Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa tuhuma nzito kwa Jeshi la
Polisi, baada ya kudai askari wake kuvamia nyumba ya Mwenyekiti wa chama
hicho, Freeman Mbowe kwa nia ya kumkamata.
Tuhuma hizo
zimetolewa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Ukombozi eneo la Manzese jijini
Dar es Salaam jana.
Mkutano huo uliitishwa kwa ajili ya kutoa tamko kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya kwa wanachama na wafuasi wa chama hicho.
Dk. Slaa
alisema polisi wakiongozwa na mkuu wa upelelezi mkoa wa Kinondoni,
walivamia nyumba ya kiongozi huyo juzi usiku majira ya saa 6.55 na
kulazimisha kuingia ndani kwa ajili ya kumkamata.
Alisema
kitendo hicho alichokiita kuwa ni kinyume na utaratibu, kilifanywa huku
ikiwa imepita siku nne tangu Rais Jakaya Kikwete kuliagiza jeshi hilo
kuacha tabia ya kuwaandama wapinzani.
"Tunataka
maelezo kwanini polisi wavamie nyumba ya Mbowe katika muda huo ambao
kisheria hawaruhusiwi kumkamata kutokana na hadhi yake," alisema Dk.
Slaa.
Aidha,
alilitaka jeshi hilo kuomba radhi kutokana na kitendo hicho alichokiita
cha udhalilishaji kwa Mwenyekiti wao wa chama, Kiongozi wa kambi ya
upinzani Bungeni na Mbunge wa Jimbo la Hai.
Aliwaambia
wafuasi wa chama hicho kuwa vurugu zinazotokea sehemu mbalimbali nchini
zinatokana na jeshi hilo kufanyakazi kwa upendeleo na bila kufuata
taratibu za kazi.
"Polisi
hawakuleta barua ya kumkamata au kutakiwa kwenda ofisini kwao, kibaya
zaidi kutokana na wadhifa wake hastaili kukamatwa baada ya saa 12:00
jioni, kinachofanyika sasa ni ukandamizaji wa hali ya juu," alisema.
Akijibu
tuhuma hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura,
alimtaka Dk. Slaa akasome sheria ya polisi vizuri kabla ya kutoa tuhuma
hizo.
Alisema
polisi wana mamlaka ya kukamata mtu wakati wowote na kwamba kumkamata au
kutomkamata liko ndani ya jeshi la polisi, hivyo hawezi kutoa maelezo
yoyote.
Awali,
wakitoa tamko la chama hicho, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki,
Tundu Lisu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando walisema
chama hicho kinaunga mkono Rasimu ya Katiba Mpya iliyotolewa na Jaji
Joseph Warioba.
Walisema
wanashangaa kwanini CCM inapinga baadhi ya mapendekezo yakiwamo ya
kuundwa kwa serikali tatu na tunu ya Taifa, ikiwa vifungu hivyo vinataka
kuiweka Tanzania katika hali bora na udhibiti wa maliasili.
Lisu
alitahadharisha Watanzania wawe tayari kupiga kura ya kudai Uhuru endapo
Serikali ya CCM itaendelea kutumia nguvu kuifanya nchi kuwa ya serikali
mbili ambayo imeonekana kuparaganyika.

Post a Comment