Na Bryceson Mathias
CHAMA
cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kupitia kwa mwenyekiti wake,
Freeman Mbowe, hivi karibuni kimewahakikishia watanzania kuwa kitafanya
kila linalowezekana kurejesha mali zote za Taifa zilizouzwa kinyemela
kwa mikataba mibovu.
Ni rai yangu, Kama wenye mapenzi mema na nchi hii wanaona viongozi na CHADEMA
inafanya kazi ya kumuondoa Kaburu Mweusi nchini, ili watoto wetu,
vijukuu, vitukuu waje kuwa na rasilimali endelevu, basi wapongezwe na
kuungwa mkono.
Mbowe alidai kuwa, Mwalimu
Julius Nyerere na viongozi wenzake walipigana kuwaondoa Makaburu weupe
na hivyo CHADEMA nao sasa wanafanya kazi ngumu ya kumuondoa Kaburu weusi
ili watoto wanaokuja waweze kufaidi rasilimali zilizopo nchini.
Mbowe alisema hayo akitembelea
Kata za jimbo la Hai, akiwa na wabunge zaidi ya 11 wa Chadema toka
majimbo mbalimbali na kuweka wazi kuwa, ili kufanikiwa vita hivyo,
watahakikisha Katiba mpya inaweka wazi ulazima wa kuanika mikataba yote
ya kiuchumi iliyoingiwa na serikali.
Kauli
ya Mbowe, imepokewa kama kufutwa machozi ya wananchi wengi wanaopenda
haki zao zilizopiganiwa na Nyerere zirejeshwe, wakifananisha na Wana
Ndoa waliofiwa watoto, hivyo mke kuwa na Ujauzito wenye Uhakikika wa
mtoto atakayeishi ni furaha kwao.
Mwenyekiti
huyo ambaye ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, alitolea
mfano wa shamba alilopewa mwekezaji anayezalisha sukari la TPC, akisema
hakuna anayejua ni kiasi gani cha fedha kinachoingia serikalini wala
kilichoandikwa kwenye mkataba huo.
Mbowe
alidai Mwekezaji huyo alipatiwa eneo kubwa la shamba pamoja na maji,
huku wananchi wa maeneo hayo wakitaabika kwa uhaba wa ardhi.
“Hatuwezi
kuangalia mali yetu ikienda na wananchi wanataabika. Tukipata katiba
mpya lazima mali zote zilizochukuliwa na wawekezaji mikataba irudiwe na
iwekwe hadharani.
“Mkoa
wa Kilimanjaro ulikuwa na viwanda vingi vilivyokuwa vinafanya kazi
vizuri, lakini wamepewa wawekezaji ambao kwa sasa hakuna anayejua
mkataba walioingia na serikali na viwanda vingi Moshi vimekufa,”
alisema.Mbowe.
Mbowe
aliwakumbusha watanzania Juhudi za Mwalimu Nyerere na kusema, Nyerere
na viongozi wenzake walipigana kuwaondoa Makaburu weupe na hivyo kuwa
CHADEMA sasa nayo inafanya kazi ngumu kumuondoa Kaburu mweusi ili watoto
wanaokuja waweze kufaidi rasilimali zilizopo nchini.
“Hivyo
wananchi wangu wa Hai mkiniona niko kimya natafuta ukombozi wa nchi
hii, baada ya kutoka hapa nitafanya mikutano nchi nzima, lakini
ninawaahidi tukimaliza Bunge la Katiba lazima nije kushinda na nyie
kusikiliza zaidi kero zenu,” alisema Mbowe.
Angalizo
la Mbowe na Chama chake cha Chadema, litufumbuwe macho watanzania, kwa
sababu ni ukweli usiopingika kwamba, viwanda vyote vya sukari nchi
kikiwemo Mtibwa, Kilombero na Kagera, sasa hivi vimekuwa havina faida
kwa wananchi na wafanyakazi wa maeneo husika.
Yapo
maeneo mengi ya uwekezaji, ambayo yana tatizo la mikataba mibovu
inayodaiwa ni ya siri, ambayo licha wananchi kukosa maeneo ya kulima,
lakini wanakosa hata haki za kupata maendeleo yao wenyewe kuhusiana na
kuwepo kwa uwekezaji huo.
Pengine
kwa tamko la CHADEMA na viongozi wake, limegusa mioyo ya watanzania,
ambao kwa hapa nchini katika uwekezaji, wamekuwa watumwa wa wawekezaji
katika nchi yao wenyewe, huku wakifanyizwa kazi utumwa kwa kipato duni,
ndani ya rasilimali walizoziasisi wenyewe, huku faida ya kutisha
ikisombwa na kusafirishwa kwenda nje.
nyeregete@yahoo.co.uk 0715933308
Post a Comment