RIWAYA: ROHO MKONONI
MTUNZI: George Iron mosenya
SIMU: 0655 727325
SEHEMU YA KUMI NA TANO
Hali aliyoikuta kwa Fonga ilimfanya afikirie upya juu ya Isaya!!
Akafikiria kumwendea bwana huyo ili amlilie katika shida yake, nafsi ilimwingia baridi sana kwa jaribio alilotaka kulifanya lakini angefanya nini iwapo mambo yanamuwia magumu kiasi hicho!!
Akaishika simu yake aweze kumpigia Isaya!!
Alisita mara kadhaa, akaghairi na kuamua tena zaidi ya mara tatu. Kisha akabofya na kuanza kusikiliza upande wa pili.
Simu ikaita lakini haikupokelewa!!
Alipojaribu kupiga tena mara simu yake ikaanza kuita akajikuta anapokea upesi akidhani ni Isaya.
“Mambo bro Isaya!!” alisabahi..
“Kituo cha polisi Magomeni Usalama….Joyce Keto. Unahitaji kituoni haraka iwezekanavyo!! Fika upesi bila kukosa, Asante. Ukifika mapokezi utakuta maelezo.”
Simu ikakatwa!!
Ebwana eee!! Joyce alitamani kukimbia, akatamani apae juu na apotee kabisa. Miguu ilikuwa inatetemeka kupita kawaida, mara mkoba mdogo aliokuwanao ukaanguka chini. Akahaha huku na kule katika kuuokota mara pikipiki zikapiga honi.
Hofu hii ilikuwa kubwa zaidi, yaani anaitwa polisi? Kwa jinsi alivyokuwa anayaogopa mambo ya polisi leo hii anaitwa polisi haraka iwezekanavyo!! Weeee!
MSHIKEMSHIKE!!!
Joyce baada ya kutuliza akili kwa muda akaamua kuondoka muda huo huo kuelekea kituo cha polisi Magomeni.
Njia nzima alikuwa analikumbuka onyo alilopewa la kutowashirikisha polisi juu ya taarifa na masharti aliyopewa, kwani kwa kufanya hivyo angeupoteza uhai wa Betty na yeye pia kujiweka katika mashaka ya hali ya juu.
Joyce akitokea maeneo ya chuo kikuu, aliwasili Ubungo baada ya robo saa kisha akachukua basi lililompelekahadi Magomeni Usalama.
Ndani ya dakika ishirini alikuwa akitazamana na kituo cha polisi. Kwa mara ya kwanza jijini Dar es salaam.
Mawazo yake kila alivyotazama kituo cha polisi yalikuwa juu ya kufungwa jela, alivyofikiri kuhusu hili akaanza kutetemeka miguu na mikono huku moyoni akifanya majuto asijue anajutia nini.
Macho ya askari wa kike yakatazamana naye mbele ya mzunguko wa mapokezi.
“Nini shida!” aliulizwa
Akajieleza juu ya kupokea simu ya kuhitajika kituoni pale. Alipojieleza zaidi na zaidi akaombwa ile namba ambayo ilimpigia. Wakati anataka kuitoa ile namba mara akaganda kama sanamu la kuchongwa.
Macho yake yalikuwa yanatazamana na Isaya, alikuwa pamoja na polisi aliyevaa sare zake rasmi.
Isaya alipomuona Joyce akanyoosha kidole kama anamwonyesha kitu yule afande. Hapa Joyce alitamani kukimbia lakini miguu ikawa mizito!!
Yule askari akamkaribia Joyce na kumuuliza iwapo ni yeye aliyepokea ile simu, Joyce akakubali kuwa ni yeye. Akashikwa mkono na kuongozwa kuelekea mahali.
Wakakifikia chumba fulani hivi, huko yakaendelea mahojiano juu ya wapi asili ya Betty na ni nani yake, na kuhusu namna alivyotekwa iwapo kuna taarifa yoyote anaweza kuwanayo.
“Joyce, inavyoonekana kuna dalili kuwa unajualolote kuhusiana na jambo hili, maana kwa maelezo ya Isaya ni kwamba mlikuwanaye karibu lakini ghaflaakamvisha pete Betty ambaye n I rafiki yako, hivyo wivu wa kimapenzi ukakusababisha uchukue uamuzi wa kumteka Betty na kumfanya lolote ujualo. Na baada ya muda mrefu kupita leo Isaya akiwa chumba cha mahojiano ulimpigia simu, bila shaka ulitaka kumweleza kuwa Betty ametoweka wewe uchukue nafasi binti” alijieleza yule askari huku akimkazia macho Joyce.
Joyce ambaye hakuna hata dakikamoja aliyojaribu kuizoea hali yam le ndani alifanya jitihada za kujitetea lakini kwa sababu ilikuwa mara yake ya kwanza kuhusisishwa katika kesi ya aina hii alijikuta akijiumauma tu!
“Naapa afande, Betty ni rafiki yangu sana mimi, hakuna ubaya kati yangu mimi na yeye. Sijawahi kufikiri na sikuwahi kumfanyia hivyo!! Naapa kabisa afande.” Alijibu huku akitetemeka.
“Lakini umewahi kuwa na wivu juu yake alipovishwa pete na Isaya.”
“Hapana sijawahi afande, sijawahi hata siku moja.”
“Mbona hukuhudhuria sherehe yake kama kweli hauna wivu, tena wivu mkubwa?” aliulizwa swali ambalo lilimchanganya sana. Alikosa cha kujibu akaanza kujiuma uma kucha zake.
“Na inavyoonyesha wakati sherehe zikiendelea wewe hapo na ndugu zako mlikuwa katika mpango kabambe wa kumteka Betty na Isaya, mbinu yenu chafu ikatibuliwa ndipo mkajipanga tena. Ndo maana haukuwa katika sherehe wewe Joy. Unaona sasa ulivyokuwa muongo?” askari mpelelezi wa ile kesi akazidi kumbana maswali yenye ushahidi Joyce.
Hapa sasa Joy akaona amekamatika, kweli hakuhudhuria sherehe na ni kweli muda ule aliutumia kufanya mtego wa kumzuia Isaya asifanye mapenzi na Betty ilimradi tu asiukwae Ukimwi.
Mambo mengi kwa pamoja yakakizingira kichwa cha Joy. Akatamani sana kusema juu ya tukio la usiku ule, lakini bilakusema kuwa Betty ni muathirika basi hataaminika na atajiweka katika kitanzi mwenyewe, akatamani pia kusema juu ya ujumbe alioletewa usiku katika bahasha ya kaki, lakini akahofia kuwa Betty atauawa na yeye kujikuta matatani.
Mkanganyiko huu wa aina yake ukamweka katika fumbo. Akakosa cha kujibu, jasho likaanza kumtoka.
“Mtoto mzuri kama wewe unajihusisha katika utekaji nyara, kwani wanaume mbona wapo wengi tu akina sisi hapa hatujaoa mbona umng’ang’anie huyo Isaya. Tatizo lenu watoto wa chuo mnapagawa sana kusikia mtoto wa mbunge…haya nd’o hautoki tena hapa.” Alisema kwa kebehi yule askari.
“Jamani afande mimi sijahusika na chochote, siwezi kumfanyia hivyo swahiba wangu siwezi mimi hata yeye akiletwa hapa sekunde hii hapa atausema ukweli lakini mimi sijui lolote afande, jamani afande mimi bado mwanafunzi nionee huruma mimi nakuomba.” Joyce alisihi, safari hii huku akibubujikwa na machozi. Afande yule hakujali, badala yake akachukua karatasi na kalamu.
“Haya binti nyamaza, huu ni wakati wa kutoa maelezo yaliyonyooka sasa kuhusiana na utekwaji nyara wa rafiki yako.” Afande alimsihi, kisha akaanza kumuuliza maswali ya kawaida tofauti na yale ya awali ambayo yalikuwa maalum kwa ajili ya kumtetemesha. Na hakika alitetemeka kweli!!
Baada ya mahojiano Joyce pasi na kutarajia alishangaa akiingizwa katika karandinga ya polisi.
Alitakiwa kuongoza njia kwenda mahali alipokuwa anaishi ili aweze kupekuliwa iwapo kuna ushahidi wowote wa kumuweka matatani.
Moyo wa Joyce ukapasuka kwa hofu kuu! Akaduwaa kama vile anaangalia filamu ya kutisha ambapo anangoja tukio moja limalizike kisha lifuate jingine.
Alikuwa amekumbuka juu ya ujumbe aliotumiwa katika bahasha ya kaki. Alitamani kumwagiza mtu yeyote yule akautoe kabla hawajafika pale lakini bahati mbaya simu yake ilikuwa imekamatwa na kuzimwa tayari ili asije kuharibu upelelezi wa kesi ile.
Karandinga lilifunga breki kwa fujo katika maeneo ya Ubungo Kibangu ambapo ndipo aliishi Joyce na Betty katika nyumba ya chumba kimoja na sebule, huku sebule ikigeuzwa kuwa jiko.
Askari takribani wanne walishuka kisha akatelemka Joyce, mrundikano wa watu kundi kwa kundi ukaanza kufuatilia tukio hili huku wengine wakijifanya wanajua tayari kinachoendelea.
Joyce alikuwa katika fedheha kubwa ambayo hakuwahi kuitegemea hata siku moja, hakikalilikuwa jaribu ambalo alihisi lilikosea njia na kumkumba yeye.
Mapenzi haya!! Alijisemea huku akimfikiria Isaya. Laiti kama asingekuwa yeye basi asingekuwa hapo alipo.
Akatamani kumchukia lakini akakosa sababu ya kumchukia maana alimpenda mtu aisyejua kama anapendwa kwa dhati!!
Chumba kikafunguliwa,baada ya mwenyekiti wa mtaa kutoa Baraka za ukaguzi huo. Joyce akaingia pamoja nao ndani iwapo watahitaji upekuzi zaidi aweze kuwasaidia.
Hii haikuwa kesi ya kawaida!! Polisi walikuwa wamejikita vilivyo, wakapekua kila kona, lakini waliishia kupata picha za Joyce na Betty wakiwa katika furaha. Mara maua na kadi walizotumiana kama ishara ya upendo.
Simu ya Joyce nayo ikapekuliwa lakini hapakuwa na ujumbe wowote hatarishi.
Hatimaye wakafikia madaftari ya Joyce, daftari moja bada ya jingine. Sasa walikuwa wamelifikia daftari lililokuwa na ile bahasha, lilivyonyanyuliwa tu bahasha ikadondoka chini, askari akainamana kuikota. Joyce alitamani kufanya muujiza bahasha ile isifunguliwe lakini haikuwa hivyo bahasha iukafunguliwa.
Karatasi ikatolewa.
Nimekwisha!! alijisemea Joyce huku akiinama chini kungojea aibu ya mwaka ya kupigwa pingu na kisha kubambikiziwa kesi ya utekaji nyara.
Karatasi ile ilikuwa imeandikwa maneno machache tofauti na awali. Polisi akasonya na kuitupa mbali, Joyce bado alikuwa ameinama akingoja maswali lakini hapakuwa na swali lolote.
Polisi wakakiri kuwa hapakuwa na lolote la kuwasaidia kutoka kwa Joyce.
“Tukikuhitaji wakati wowote tutakuita kituoni na ufike mara moja kwa wakati.” Askri mmoja alitoa amri hiyo, kisha akaongozanana wenzake wakatoka nje na kuliendea karandinga.
Joyce akaketi huku akiwa haamini kabisa kama alikuwa ameachwa huru siku hiyo. Machozi yalikuwa yanamtoka na jasho jingi. Alikuwa akijiuliza ina maana hawakuelewa ujumbe katika ile bahasha, hapo akainuka ghafla na kuisaka tena ile bahasha.
Huku akakutana na ile bahasha, ujumbe ukiwa pembeni lakini safari hii ulikuwa tofauti kabisa na ule wa awali.
“MAMBO SHOSTI” ujumbe uliandikwa hivyo kwa herufi kubwa!!
Joyce akachoka!!
Majirani walikuwa mlangoni wakitaka kumuuliza nini kimetokea, akasimama kama anayetaka kuwasikiliza, akaufikia mlango akaufunga kisha akaingia chumbani kwake akajirusha kitandani.
Tayari ilikuwa saa kumina moja jioni!!
*****
FONGA alishtushwa sana na habari za Joyce kuwa kituo cha polisi. Habari hizi alizipata mapema sana kupitia kwa Isaya ambaye alikuwa amemaliza kuhojiwa.
Kwa uzoefu wake kidogo Fonga alitambua kuwa Joyce atatetemeshwa sana na kutishwa sana ili aseme hata asilolijua.
Huruma ikamwingia na akawa kama anayemuona Joyce jinsi anavyohangaishwa na maswali ya polisi watukutu.
Fonga akaamua kutumia nafasi hii!!
Aliiona ya kipekee sana.
Majira ya saa tatu usiku alikuwa katika nyumba ya kulala wageni maeneo ya Sinza, alikuwa ametulia tuli akijitahidi kuondoa uoga aliokuwanao.
Baada ya nusu saa mlango ukagongwa.
Akaufungua, Joyce akaingia ndani!!
Akaketi katika mojawapo ya viti vilivyokuwa katika nyumba ile.
Fonga alikuwa mwingi wa mawazo na aliyetazamika kama mtu mwenye uchungu sana. Macho yake yalipepesa huku na kule kabla hayajatua katika uso wa Joyce.
Akainama chini na kuanza kutiririka maneno mfululizo ambayo yalikuwa mageni sana kwa Joyce.
“Unajua Kidoti, huwa inafikia mahali kama mwanadamu inabidi useme tu inapobidi. Ni muda mrefu sana mimi nimefahamiana na wewe japo sio kwa ukaribu kama huu wa sasa. Joyce nimeguswa sana na tatizo lako, na nimesikitika zaidi na kufadhaika niliposikia umepelekwa polisi na kisha kuondoka na karandinga, mrembo kama wewe hakika haustahili hata kidogo. Ni kweli mimi ni maskini lakini hii haijalishi linapotokea tatizo kwa mtu ambaye unampenda. Nipo radhi kufanya jambo lolote jema hata kama linanigharimu kwa mtu nimpendaye, Joyce Kidoti mimi sina elimu labda nd’o maana nikajikuta nikishindwa kuwa imara na kukabiliana nawe wakati ukiwania mashindano ya urembo hapo chuoni, lakini sasa najihisi kama nakosa kabisa amani nikiendelea kujinyima haki hiyo. Huenda Mungu ametuunganisha tena kwa namna ya kipekee ili niweze kujieleza kuwa nakupenda sana. Na ninakuhitaji hakika, ulipokuwa jirani na Isaya sio siri nilikuwa naumia sana. Niliumia sana kwa sababu moja tu Isaya hana mapenzi ya kweli. Na hapo alipo anafanya kuwachezea tu wasichana na kuwaacha, wewe hukustahili kuchezewa hata kidogo, mimi ni jasiri na huwa sina mpango wowote na watoto wa kike zaidi ya kujikita katika kazi zangu uzijuazo lakini kwako Joy naweza kusema nimeshindwa kabisa.
Sitaki niseme mengi katika hili tatizo huenda unaweza usinielewe kutokana na wakati tunaopitia kwa sasa ambapo Betty ametoweka. Basi nakuomba tu kwa muda huu utambue kuwa ile milioni tatu, imepatikana na kama kweli hao watekaji wana shida hiyo tu basi Betty watamuacha huru!! Haijalishi imenigharimu ama itanigharimu katika siku za usoni lakini nimeyafanya haya kwa msichana ambaye ninampenda kwa dhati” hapa akamaliza akamtazama Joy machoni.
Akakutana na macho yanayong’ara kwa furaha kuu, Fonga akatambua kuwa amezipanga karata zake vizuri kabisa na sasa alitakiwa kufunga goli na mchezo uishie hapo.
Joy akamrukia Fonga na kumkumbatia, alimkukumbatia kwa mambo mawili makuu kwa wakati huo, kwanza alikuwa ameongea maneno ambayo Joy aliwahi kuyasema wakati akijitoa kwa marehemu mwalimu Japhary na kisha kuukwaa Ukimwi, ‘Nipo tayari kufanya lolote kwa mtu ninayempenda’……pili alimkumbatia kwa sababu alikuwa kama malaika wa ukombozi.
Hapa angeweza kumwonyesha Betty ni jinsi gani anamjali kwa kumwokoa kutoka katika mikono ya watu wabaya.
Furaha ikizidi sana hupunguza uwezo wa kufikiri!! Uchungu ukizidi vilevile huleta tatizo hilo hilo.
Joyce akalala na Fonga hadi asubuhi.
Alipotoka pale ndani alikuwa na milioni tatu kibindoni huku nyuma akimwacha Fonga akijiuliza ile ladha ya penzi alilolingoja kwa muda mrefu hatimaye ameipata.
Watu wawili walikuwa wanaota kwa pamoja lakini ndoto mbili tofauti.
Joyce akiota kumuokoa Joy kwa sababu pesa aliyoipata akiongezea na ile ya kwenye akaunti ya Betty basi jumla inafika milioni sita!!
Fonga akaota ndoto ndogo tu lakini nzito, akaamua kuweka tena kichwani suala la kuoa. Kumuoa Kidoti.
Baada ya muda mrefu wa kuachana na mapenzi baada ya tukio la mwenye pesa mmoja kumnyang’anya mpenzi wake aliyempenda hadharani kisha kumweka rumande kwa kesi asiyoijua, kesi iliyomfanya atumikie kifungo cha miezi tisa jela.
Kitendo ambacho kilimfadhaisha Fonga na kukoma kabisa kujihusisha na mapenzi, sasa alikuwa amefika tena kwa Joyce Kidoti. Na kisha akatangaza ndoa katika nafsi yake.
Hakika ilikuwa ndoto ndogo, lakini nzito sana!! Ilikuwa nzito kwa sababu hakujua kama kuna mambo mengine mazito yalikuwa yakiendelea chini ya pazia!!
***FONGA ametumia msaada wake kulinunua penzi la JOYCE KIDOTI, JE! Ni usiku huo pekee ama penzi hilo litaendelea??
***JOY atafanikiwa kumkomboa BETTY? Na ni nani huyo ambaye amemteka na kwa nini?
***UJUMBE ndani ya bahasha hauonekani…..KULIKONI
LIKES, SHARES, bila kusahau kuweka MAONI YAKO……
ITAENDELEA…….
Post a Comment