
Macho yalikuwa mekundu sana, akasingizia kuwa anaumwa kichwa, Betty akamtafutia dawa na kumpatia anywe, Joy akazipokea na kuzimeza. Kisha akakirukia kitandani, kizunguzungu kikiwa kimemwandama.
Kitanda kikaonekana kama kinazunguka kwa kasi katika namna yua kukera, joto likaizidi maarifa feni iliyokuwa inapuliza pale ndani, Joy akaondoa nguo zake na kujifunika na kanga pekee.
Akajilazimisha kulia machozi hayakutoka lakini kuna donge lilikuwa limemkaba kooni.
Ama kwa hakika Joyce alikuwa amefikwa.
Uzito wa roho kadhaa mkononi mapema kabisa ulionekana kumzidia. Ili apate ahueni alitakiwa kuchagua nini cha kutupa na kipi cha kubaki nacho. Joyce alitakiwa kufanya maamuzi ya kuokoa roho mojawapo. Ili asishindane na ule usemi ambao mchumia janga hula na wakwao.
Joy akabaki kuwa mfa maji asiyeisha kutapatapa….
USINGIZI ukiwa umegoma kabisa kumtembelea Joy na kumtenganisha na dunia kwa muda na kuyasimamisha mawazo. Mara alisikia mivumo ya sauti ikinena lugha ambayo hakutaka kuisikia kabisa, lugha ya kumzungumzia Isaya. Na mnenaji alikuwa ni Betty.
“Yaani huyo ameingia pabaya lakini ujue nini, mimi shida yangu ni huyo baba yake anayejiita mbunge. Nikimpata huyo sikosi milioni kama thelathini hapa. Wanajua kuhonga hao wajinga. Sasa milioni thelathini hapa hatujarekebisha walau ki’zahanati chetu cha Ukala, hatujaweka madawati kadhaa katika ile shule tuliyosoma pale Ukala. Ujue nilikuwa nachukia kukaa chini yaani we acha tu, nd’o maana nakwambia Joy mi sitaki kuondoka hivi hivi acha tu nizichume dhambi lakini hata Mungu anajua kuwa sizichumi kwa sababu ya starehe Joy wangu. Ingekuwa ni kwa ajili ya starehe nadhani hata hapa kwako ningekuwa n’shahama…mi nataka pesa kwa ajili ya maendeleo. Sijui mtoto wa mbunge sijui mtoto wa diwani mimi sijali cha msingi ni mwanaume mwenye tamaa basi ile OLE inamuhusu…..” mara Betty akasita kisha akasema kwa sauti ya chini kidogo, “Sijui Joy mwenyewe keshalala najipigisha makelele peke yangu!!” kisha akaanza kujiimbia nyimbo alizokuwa amezikariri.
Joy hakuwa amelala alisikia kila kitu, maumivu makali kabisa yakapenya katika moyo wake, akajikaza asisike kama analia lakini machozi yalimwagika kwa wingi.
Akiwa hapo kitandani akakumbwa na wazo la kutatua tatizo hili, akafikiria kumweleza Isaya kuwa anampenda sana na yupo tayari kuwa katika mahusiano naye. Lakini akakumbuka mambo mawili makuu, jibu la mwisho alilowahi kumpa Isaya, “SIJAWAHI KUKUPENDA ISAYA”….hili lilimuumiza hata yeye maana lilikuwa jibu kavu linalochoma kwelikweli. Kisha akakumbuka na ujumbe alioupokea kutoka kwa Isaya siku moja iliyopita, “SITAKI MAZOEA YA KARIBU NA WEWE.”
Joy alipoukumbuka ujumbe huu akazidi kutiririkwa machozi na kuona kuwa hakutendewa haki hata kidogo kupewa jibu lile.
Ama hakika mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu.
Kwa majibu haya mawili katika siku tofauti Joyce aliuona utata waziwazi, Isaya asingekuwa mwanaume mjinga akubali kirahisi kuwa katika mahusiano na mtu ambaye alimtamkia kuwa hana hisia naye.
Hapa sasa Joy akaamini kumwendea Isaya na kumweleza kuna uwezekano wa kukutana na mambo mengine yenye utata zaidi, ama kupuuzwa na kutukanwa hadharani kuwa anamtaka Isaya kwa ajili ya pesa zake, ama la kuwa katika mapenzi ya foleni. Jambo ambalo binti huyu hakuwa tayari.
Mawazo haya yakazidi kumpasua kichwa Joy.
Mara akafikiria pakipambazuka amweke Betty kitako na kumweleza kila kitu kilivyo juu ya huyo Isaya ambaye anajiita Joram. Wazo hili akaliona ni jema sana, lakini ghafla akakumbuka kitu. Ni kwamba Betty atamkubalia hoja yake mara moja na ataachana na Isaya.
Ehe! Baada ya hapo!!
Hakuna jipya jingine Isaya ataendelea na maisha yake na atakuwa na msichana mwingine ambaye Joy hana mazoea wala ukaribu naye, hivyo Joy atazidi kuumia akimuona Isaya na msichana mwingine.
Joy akatambua kuwa alichokitaka yeye ni kuwa katika mahusiano na Isaya na wala si kwamba Isaya asiwe katika mahusiano na Betty.
Silaha kubwa na pekee ambayo ingeweza kuirejesha imani ya Isaya kwa Joy ni kiasi cha Joy kumtafuta na kumweka kitako kisha kumweleza kuwa msichana ambaye wapo naye katika mahusino ni mwathirika. Hivyo amemweleza hayo kwa sababu anampenda sana. Kwa kauli hiyo mwanaume yeyote duniani hawezi kuchomoka tena, na hatahitaji uthibitisho mwingine kujiaminisha kuwa anapendwa.
Lakini kumweleza Isaya hayo ni sawasawa na kumsaliti, tena usaliti mkubwa kwa Betty.
Kizungumkuti kikuu!!!
Joy akakosa maamuzi.
****
ISAYA AKUNAAY. Mtoto wa mbunge wa Geita mjini, alikuwa ameamua kumuumiza Joyce haswaa kwa akitendo chake cha kuingia katika mahusiano mengine na msichana mwingine ambaye ni mtu wa karibu wa Joyce.
Alijua kuwa taarifa zimemfikia tayari, lakini hiyo ilikuwa haitoshi bado alihitaji kufanya jambo kwa ajili ya kupigilia msumari wa mwisho.
Pesa huzungumza, hii ni kweli. Akiwa kitandani kwake akapata wazo la kumtambulisha Betty kwa marafiki zake na wanachuo wengine. Hakuwa na wasiwasi katika hili kwa sababu kwa kitendo chake cha kubadilika ili ampate Joyce hakuwa na wasichana wengine tena, hivyo hakutegemea mtafaruku wa aina yoyote ile. Na isitoshe alikuwa amepigiwa chapuo agombee nafasi ya uraisi wa chuo basi alihitaji kuwa mfano kwa wanafunzi wengine. Mfano katika namna ya kuishi na pia uwazi katika mahusiano.
“Yes! Ndege wawili kwa jiwe moja tu. Hapa namkomoa Kidoti na upande huu najijengea mazingira mazuri ya kuuchukua uraisi wa chuo.” Alishangilia Isaya huku akijirusha rusha kitandani kwake.
Wazo hilo halikuhitaji mshauri bali lilihitaji utekelezaji.
Siku iliyofuata akiwa na Betty ufukweni na wapambe lukuki kama kawaida alimweleza nia yake ya kufanya ‘engagement’ na kumvika pete rasmi kabla ya uchumba.
Kwanza Betty hakuamini kama Isaya alikuwa amezama kiasi kile, alidhani ni wale wanaume wa kuhitaji mapenzi tu na kisha kuendelea na mambo yao. Tangu atue jijini Dar es salaam hii ilikuwa mara ya kwanza kwa mwanaume kumtamkia juu ya kumtambulisha kisha uchumba na ndoa.
Mapigo ya moyo yakaongezeka kasi yake, hakika hili lilikuwa shambulizi la ghafla sana. Shambulizi lisilotegemewa kabisa.
Betty akashikwa na kigugumizi akakosa cha kusema, wakati huo tayari Isaya alikuwa amemvuta na kumlaza kifuani mwake.
Zile busara alizorithi kutoka kwa mtaalamu wa saikolojia na mapenzi bwana Matanuru sasa zikaanza kufanya kazi, akamshawishi Betty kwa maneno makali ya kimapenzi, sauti maridhawa kabisa ya kiume ikapenya katika masikio ya Betty na kisha kwa mara ya kwanza ikatua katika mtima wake.
Betty alikuwa amekutana na mwanaume ambaye ana hisia za hali ya juu kwake. Akajisikia vibaya kwa sababu hana msamaha kwa ajili ya mwanaume yeyote akajijutia kuupata Ukimwi akiwa bado mdogo.
Laiti ningekuwa salama ningenyanyua kinywa change na kukiri kuwa hatimaye nimempata mwanaume anifaaye!! Aliwaza Betty.
“Mbona kimya mamii.” Sauti ya Isaya ilimrejesha tena mahali pale.
“Hapana mpenzi basi tu nilikuwa nafikiria juu yako. Elewa kwamba wewe ni kila kitu kwangu, nilikueleza siku ya kwanza kuwa umenikuta mimi kama Betty na sasani Betty wa Isaya. Nakusikiliza wewe.” Betty alinong’ona kimahaba. Akamkosha Isaya. Kijana akambeba na kumrusha juu juu. Kisha wakakimbilia ndani ya maji wakikimbizana huku na kule.
Siku hii ikamalizika kwa furaha ya aina yake. Lile lengo la Isaya likapiga hatua moja mbele.
****
JOYCE alikuwa akingojea wakati ambao Betty atarejea aweze kuzungumza naye na kumweleza kitu ambacho kinaisumbua nafsi yake. Aliamini kuwa ni Joyce pekee awezaye kumshauri ama walau kumtia moyo juu ya kitu ambacho kinaendelea kusafiri katika moyo wake. Aliamini fika kuwa bila kulitatua tatizo hilo basi ajiandae kuanguka vibaya katika masomo yake jambo ambalo hakuwa tayari kulishuhudia kwa macho yake likitokea.
Masaa yakasogea hatimaye mlango ukagongwa, alikuwa ni Betty. Betty mwenye furaha tele.
Ni heri Betty angemwacha Joy azungumze kwanza, lakini ilikuwa bahati mbaya kwake maana Betty alianza kuzungumza kabla.
“Mwenzangu…..kuna wanaume wanapenda jamani. Eti katangaza uchumba mwenzangu duuh. Sema ni mtanashati ila ndo hivyo mi siangalii nyuma, hiyo sherehe nahudhuria, pete navikwa halafu usiku huo wa pete nampa na zawadi yake ya tamaa za kijinga jinga. Maskini Joram wangu. Pole yake.” Alizungumza Betty kwa papara huku akihesabu noti kadhaa alizopewa na Isaya aitwaye Joram kwa ajili ya kununua vazi maalum kwa sherehe ile na pia kwa ajili ya matumizi yake.
He! Wamefikia mambo ya uchumba tena? Mungu wangu Isaya anakufa jamani. Isaya wangu!! Alilalamika Joyce katika nafsi yake. Lakini kufikia pale hakuwa na kauli tena dhidi ya Betty.
“Sasa hapo najua atataka kunipeleka kwa mzee wake, huyo mbunge. Hapo ndo napataka sasa, si ifike hiyo siku ya kuvikwa pete mtoto wa watu mie. Duh sipati picha, shosti wewe usihudhurie maana nitaona aibu si unajua nipo kazini mimi.” Alizidi kubwatuka Betty bila kumpa nafasi Joy kusema lolote.
Joy alilazimisha tabasamu huku akijiona akiisindikiza safari ya Isaya kuelekea kaburini.
WAKATI Joyce akiwa aamsikiliza Betty, wafuasi wa Isaya akiwemo Matanuru ambaye alikuwa mshauri mkuu walikuwa wakipanga bajeti kuhusiana na sherehe hiyo.
Ukumbi, vinywaji, muziki, mapambo na mengineyo mengi vilikuwa katika orodha kuu.
Isaya alingojea tu kupewa jumla ya pesa inayohitajika.
Kubwa zaidi Isaya aliwahakikishia wajumbe wake kuwa patakuwepo na wabunge wasiopungua wanne pamoja na baba yake mzazi. Ilisisimua sana kuisikiliza habari hii.
Baada ya siku mbili habari hii ikatapakaa chuo kizima. Isaya anamvisha mtu pete. Kila mpenda sherehe aliingoja sherehe hii.
Sherehe ya mtoto wa mbunge.
****
UKUMBI ulikuwa umetapika haswaa, wenye nazo wachache walichanga pesa, mtoto wa mbunge akajazia za kwake na baba yake.
Waalikwa hawakutakiwa kuchangia chochote zaidi ya zawadi ambazo pia zilikuwa hiari. Isaya aliutazama ukumbi na kukiri kuwa hili ni pigo kwa Joyce Kidoti na pia ni nafasi ya yeye kujitangaza kisiasa hapo chuoni. Mzee wake alihimiza uhudhuriaji wa watu wengi ili kuzidi kumkita mtoto wake katika siasa ili ikiwezekana aweze kumrithi kiti chake cha ubunge wakati atakapostaafu.
Sherehe ikafana haswa!!
Kila jicho la mwsanaume lilimtazama Betty katika namna ya matamanio, wasichana wenye wivu walitafuta cha kukosoa wakakikosa, wakabaki kusema neno moja tu ambalo huenda lilikuwa na ukweli ndani yake.
Betty alikuwa akijilazimisha kutabasamu!! Japo alipendeza lakini lile tabasamu….lile tabasamu lilikuwa na utata…..
Lakini nani angejali kuhusu tabasamu wakati alikuwa ameng’ara?
Akavikwa pete Betty, akakumbatiana na mbunge wa Geita, na wabunge wengine watatu wa majimbo tofauti tofauti. Picha zikapigwa kwa wingi.
Wale wenye wivu nao wakajisemesha kuwa wanawatakia maisha mema wawili hao.
Isaya alitabasamu kutoka moyoni, alitabasamu kwa sababu alikuwa ni mshindi katika vita mbili. Vita ya mapenzi na siasa.
Lakini angetambua kuwa palikuwa na vita kubwa inamsubiri, vita yenye kuogofya na kufedhehesha basi asingeruhusu jino lake hata moja kutazamwa na watu.
Ama kwa hakika liishalo ni heri kuliko lijalo.
Hakulijua hili Isaya.
Majira ya saa sita usiku wale wapendanao walipanda katika gari la kifahari kuelekea katika hoteli ya kifahari katikati ya mji.
Jicho kali liliitazama ile gari, mwanaume akiwa amekumbatiana na mwanamke.
“Isaya….Isaya usife Isaya….nakuhitaji bado pliiz!!” mwenye lile jicho alisema kwa sauti ya juu kidogo kisha akajikurupua na kujiapiza kuwa alikuwa muuaji kuruhusu Isaya afanye zinaa na Betty muuaji wa kukusudia.
Lakini akiwa anawaza haya magari yalikuwa yametoweka tayari.
Joyce akataharuki, akahaha huku na kule. Alitamani kupiga mayowe kila mtu ajue kuhusu hatari iliyopo mbele yake.
Lakini mara akakumbuka kile kiapo cha kuitunza siri ya Betty, siri ya kuua maksudi kwa kuambukiza Ukimwi.
Nafsi ikamsuta akajiona mjinga sana anayeenda kujichumia dhambi ambayo anaweza kuiepuka.
Joy akaikumbuka ahadi ya Betty kuwa usiku huo ndio usiku wa kumpa zawadi Isaya. Zawadi ya kifo.
Kauli hii ikamsisimua na kumtoa katika pumbazo Joyce. Nguvu ya mapenzi ikamtekenya, ni kweli alikuwa anampenda sana Isaya, na sasa alikuwa anabariki mauaji haya ya maksudi.
Upendo gani wa kushindwa kutetea ukipendacho…
UTATA….
JOYCE akaamua kufanya jambo. Jambo ambalo badala ya kuwa utatuzi wa tatizo, jambo likazua jambo. Roho mkononi zikamzidia uzito, tamaa ya kuzishikilia zote tatu kwa pamoja ikamvuruga akili.
****Usiku wa BETTY kufanya mauaji umedwadia…ANA kwa ANA na ISAYA…..
***JOYCE atafanya nini??
NI UTATA…..
ITAENDELEA
Post a Comment