Dk. Slaa awavaa CCM

ATAKA UBABE WAKE UDHIBITIWE NA GEORGE MAZIKU NA ASHA BANI

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema kama utawala wa kimabavu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ukiachwa uendelee, itafika mahali viongozi wake watataka kuabudiwa kama miungu.

Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la kimataifa la vijana kutoka vyama vya kidemokrasia duniani (IYDU).

Alisema kuwa Tanzania ina upungufu mkubwa wa demokrasia na pengine upungufu mkubwa zaidi wa utashi wa chama tawala kuruhusu demokrasia ya vyama vingi.

“Ikiwa mfumo huu wa utawala wa kimabavu utaendelea, viongozi wetu wataanza kujiita kwa vyeo vya kikoloni kufuatia majina yao kama vile, Mheshimiwa A.N. jingine ; K.C.M.G; Mheshimiwa B.N. jingine G.C.M.G,” alisema.

“K.C.M.G linamaanisha Keep Calling Me God, yaani endelea kuniita Mungu na G.C.M.G linamaanisha God Calls Me God, yaani Mungu huniita Mungu,” alifafanua.

Dk. Slaa alibainisha kuwa hulka ya chama tawala nchini kutegemea mabavu kuongoza nchi inatokana na chama hicho kudumu madarakani kwa zaidi ya miaka 27 peke yake bila kuwepo vyama vya upinzani.

Alisema kipindi hicho kirefu ambacho CCM ilitawala bila kuwepo upinzani iliwafanya viongozi wake waamini kuwa wanayo haki ya kuitawala Tanzania peke yao.

“Kama inavyoeleweka kuwa madaraka hulevya, madaraka makubwa kupindukia hulevya zaidi. Viongozi wetu waliamini katika matumizi ya madaraka ya kisiasa ili kudumisha utawala wao. Waliwatazama wapinzani wote kwa ghadhabu bila kujua kuwa ghadhabu ni jambo la hatari,” alisisitiza.

Alisema kuwa kwa sasa CHADEMA inaandamwa vikali na taasisi mbili za kiserikali ambazo ni Msajili wa Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi.

Aliongeza kuwa msajili amekuwa akitishia kukifuta chama hicho huku polisi wakiwaandama viongozi na wanachama wa CHADEMA, na watu wengine wote wanaojitokeza kuwatetea.

Alibainisha kuwa hali hiyo inatokana na tangazo la hivi karibuni la chama chake kwamba kinaanzisha mafunzo ya ukakamavu kwa vijana wake ili waweze kutoa ulinzi kwa viongozi wao na mali za chama hicho.

Alisema kuwa pamoja na kwamba mafunzo hayo yamo katika katiba ya chama chao iliyosajiliwa na msajili wa vyama vya siasa, na pia kuruhusiwa na sheria za nchi, amekuwa akidai mafunzo hayo yanakiuka sheria na kutishia kukifuta.

Aliongeza kuwa wakati msajili akitishia kuifuta CHADEMA, polisi wamekuwa wakiendeleza harakati za vitisho vya kuwakamata na kuwashtaki.

Dk. Slaa alisema matukio ya siku za karibuni ya polisi kuzidi kuwaandama viongozi wao na kufikia kuwavamia majumbani wakiwa na silaha nzito, yamezidi kuwatia woga.

Hata hivyo, Dk. Slaa alisema kuwa vikwazo vinavyowekwa na CCM dhidi yao ni ufunguo wa kufikia malengo yao ya kuwapatia wananchi nguvu ili wazitumie nguvu hizo kuilazimisha serikali yoyote kuwajibika kwao kwa kutekeleza matakwa yao.

“Mafanikio makubwa yanahitaji ukakamavu. Tuna haki kama chama kilichosajiliwa kisheria kujilinda sisi na mali zetu,” alisisiza Dk. Slaa.

Chanzo - Tanzania Daima

Post a Comment

Previous Post Next Post