Baada ya Tanzania kutema cheche; Marekani yaunga mkono kupeleka brigedi maalumu DRC

Picture
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bw. John Kerry, akizungumza wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, uliokuwa ukijadili hali katika eneo la Maziwa Makuu na uungaji mkono Mpango Mpana wa Kisiasa wa Umoja wa Mataifa wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Maendeleo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Maziwa Makuu.
Imeandikwa na Mwandishi Maalum, Umoja wa Mataifa, NY — Wakati  hali ya usalama  ikiendelea kuwa tete Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,  kufuatia   kuibuka upya kwa  mapigano hivi karibuni. Marekani  imetamka bayana mbele ya Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa,  kwamba, inakaribisha na kuunga mkono upelekaji wa  Brigedi Maalum ( Force Intervention Brigade) pamoja na mamlaka iliyopewa kupitia Azimio namba 2098 la 2013.

Brigedi  hiyo Maalum inaundwa  na wanajeshi kutoka Tanzania,  Afrika ya Kusini na Malawi. Na imepewa mamlaka na Baraza  Kuu la  Umoja wa Mataifa ya, pamoja na mambo mengine, kuyakabili na kuyadhibiti na ikibidi kutumia nguvu  za ziada pamoja na kuyapokonya silaha makundi ya wanagambo  wakiwamo M23 na FDRL.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bw. John Kerry ameyasema hayo wakati alipokuwa akiongoza mkutano  wa Baraza Kuu la Usalama katika  ngazi ya  Mawaziri  ulioandaliwa na Marekani ambaye  ndiyo Rais wa Baraza hilo  kwa Mwezi huu wa Julai.
Picture
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akizungumza kwa niaba ya Serikali.
Ajenda iliyoandaliwa na Marekani na kujadiliwa na Baraza hilo  siku ya Alhamisi  ilihusu hali katika Eneo la Maziwa  Makuu na Uungaji  mkono Mpango Mpana wa Kisiasa wa Umoja wa Mataifa wa Amani , Usalama na Ushirikiano wa Maendelea katika DRC na eneo la Maziwa Makuu (PSC Framework).

Anasema  Bw. Kerry “ Marekani  inakaribisha upelekaji wa  Brigedi Maalum na inaunga mkono mamlaka iliyopewa ya  kutangua makundi yote  ya wanamgambo yenye silaha, na kuwalinda raia ili hatimaye Amani iweze kutawala”

Amesisitiza kwa kusema,  Marekani  inaunga mkono  jitihada zote za kutafuta Amani katika DRC ikiwa ni
pamoja na kuziunga mkono  nchi 11 na wadhamini wanne (11+4) waliotia saini mpango mpana wa kisiasa na kwamba itashirikiana nao katika  utekelezaji wa mpango huo.

Hata hivyo amesema, nchi yake inasikitishwa  sana na taarifa  mpya na za hivi karibuni zinazoonyesha kwamba bado makundi ya waasi ya M23 na FDRL  yanaendelea kupewa misaada kutoka nje.

Na kwa sababu hiyo, amesisitiza kwa kuzitaka pande zote zinazohusika kuacha mara moja kuyasaidia makundi hayo na kwamba kila nchi  ihakikishe wale wote wanaokiuka haki za binadamu wanachukuliwa hatua na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kama hiyo haitoshi Bw. Kerry ametoa changamoto kwa nchi zote ambazo zimetia saini PSC Framework kuheshimu  na kutoiingilia  DRC  katika mambo yake ya ndani  ikiwamo mipaka yake.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  Ban Ki Moon, Mshauri wake Maalum katika Maziwa Makuu, Bi. Mary Robinson,  Mawaziri kadhaa  wakiwamo wa kutoka nchi za Maziwa Makuu, SADC, EU, na Umoja wa Afrika na   Mkuu wa Bank ya Dunia aliyeongea kwa  njia ya  Video  kutokea Washgton DC.

Waziri  huyo wa Marekani pia amesema suala la eneo la Maziwa Makuu na DRC ni  moja wapo ya vipaumbele vya serikali ya Rais Obama na kwamba kwa kuutambua umuhimu huo,  Obama amemteua, Seneta mstaafu, 
Picture
Taswira ya Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ulivyokuwa siku ya Alhamisi wakati wa mkutano uliojadili hali katika eneo la Maziwa Makuu, mkutano huo ulihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, Mwakilishi wake wa Maziwa Makuu Mary Robinson, Mawaziri kutoka nchi za Maziwa Makuu, SADC , Umoja wa Afrika, EU, na Mkuu wa Banki ya Dunia aliyeongea kwa njia ya Video kutokea Makao Makuu ya Banki hiyo jijini Washington.
Bw. Russ Feingold  anayetajwa kuwa na uzoefu na utaalam mkubwa  kuhusu masuala ya Afrika kuwa Mjumbe Maalum wa Marekani katika Maziwa Makuu.

Miongoni mwa nchi chache  nje ya wajumbe wa Baraza Kuu zilizokaribishwa  kuzungumza katika mkutao huo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza kwa  niaba ya Serikali, Balozi Tuvako Manongi aliweka bayana msimamo wa Tanzania kuhusu suala zima la  ushiriki wake katika mchako mzima wa utafutaji wa Amani ya kudumu katika DRC.

Katika mchango wake Balozi Manongi alianza kwa kulikumbusha   Baraza Kuu la Usalama  tamko  la  Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwamba,   suluhu ya upatikaji wa  Amani ya kudumu katika DRC haiwezi kuwa kwa njia za kijeshi bali ni kwa  mchakato wa kisiasa na ambao  nyuma yake kuna utekelezaji  wa PSC Framework.  Na kwamba  suala la kuyahusisha makundi yote katika majadiliano bila ya kubaugua haliepukiki.

Na kwa sababu hiyo akasema  ndiyo maana  Tanzania inaunga mkono  na kushiriki  juhudi zote za  kimataifa na kikanda zikiwamo za utekelezaji wa mpango mpana wa kisiasa,  pamoja na  utoaji wa wanajeshi wake kushiriki katika Brigedi Maalum kama sehemu ya MONUSCO kwa mamlaka iliyoainishwa katika Azimio namba 2098(2013) la Baraza Kuu la Usalama.

Akasema  Brigedi hiyo Maalum inahitaji kuungwa mkono na watu wote na hasa kutoka Baraza Kuu la Usalama.

Akasisitiza kwamba  Brigedi  Maalum  haipashwi  kuvunjiwa heshima kwa tuhuma za uongo na zisizokuwa na  ushahidi wowote.

Balozi Tuvako Manongi amesema  katika siku za hivi karibuni kumeibuka tuhuma dhidi ya uongozi wa juu wa  Brigedi Maalum na kwamba tuhuma hizo za kuwapaka matope wale wote ambao wamejitolea kwa nia njema kusaidia katika  eneo la Mashariki ya Kongo, zinatia shaka.

Na kwa sababu hiyo  Tanzania kupitia Mwakilishi wake huyo imelitaka Baraza Kuu la  Usalama, lidai ushahidi dhidi ya tuhuma   ambazo zimekuwa zikielekezwa kwa Uongozi wa Juu wa  Brigedi Maalum

Akalikumbusha Baraza Kuu kwamba hata Tanzania iliwahi kupata  heshima ya kuwa mjumbe wa Baraza hilo, heshima ambayo iliibeba kwa dhamana kubwa , ikikatekeleza wajibu wake kwa uadilifu wa hali ya juu kwa sababu ilitambua  iko ndani ya chombo hicho kuiwakilisha Afrika na Jumuiya ya Kimataifa kwa ujumla na kamwe si  kwa maslahi binafsi au  kuitumia vibaya nafasi hiyo.

Akasisitiza kwamba  lazima Baraza Kuu la Usalama  lichukue hatua madhubuti za kuwalinda wale ambao wamekabidhiwa jukumu  hilo adhimu.

Aidha akasema Tanzania inalipongeza Baraza  Kuu la Usalama  kwa kuendelea kuunga mkono MONUSCO katika utekelezaji wa  mamlaka iliyokabidhiwa licha  ya  mlolongo wa  kampeni chafu kutoka kwa makundi ya waasi na waharibifu wengine.

Akasema Tanzania inaamini kwamba, kampeni hizo chafu na tuhuma zisizokuwa na ukweli dhidi ya Brigedi Maalum zinalenga kudhoofia utekelezaji wa mpango mpana wa kisiasa na kudhoofidha mamlaka ya  MONUSCO.

“ Tunaamini  jumuiya ya kimataifa itashinda, hakuna nguvu au propaganda chafu zitakazodhoofisha kiu  ya kutafuta amani, usalama na  ustawi katika eneo la Maziwa Makuu.  Huu ndiyo Mpango wa Matumaini ambao Tanzania  inaunga na itaendelea kuunga mkono.” Akasisitiza Balozi Manongi.

Baadhi ya nchi zilizozungumza zikiwamo Ufarasa na Uingereza   zimeunga mkono mchakato wote wa upelekaji wa Brigedi Maalum huku Uingereza ikisema  tuhuma za uongo na zisiokuwa na ushahidi dhidi ya Brigedi hiyo hazina maana  yoyote na zinalenga  kudhoofisha upatikanaji wa Amani. Na ikatakakuharakishwa upekelekaji wa teknolojia ya kisasa ya ndege ambazo haziendeshwi na binadamu ( UAVs)

Waziri kutoka Ufaransa yeye alikwenda mbali Zaidi kwa kuitaka FIB ianza kazi haraka iwezekanavyo.

Mwishoni mwa mkutano huo  ilitolewa  taarifa ya  Rais wa Baraza Kuu, taarifa ambayo pamoja na mambo mengine  ilielezea uungwaji mkono wa  Brigedi  Maalum, huku ikitaka makundi ya waasi wanaopigana  kuacha mara moja mapingano

Post a Comment

Previous Post Next Post