
MWENYEKITI
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema
kuwa kitapigana hadi tone la mwisho la damu kurejesha mali zote za
wananchi zilizouzwa kinyemela.
Mbowe akiwa
katika ziara yake kutembelea kata zote za jimbo la Hai, akiambatana na
wabunge zaidi ya 11 wa chama hicho kutoka majimbo mbalimbali, alisema
ili kufanikiwa katika vita hivyo, watahakikisha katiba mpya inaweka wazi
ulazima wa kuanika mikataba yote ya kiuchumi iliyoingiwa na serikali.
Mwenyekiti
huyo ambaye ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Upinzani Bungeni alitolea
mfano shamba alilopewa mwekezaji anayezalisha sukari la TPC, akisema
hakuna anayejua ni kiasi gani cha fedha kinachoingia serikalini wala
kilichoandikwa kwenye mkataba huo, ambao umempatia mwekezaji huyo eneo
kubwa la shamba pamoja na maji huku wananchi wakitaabika kwa uhaba wa
ardhi.
“Hatuwezi
kuangalia mali yetu ikienda na wananchi wanataabika tukipata katiba mpya
lazima mali zote zilizochukuliwa na wawekezaji mikataba irudiwe na
iweke hadharani.
“Mkoa wa
Kilimanjaro ulikuwa na viwanda vingi vilivyokuwa vinafanya kazi vizuri,
lakini wamepewa wawekezaji kwa sasa hakuna anayejua mkataba walioingia
na serikali na viwanda vingi Moshi vimekufa,” alisema.
Alisema
Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wenzake walipigana kuwaondoa Makaburu
weupe na hivyo CHADEMA nao wanafanya kazi ngumu kumuondoa Kaburu weusi
ili watoto wanaokuja waweze kufaidi rasilimali zilizopo nchini.
“Hivyo
wananchi wangu wa Hai mkuniona niko kimya natafuta ukombozi wa nchi hii
baada ya kutoka hapa nitafanya mikutano nchi nzima, lakini ninawaahidi
tukimaliza Bunge la Katiba lazima nije kushinda na nyie kusikiliza zaidi
kero zanu,” alisema.
Katika hatua
nyingine, Mbowe alisema katiba ya sasa imetumiwa vibaya na viongozi
walioko madarakani kuwalimbikizia wananchi kesi pamoja na kutowachukulia
hatua viongozi wanaoiba rasilimali za umma.
Alisema
wafungwa wengi magerezani ni wale wezi wadogo wadogo huku viongozi
walioiba mabilioni wakiendelea kufurahia maisha uraiani.
Kwa upande
wake Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema, alisema kuwa kama kuna
kiongozi wa upinzani ambaye akifa CCM watafanya sherehe ni pamoja na
Mbunge wa Hai Freeman Mbowe.
Alisema Mbowe amekuwa akifanya kazi ngumu na kuleta mafanikio makubwa yakiwemo ya kuwa na wabunge wengi vijana ikiwemo yeye.
Miongoni mwa
wabunge walio kwenye ziara hiyo ni pamoja na Ezeckiel Wenje, Peter
Msigwa, Joshua Nasari, Lucy Owenye, Grace Kiwelu, Joseph Selasini,
pamoja na madiwani wa CHADEMA kutoka Moshi, manispaa na Hai.
Wakati huo
huo CHADEMA imepinga kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
Jaji Joseph Warioba kwamba hawatapokea maoni yatayopelekwa kwa njia ya
Chopa.
Akizungumza
na wananchi wa kata ya Mabibo, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa
CHADEMA, John Mnyika, alisema chama chao kitatumia kila njia kuwafikia
Watanzania na kuwaelewesha rasimu ya Katiba mpya na msimamo wao.
Mnyika
alisema kila chama cha siasa sasa kinawafikia wananchi wake,
kuwaelewesha na kupata maoni yao kuhusu kuandikwa kwa Katiba mpya, hivyo
haoni kama ni kosa kwao.
Alisema
CHADEMA imeshaanza ziara na kueleza kwamba mwenyekiti wao Freeman Mbowe
akishirikiana na Tundu Lissu wako mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kati huku
Dk. Willibrod Slaa na Mabere Marando wakitoa elimu mikoa ya kusini na
kaskazini.
Mnyika
ambaye pia ni mbunge wa Ubungo alisema wakiwa katika mchakato huo, Jaji
Warioba akishirikiana na wenzake ametaka kupindisha sheria ili wampe
madaraka Rais Jakaya Kikwete kufanya uteuzi wa wajumbe wengine zaidi ya
100 kuingia katika Bunge la Katiba jambo ambalo CHADEMA haikubaliani
nalo.
Alisema
kutokana na hilo pamoja na mengine ambayo yanaweza kuchomekwa,
wamemwagiza Lissu kukatiza ziara yake ili ashirikiane na wanasheria
wengine kukabilina na jambo hilo.
“Baada ya
kutokea dharura hiyo, nawaomba wananchi wangu nikachukue nafasi ya Lissu
… nitaondoka Jumapili, nitakaa huko kwa siku 12 ili niweze kusaidiana
na mwenyekiti wangu kupata maoni ya Watanzania,” alisema.
Mnyika
alisema pamoja na hilo, CHADEMA imetengeneza kitabu kinachozungumzia
msimamo wao kuhusu muundo wa Katiba mpya ambacho wameanza kukisambanza
kwa wananchi kwa gharama ya sh 300.
Kiongozi
huyo aliwataka Watanzania na Wanachadema ambao wanapenda mabadiliko
kukinunua kwa ajili ya kupata uelewa kuhusu rasimu hiyo na nini
wanapaswa kuchangia.
Wakati
huohuo, Mnyika aliwataka wananchi na Wanachadema kumchagua mgombea
uenyekiti wa mtaa wa Sahara Relini Mayunga Kadwisha katika uchaguzi
unaotarajiwa kufanyika kesho Agosti 11, mwaka huu.
Akimnadi mgombea huyo, Mnyika alisema nchi hii inapaswa kuongozwa na mtu anayependa mabadiliko hasa CHADEMA na si vinginevyo.
‘Wananchi wa
Sahara na Reline, mchagueni Kadwisha siku ya Jumapili kwa ajili ya
maendeleo ya mtaa wenu … hakuna mgombea mwingine, na hapa nafikiri kama
CHADEMA isingemweka mgombea huyu likawepo jiwe, mngechagua jiwe kuliko
CCM,” alisema Mnyika.
Post a Comment