RIWAYA: ROHO MKONONI
MTUNZI: George Iron Mosenya
SIMU: 0655 727325
SEHEMU YA KUMI NA TATU
Siku ikawadia ya Betty kuonana tena na Isaya. Bila kujua Joy ni adui yake ndani ya nafsi kwa sababu ya Isaya alimweleza kila jambo lilivyo, muda na mahali ambapo watakutana na Isaya.
“Yaani huyu mkaka anaulilia ujira wake hadi namwonea huruma ati.” Alisema Betty huku akifanya maandalizi ya mwishomwisho kwa ajili ya kwenda kukutana na Isaya.
Joy alijilazimisha kutabasamu bila kusema neno lolote lile. Mapigo ya moyo yalianza kwenda kasi tena. Alikuwa anaingia tena katika vita ya aina yake, safari hii alikuwa hajajipanga kabisa japo awali pia hakuwa amejipanga kwa shambulizi lile.
Betty akaaga huku akimweleza Joy kuwa atakuwa akiwasiliana naye mara kwa mara kwa kila hatua atakayokuwa amefikia.
Joy alibaki nyuma akiumiza akili yake ni kitu gani anaweza kufanya ili aweze kumwokoa tena Isaya na janga hilo lililokuwa likielekea kumkabili.
Akili ilizunguka sana bila kupata suluhisho, hofu nayo ikazidi kumwandama.
Joy akatamani kumweleza Betty hata kwa njia ya simu juu ya utaabani wake juu ya penzi la Isaya, alitamani na angeweza kufanya hivyo lakini alijionya mengi sana ambayo yakakifanya kichwa chake kiume haswa.
Alikosa maamuzi!!
Mara akaamua jambo moja ambalo lilikuwa zito kukubaliana nalo kama litaweza kufanya kazi lakini aliamua kujiaminisha
Alitambua kuwa alikuwa na kipindi darasani muda huo ambao aliamua kuutumia katika kutimiza azma yake na kujiepusha na hatia ya nafsi kumsuta.
Kama alivyotarajia Betty alikuwa akimpa maelekezo kadha wa kadha juu ya wapi walipo na nini kinaendelea, hivyo hakuhangaika sana kutambua wapi pa kuanzia,lakini kigumu kilikuwa ni nani atamsaidia katika hili jambo.
Akiwa amekitoa muhanga kipindi cha darasani kwa ajili ya kumfuatilia Betty na Isaya, Joy aliamini kuwa kuna mtu alikuwa akimuhitaji ili aweze kumsaidia zaidi katika hili. Akakumbuka kuwa katika akaunti yake kuna pesa, ni lazima na yenyewe itumike ili jambo hilo liweze kwenda sawa.
Wakati akiumiza kichwa na huku dakika zikizidi kusogea mbele, mara akamkubuka Fonga, tabasamu likajisogeza kidogo katika himaya ya uso wake na kisha likatoweka upesi kama halikuwepo hapo kabla.
Hakika Fonga angeweza kumfaa zaidi kwa kipindi kile.
Huyu alikuwa ni kijana ambaye alikuwa shushushu wakati wa kinyang’anyiro cha taji la urembo hapo chuoni, huyu alikuwa kambi ya Kidoti. Alikuwa akizipata siri za wapinzani na kuzifujisha katika kambi anayoishabikia ili waweze kujipanga vizuri.
Fonga alikuwa mwingi wa maneno na kuna watu walikiri kuwa alikuwa na akili ya ziada nd’o maana aliwafaa sana.
Wagombea mbalimbali wa vyeo kadhaa hapo chuoni walipenda sana kumtumia katika kuzing’amua siri za wapinzani.
Kwa mtaji huu Fonga akawa anachuma pesa za wanaotaka kumtumia kujua mambo, kilichokuwa kizuri kwa Fonga alikuwa na timu yake ambayo watu wengi hawakuijua, ni jambo hili lilimpa wepesi katika kufanya ushushushu wake. Wakati kambi pinzani inategemea kumwona Fonga akianza kujisogeza, wanashangaa yupo amejikita na mambo yake lakini siri inapovuja ndipo hupagawa na kukiri kuwa Fonga ni kiboko.
Joyce, akaichukua simu yake na kuwapigia watu kadhaa baada ya dakika mbili akawa na namba ya Fonga kwenye simu yake. Upesi akaipiga namba ile.
Hakika alikuwa Fonga, Joyce akamsihi kuwa anahitaji mno kuonana naye. Fonga aliposikia kuwa anayemuhitaji ni Kidoti hakuwa na nafasi ya kukataa.
Mwanaume kwa mwanamke!!!!
Bahati ikawa upande wa Joyce, Fonga akafika upesi. Baada ya salamu mbili tatu, Joyce alimwelezea Fonga hali halisi juu ya kitu anachokihitaji kwa wakati huo. Aliufahamu vyema wivu wa wanaume hivyo hakutaka kumtajia Fonga moja kwa moja kuwa anamwokoa Isaya kutoka mikononi mwa Betty, bali alizuga kuwa anamuokoa Betty ambaye ni ndugu yake kutoka katika mikono ya Isaya.
“Yaani shida yangu ni kwa leo tu yaani. Tena leo yenyewe nd’o muda huu Fonga.” Alisihi Joyce, kisha akaendelea… “yaani huyo binti ni machachari sana….” Joyce alianza kuelezea kuhusu Betty na tabia zake, lakini hakuthubutu kusema kama ni muathirika wa gonjwa la Ukimwi,alieleza mengi ambayo Fonga aliyahitaji katika kutimiza shughuli yake.
Kwa mara ya kwanza akausikia moyo wake ukimshtaki kwa kumsema rafiki yake kipenzi mbele za watu baki wasiotambua historia iliyopo kati yao. Akaunganisha meno yake kwa uchungu lakini akakiri kuwa penzi lashinda nguvu ya kiapo.
Lakini hakutaka wazo hili lifikie jibu baya la kutoboa siri!!
Fonga akashusha pumzi kisha akamweleza Joyce kuwa hakika hakuwa amewahi kujihusisha katika ushushushu wa mapenzi kama alivyotaka yeye Joyce, lakini hili halikuwa jibu pekee aliloishia. Akampa moyo Joyce kuwa kwa sababu amesema ni kwa siku hiyo tu basi atamsaidia kwa kadri ya uwezo.
“Shilingi ngapi nikuandalie sasa.” Alihoji tena Joyce.
Hapa Fonga akawa mzito kiasi, kisha akamwambia ampatie pesa ya nauli tu ya taksi. Mengineyo watazungumza baadaye.
“Ujue nahofia kuchukua pesa yako kwa jambo la kushtukiza kama hili. Ngoja tupate matokeo kwanza.” Fonga alimwambia Kidoti. Kisha akamfanyia konyezo maridhawa.
Kidoti akajilazimisha kutabasamu. Akafungua pochi na kumpatia Fonga kiasi cha pesa, halafu akamkumbusha mahali ambapo walikuwepo wawili wale.
Fonga akatokomea.
Joyce akamtazama kijana yule kisha akakiri kwa imani nyake ya dini ambayo aliijulia ukubwani alikuwa anafanya makosa makubwa sana kumtegemea mwanadamu mwenzake, hiyo haikuwa na tofauti ya kumfanya Fonga kuwa Mungu wake.
Dhambi!!
Akainama kwa aibu tele.
Amemsaliti rafiki japo kwa siri chache, kisha ameisaliti na imani yake!!
Pabaya hapo…..
Mapenzi ni kitu gani??
*****
MAENEO ya Kinondoni Morocco, katika mgahawa wa Best Bite. Mgahawa maarufu jijini Dar es salaam. Betty na Isaya walikuwa wakipata kitu roho inapenda.
Isaya aliamua wapate chakula eneo lile kwa sababu tayari alikuwa amechukua chumba katika hoteli ya Chichi ambayo haikuwa mbali sana na maeneo yale.
Wote walikuwa wanafurahia ‘chicken chips’ iliyokuwa mezani. Betty aliwasifu kutokana na kuku wao wa kienyeji kuandaliwa katika namna ya kipekee inayovutia.
Isaya naye alisifia kile alichoweza ilimradi kuusindikiza mlo wao.
Walimaliza kwa kunywa juisi kushushia kile chakula.
Lakini Betty hakunywa sana ile juisi akaagizia mvinyo maridadi kabisa uliotengenezwa kwa zao la ‘rozela’. Mvinyo maalum kwa ajili ya kuchangamsha mwili.
Hakika ulikuwa unachangamsha!!
Taratibu huku mvinyo huku maji ya matunda, hatimaye walikuwa wameimaliza shughuli ya kukipata chakula.
Kilichofuata hapo ni kulipa bili kisha kuondoka, Betty akiwa nyuma ya Isaya ambaye alikuwa amekikamata kiganja cha Betty.
Haukuhitaji elimu ya chuo kikuu kutambua kuwa wale ni wapenzi. Tena wa siku nyingi tu.
Walipotoka waliangaza huku na kule kwa muda kisha wakaanza kujongea katika gari lao.
“Samahani bro…” Isaya aliitwa akageuka.
“Nani…mimi?” aliuliza kizembe huku akijiona ni yeye pekee ndiye yupo na jinsia ya kiume pale.
Kijana nadhifu aliyemuita akamsogelea kisha akamsalimia na kisha kumvuta kando kidogo, biula shaka Betty asiweze kusikia kitu chochote.
“Kaka samahani, nadhani huyu uliyenaye ni mpenzi wako.” Alielezea yule kijana. Isaya kwanza hakujibu swali lile, akamtazama vyema muulizaji.
“Aaah! Samahani kama nimeuliza vibaya lakini sisi tuna shida naye.” Aligandamiza tena kijana yule.
Shida gani na mpenzi wangu!! Alijiuliza Isaya. Lakini ni kama yule kijana alikuwa katika akili ya Isaya.
“Demu wako ni tapeli!!” alijibu kijana yule.
Hapa sasa Isaya akataka kugeuka mbogo, akajaribu kuidhibiti hasira yake. Akamtazama Betty aliyekuwa ametangulia ndani ya gari huku akiwa ameuacha mlango wazi.
Isaya alitamani kuwatukana vijana wale lakini ghafla akaonyeshwa kithibitisho cha kumkamata Joyce, yaani ‘RB’.
Hapa sasa Isaya akapagawa, jazba aliyokuwa nayo ikashuka.
“Afande Meku! Mchukue huyo.” Aliongea kiaskari sasa akiamrisha na sio kuomba, upesi mwanaume mwingine akaruka ndani ya gari kwa mbwembwe na machachari yote akamkwapua Betty. Akamshika mkono vyema kisha akmwingiza katika taksi waliyokuja nayo.
“Joraam…Joraam….sijaiba cha mtu mimi Joram, wazuie Joraaam…..” alilia huku akitapatapa Betty, kilio chake kikaufikia moyo wa Isaya. Akazidi kuhaha nini afanye lakini akapewa onyo kuwa akithubutu kufanya vurugu basi amelizuia jeshi la polisi lisiifanye kazi yake ipasavyo.
“Utakuja kumtoa kituoni na milioni tatu na laki sita za watu.” Yule bwana aliyekuwa anazungumza na Isaya aliruka garini upesi huku akimweleza Isaya maneno yale.
Hakuna aliyejua nini kinaendelea, Isaya alibaki katika hamaniko akijiuliza jambo kama hilo linatokeaje. Kilio cha Betty kikamfanya azidi kuumia nafsi.
Ghafla akajiona mpumbavu, akaikumbuka simu kutoka kwa baba yake kuwa kuna watu wabaya wanawafuatilia.
Maskini Isaya hakukumbuka hata kuomba vitambulisho vya watu wale!!!
Sasa Betty ametokomea na hajulikani alipo!! Hajui hata ni kituo gani cha polisi aende kumuulizia. Isaya akabaki mpweke eneo lile.
Akaamua kupiga simu kwa marafiki wa baba zake ambao ni maafisa wa juu wa polisi. Akawaeleza kilichotokea.
Taarifa zikasambazwa katika vituo kadhaa wakingojea Betty afikishwe kituoni ili Isaya aweze kupewa taarifa. Lakini kadri muda ulivyokwenda ndivyo hali ilizidi kuwa tata.
Jioni Joyce anapewa taarifa na baadhi ya watu kuwa mchumba wa Isaya, Betty ametekwa na hajulikani alipo.
Joyce akapagawa huku akiwa amesahau kabisa kuwa aliwahi kuzungumza na Fonga juu ya mpango wa kumchoropoa Betty kutoka katika mikono ya Isaya.
Hofu ikamtawala, akajitoa katika kundi la watu wengi akajiweka mahali na kumpigia simu Fonga.
Wapi!! Haipatikani. Hapa akazidi kujikuta katika sintofahamu ya aina yake. Akajaribu kumpigia Betty, na yeye hakuna kitu hapatikani.
Jasho likaanza kumtoka, na akajikuta akatika msimu mbaya wa majuto. Akahisi huyu majuto amekuja kabla hajawa mjukuu.
Ilikuwa mapema sana kujutia maamuzi yaliyotoka ndani ya dakika kadhaa nyuma. Lakini atafanya nini wakati hali ilikuwa namna ile.
Usiku ukafika!!
Betty hajulikani alipo bado!!!
Joyce akiwa kitandani aliikosa amani kabisa. Alishindwa kulala bila kuwa anafahamu hatma ya Betty. Alihaha huku na kule.
Akajikuta akitamani kurudisha muda nyuma asiweze kufanya jaribio alilofanya la kumdhibiti Betty asimwambukize Isaya Ukimwi lakini sasa anajikuta ile roho mkononi ambayo ni halali ya Betty ikikaribia kumponyoka, hakujua nini kimetokea kiuhakika lakini alisikia kuwa ni wateka nyara wamemkwapua Betty mikononi mwa Isaya kwa kujifanya kuwa wao ni polisi na wamekuja kumkamata Betty kwa shutuma za kufanya udhulumaji wa pesa taslimu shilingi milioni tatu na ushee.
Taarifa hii ikamfanya Joyce aamini kuwa huenda Betty alikuwa amekamatwa na wale vibopa ambao aliwaambukiza Ukimwi huku akifanikiwa kuzitwaa pesa zaona kisha kutokomea bila kuaga.
Lakini akiwaanapitiwa na mawazo haya mara simu yake iliita.
Hii ilikuwa ni namba mpya akapokea upesi kabisa.
“Kidoti…..Fonga naongea hapa!!” alijitambulisha kisha akaacha nafasi kidogo ya jina lake kumuingia msikilizaji.
“Fonga,nini kimetokea kwani eeh!! Fonga amefanya nini Betty kwani..”
“Punguza papara Joy. Hili jambo ni zito kiasi fulani na hata mimi linanichanganya sana, sijui tu hata nikuelezeeje lakini naomba uelewe kuwa vijana wangu hawakufanikiwa kumpata Betty.wamefika eneola tukio lakini hawakumkuta na baadaye nasikia kuwa ametekwa.” Alijibu Fonga kwa sauti tulivu.
Acha wee! Hapa sasa Joyce akaruka kutoka kitandani akaanza kupiga mayowe huku akijisahau kuwa simu yake bado ipo hewani.
Akalia akimuita mama yake ambaye ni marehemu tayari.
Simu kutoka upande wa pili ikakatwa!!
Joyce akauhisi ule upendo ambao alidhani unatoweka kwa Betty ukirejea maradufu na kujikuta akijutia kila kitu, hakutaka kuamini kuwa Fonga hajui lolote.
Akajutia kumuamini na kumvujishia baadhi ya siri kuhusu Betty.
Alipokuja kutulia na kujaribu kupiga simu tena Betty hakuwa akipatikana.
HEKAHEKA!!!!
****BETTY ametoweka katika mazingira tatanishi…FONGA hajui, JOY hana habari na ISAYA yu katika kizungumkuti….
***NINI KIMETOKEA katika mkasa huu….na ni nani aliyemteka Betty….
ITAENDELEA ……
LIKES, SHARES na COMMENT kama tuko pamoja
Post a Comment