Ushoga ni mbaya kuliko ufisadi?


KWA kweli nilishitushwa na ukali wa mjadala ulioibuka bungeni na nje ya Bunge baada ya Mbunge wa Nyamagana (CHADEMA), Ezekiah Wenje, hivi karibuni, kukihusisha Chama cha Wananchi (CUF) na ushoga kutokana na chama hicho kuwamo katika kundi la vyama vya kiliberali, ambamo mwelekeo wa sehemu kubwa ya vyama katika kundi hilo ni kuunga mkono ushoga.
Mabishano yaliyokuwapo bungeni yalikuwa makali kiasi kwamba ilibidi Naibu Spika, Job Ndugai, afanye uamuzi wa kuahirisha kikao cha Bunge. Naambiwa mjadala uliendelea kuwa mkali kwenye viwanja vya Bunge baina ya wabunge wa vyama hivyo viwili.
Nimeshuhudia wabunge wakiitana majina ya ajabu bungeni. Majuzi tu hapa mbunge mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Peter Serukamba, naye alitukana  ndani ya ukumbi huo wa Bunge lakini ukali na hamaki iliyokuwapo haikukaribia hata nusu ya mjadala huu wa ushoga.
Nimejiuliza maswali mengi lakini moja kubwa ambalo ni je; ushoga ni uovu au tatizo kubwa zaidi kuliko ufisadi? Je, chama kutetea au kutotetea mashoga kuna athari zozote kwa taifa letu?
Mojawapo ya matatizo makuu ya jamii nyingi duniani kuhusiana na masuala ya ushoga ni kukataa kuyajadili hadharani. Hili limekuwa ni suala la marufuku na matokeo yake watu wengi hata hawafahamu wanachokichukia au wanachokikubali na badala yake wanashikilia tu misimamo yao kwa kusingizia dini au mila na desturi.
Na sababu za kidini na kimaadili zimetumika mara nyingi tu kwenye unyanyasaji wa makundi fulani ya watu. Enzi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini na kwingineko duniani ambako watu weusi walitendewa vibaya kuliko hata wanyama, dini ilitumika kutetea unyama huo.
Kwenye mafunzo ya dini ya makaburu, wayahudi na wabaguzi wengine, watu wanafundishwa watu weusi ni zao la mtoto wa Nabii Nuhu aliyeitwa Ham anayedaiwa kumchungulia baba yake akiwa utupu.
Kwamba baada ya baba yake kugundua, alimlaani na kuanzia hapo akawa mweusi na asili ya mtu mweusi ikaanzia hapo. Hii maana yake ni kwamba watu weusi ni waliolaaniwa na Mwenyezi Mungu.
Kwa Kaburu aliyepitia mafunzo hayo ya dini, huwezi kumweleza kitu kuhusu mtu mweusi na akaelewa. Hata hivyo, ukisoma maandishi tofauti tofauti ya biblia na sayansi, haileti mantiki kwa mtu kutoa laana ya kumfanya mtu atoke kuwa mzungu na au mhindi na awe mchina au mwarabu.
Biashara ya utumwa iliendeshwa pia kwa propaganda hizi. Mtu alikuwa ni mchungaji, shekhe au padri lakini alikuwa na watumwa wake. Na wala hakuona kosa lake kwa sababu alifunzwa kwamba mtu mweusi ni laana tupu.
Kadhia hii ya mashoga imewakuta pia wanawake. Wapo waliokuwa wakisema wanawake hawana haki zozote kwa sababu ndiyo waliosababisha Adamu ale tunda na kusababisha hasira ya Mwenyezi Mungu kwa wanadamu.
Ilifikia wakati, kwenye kitabu cha biblia, mwandishi anaandika kwamba katika mkutano fulani wa kidini, wanaume kadhaa walihudhuria. Wanawake hawakuwa chochote wala lolote. Hawakufaa hata kuhesabiwa.
Katika mojawapo ya hekaya za Wagiriki nilizowahi kusoma, inadaiwa kuna kipindi Wagiriki walikuwa wanaoana wanaume kwa wanaume kwa sababu walihisi mwanamke ni kiumbe cha chini mno kuwa na uhusiano nacho. Ni afadhali uoe mwanamume mwenzako kuliko mwanamke.
Na ukichunguza, utaambiwa hizo zilikuwa mila na desturi zao au mapokeo ya kidini.
Kimsingi, sababu zote hizo zilizotumika kuwanyanyasa na kuwatenga watumwa, wanawake na watu weusi siku za nyuma na hata leo, ndiyo hizohizo zinazotumika dhidi ya mashoga kwenye kizazi hiki.
Hoja yangu kubwa ya leo ni kwamba mapokeo ya kimila au kidini kuhusu jambo lolote si lazima yawe sahihi na watu hawatakiwi kuwa wagumu kubadilika kwa sababu ya kulinda mapokeo hayo.
Wiki iliyopita, katika mijadala iliyokuwapo katika mitandao ya kijamii, mtu mmoja alinishambulia kwa msimamo wangu wa kutaka mashoga wasinyanyaswe au kutendwa kama wanyama. Alishutumu kwamba mimi napenda sana umagharibi.
Jina lake alikuwa anaitwa Alphonce Godfrey. Nikamuuliza maswali mawili tu; kama yeye hapendi umagharibi, mbona jina lake ni la kimagharibi? Pili, hivi watetezi wote wa haki za wanawake ni wanawake?
Au unapotetea haki za wanyama ni lazima na wewe uwe mbwa au tembo? Nafikiri watu wengi wameshindwa kutetea haki za mashoga kwa hofu ya kuonekana ni mashoga.
Wikiendi iliyopita, nimesoma makala moja katika gazeti moja la hapa nchini ambapo shoga mmoja wa kiume amelalamika kwamba anavamiwa na vijana nyumbani kwake na kubakwa mara kwa mara.
Hakuna anayemsaidia kwa vile yeye ni shoga. Akienda polisi, anawekwa katika mahabusu ya kiume kwa vile yeye ni mwanamume. Matokeo yake anabakwa na mahabusu wenzake. Kwa sasa ameathirika na Ukimwi, lakini wabakaji hawajui na wanaendelea tu.
Vitendo hivi vya wanasiasa na watu wenye ushawishi kwenye jamii yetu kupaniki kwa sababu tu wameambiwa wana uhusiano na ushoga vinaongeza ugumu wa maisha ya wenzetu hawa.
Na kutumia ushoga kama silaha ya kumshinda mpinzani wako kisiasa katika nchi ambayo uelewa wa mambo ni mdogo kama Tanzania nayo pia ni makosa.
Kuna wanaoamini kwamba mashoga wanazaliwa kuwa hivyo. Ni masuala ya homoni na jenetiki ndiyo yanayosababisha hivyo. Sawa sawa na mtu kuzaliwa kuwa albino. Kama unatetea maalbino wasiuawe, huna haki ya kumshutumu anayetetea mashoga.
Madaktari wanasema ushoga unatokana na mazingira anayokulia mtu. Kama ambavyo hakuna mtu anayezaliwa teja, mwizi, jambazi, mlevi au mwasherati, ndivyo hivyo anavyozaliwa shoga.
Kama tunaishi na familia zetu na walevi, majambazi, mateja na mafisadi wengine, tunashindwaje kuishi kwa namna hiyohiyo na mashoga?
Maisha yetu yana unafiki mbaya sana. Kuna watu ambao wanafahamika kwamba ni mafisadi, walevi, waasherati, wauaji na wahaini lakini wanasali kila wiki, wanachaguliwa kuwa viongozi na michango yao inapokewa misikitini na makanisani.
Hebu fikiria itakuaje siku ambapo shoga ataingia kanisani au msikitini na kuomba kuchaguliwa kuwa kiongozi au kutoa mchango wa kutaka kujenga chochote? Nina imani watu wataihama nyumba hiyo ya ibada.
Mashoga na ushoga vimeishi na mwanadamu kwa miaka mingi, mingi sana. Hautaondoka kwa sababu mimi na wewe tunachukia. Hautaondoka kwa sababu tukiitwa mashoga tunataka kukunja ngumi na kutoa ngeu.
Katika ngazi ya familia, tuwakuze watoto wetu kimaadili na kidini. Viongozi wa dini, wafanye kazi zao kwenye nyumba za ibada na nje ya hapo.
Kinachobaki, tumwachie Mwenyezi Mungu. Mwisho wa siku yeye ndiye atakayetuhukumu sote… Mashoga na Wasio Mashoga
source: Raia Mwema:  Ezekiel Kamwaga

Post a Comment

Previous Post Next Post