RPC, RCO WAGEUKANA
KUNDI la polisi wenye silaha za moto jana usiku walivamia nyumbani kwa
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Freeman Mbowe, kwa nia ya kumkamata.
Askari hao wanaokisiwa kufikia saba, wakiwa na silaha nzito katika gari
la wazi waliwasili nyumbani kwa Mbowe majira ya saa saba na nusu usiku
na kuwaamuru askari wanaolinda nyumbani kwake kumtoa Mbowe nje ili
waonane naye.
Walinzi wa Mbowe walihoji uhalali wa ukamataji huo na kuwataka polisi
wawaoneshe hati ya kumkamata, lakini hawakuweza kuionesha, hali
iliyozusha wasiwasi kwa walinzi wa kiongozi huyo.
Hata hivyo walinzi hao waliwaambia polisi hao kuwa Mbowe ambaye pia ni
kiongozi mkuu wa kambi ya upinzani bungeni alikuwa safarini, jibu ambalo
lilipokewa kwa shingo upande na askari hao.
Polisi hao baada ya kuona wameshindwa kukamilisha kazi hiyo, waliwaachia
walinzi hao namba ya simu 0754-085600 ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa
Kipolisi wa Kinondoni, Ernest Kimola, wakiwaagiza kuhakikisha
wanamwambia Mbowe awasiliane na kamanda huyo.
RCO amsukumia RPC, akana
Hata hivyo, alipohojiwa na Tanzania Daima Jumapili kwa njia ya simu,
Mkuu wa Upelelezi Kimola aligoma kuzunguzia suala hilo na kumtaka
mwandishi kuwasiliana na mkuu wake wa kazi, ambaye ni Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Kinondoni, Kamilius Wambura, akidai ndiye mwenye haki ya kutoa
ufafanuzi wa jambo hilo.
“Unajua mimi si msemaji wa polisi, wasiliana na kamanda wa mkoa, maana
ndiye mwenye uwezo wa kutoa maelezo,” alisema Kimola na kukata simu.
Lakini alipopigiwa simu Kamanda Wambura aliruka kimanga, kwa mshangao,
akidai kutojua lolote kuhusiana na polisi kuvamia nyumbani kwa Mbowe.
“Kwa kweli ndiyo napata taarifa hizo kutoka kwako, kuwa kiongozi huyo
alifuatwa na polisi, maana silijui suala hilo hata kidogo,” alisema
Wambura, naye kama alivyofanya Kimola akakata simu.
Kauli ya CHADEMA
Lakini wakati Kimola akikataa kusema chochote, Katibu Mkuu wa CHADEMA,
Dk. Willibrod Slaa, alisema kuwa alizungumza kwa njia ya simu na Kimola
kuhusiana na kitendo cha polisi kuvamia nyumbani kwa kiongozi huyo wa
juu wa kisiasa, na kudai kupewa majibu ya kushangaza.
Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Manzese, Wilaya
ya Kinondoni, Dk. Slaa alisema Kimola alijitetea akidai kwanza kukana
kufika nyumbani kwa Mbowe usiku wa manane. Pili, alisema kuwa hawakwenda
kumkamata Mbowe, isipokuwa kufanya naye mazungumzo na kisha
wangemwacha.
Slaa alisema kitendo hicho kimewashitua na ni cha kinyama na
kilichokiuka sheria za nchi na haki za binadamu. Aliongeza kwamba, daima
wamekuwa wakilishutumu Jeshi la Polisi kwa kutumika vibaya kukandamiza
wapinzani, lakini mara zote CHADEMA kimepuuzwa na sasa jeshi hilo
limeamua kuvamia makazi ya viongozi wa kisiasa kwa madhumuni
yasiyoeleweka.
Alisema haijulikani nini kingetokea ikiwa Mbowe angekuwa ndani, ikiwa
walinzi wangeamua kugoma kumwachia kiongozi wao. “Tuna hofu kubwa na
usalama wetu, maana pale wangeweza kufanya lolote, hata kumuua na kisha
kutoa matamshi kuwa walikuwa wanajibishana kwa risasi, kama ambavyo
imekuwa jadi ya askari polisi kutoa taarifa za uongo na upotoshaji
wanapoua watu,” alisema Slaa.
Alisema ikiwa polisi walikuwa na shida ya kweli, wangemwita kwa njia
sahihi na si kumvamia na kuingilia uhuru wake na wa familia yake kama
wanakamata gaidi ama jambazi hatari.
Dk. Slaa alisema Mbowe anayo ofisi inayojulikana, na kama kweli hakukuwa
na jambo baya lililopangwa na polisi hao wasingeweza kufanya uhuni kama
walioufanya.
“Kama wanaweza kuvamia nyumbani kwa kiongozi mkubwa kama Mbowe wakiwa na
silaha nzito, itakuwaje kwa viongozi wa kawaida na raia?” alihoji Slaa.
Kutokana na tukio hilo la kuogofya, CHADEMA imemtaka Rais Jakaya Kikwete
kuwaeleza Watanzania maana ya matukio haya ambayo yamedhamiria kuleta
vurugu kubwa nchini. Kadhalika, wamemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi
nchini, Said Mwema, kuueleza umma kile kilichokusudiwa na askari wake
kuvamia nyumbani kwa Mbowe mithiri ya jambazi.
Itakumbukwa pia kuwa hivi karibuni askari polisi wa Mkoa wa Arusha
walivamia nyumbani kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, wakiwa na
silaha nzito na mbwa, na kumkamata, kisha kumtupa rumande kwa siku
nzima.
Chanzo: Tanzania Daima
Post a Comment