Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wakazi wa mkoa wa Lindi
kuhakikisha kuwa vijana wao wanaishi maisha ya uadilifu, wanamcha
Mwenyezi Mungu na kusoma elimu ya Dunia ili wasipotee katika Ulimwengu
wa utandawazi.
Mama Kikwete ametoa wito huo wakati wa futari iliyowajumuisha viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya siasa mkoani Lindi.
Amesema
kuwa ni jambo jema kwa binadamu kuishi maisha ya kumpendeza Mwenyezi
Mungu, kwani hakuna mtu anayejua siku yake ya kufa, hivo basi ni muhimu
kujiandaa mapema kwa kutenda matendo mema ili ukifika huko uwe na
mazingira mazuri ya baadaye na hakuna cha kusema kuwa mimi ni mdogo
bado, kwani kwa Mungu hakuna cha mdogo wala mkubwa.
Ameongeza
kuwa kufunga kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani ni lazima, kwani ni
moja ya ibada katika kutengeneza afya ya mwili wako na kuwa karibu na
Mwenyezi Mungu na ndiyo maana hata watoto wadogo wanatakiwa kujifunza
kufunga.
Lakini
siku hizi kufunga imekuwa ni mtihani kwa baadhi ya watu, kwani kuna
wengine wanasingizia ugonjwa ili wasifunge, jambo ambalo si sawa kwa
sababu kuna baadhi ya watu wanaugua ugonjwa wa kisukari na wanafunga
lakini hawapati matatizo, kwa kuwa ukidhamiria utafunga tu bila tatizo
hata kama ni mgonjwa na Mwenyezi Mungu atakupa uzima.
Aidha
Mama Kikwete pia amewataka viongozi hao wa Serikali na vyama vya Siasa
kutunza amani iliyopo, kwa kuwa amani ni tuzo ya taifa na nchi bila
ya kuwa na amani haikaliki na hakuna jambo lolote linaloweza kufanyika
kwani hata wanyama watapata tabu na kukosa mahali pa kuishi.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi Ludovick Mwananzila amemshukuru Mama
Kikwete kwa futari aliyoiandaa kwa ajili yao na kusema kuwa, dini zote
zinahimiza umuhimu wa kusali na kutubu hivyo basi ni jukumu la kila mtu
kufanya hivyo.
Mkuu
wa mkoa huo amesema kuwa kila mtu anatakiwa kumcha Mungu na kumtukuza
bila kusahau kuwasaidia watu waliopo katika dhiki, ambao wanatakiwa
kusaidiwa kwa kufanya hivyo watapata thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Naye
Shekhe na Kadhi mkuu wa mkoa wa Lindi Mohamed Mushangani amesema kuwa
utaratibu wa watu wa aina mbalimbali kukutana na kufanya jambo kwa
pamoja, kunawafanya wapendane zaidi kwani mtu akikupenda nawe utampenda,
hivyo basi wawe na mapenzi na kupendana ili wapate raha katika maisha.
Amesema
kuwa katika kumi la pili la kufunga ni la msamaha kama alivyosema Mtume
Swalallahu Alayhi Wassalam (S.A.W), hivyo basi kwa wale wanaofunga
wanatakiwa kujikita zaidi katika kufanya mambo mazuri kwa watu ikiwa ni
pamoja na kulisha wengine, kwani ukimpa kula na kunywa mwenzako
Mwenyezi Mungu anakulipa zaidi.
Post a Comment