Dar es Salaam. Wakati matukio ya baadhi
ya vigogo na wasanii maarufu
wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara
ya dawa za kulenya hayajapoa, imebainika
kuwa mtambo maalumu wa kuchanganya
na kuziongezea thamani dawa hizo upo
hapa nchini.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili zimeeleza
kuwa mtambo huo ambao awali ulikuwa
unapatikana Mombasa, Kenya, pekee,
unatumika kuchanganya dawa za kulevya
na kemikali nyingine ambapo nusu kilo ya
heroine huongezwa hadi kufikia kilo mbili.
Uchunguzi unaonyesha kuwa kuwa mtambo
huo ulioingizwa mwaka huu na kigogo
mmoja wa dawa hizo, upo katika nyumba
moja iliyopo eneo la Mbezi Beach.
Mmoja wa watumiaji wa dawa hizo ambaye
hakutaka kutajwa gazetini kwa kuhofia
usalama wake, alisema mtambo huo
umerahisisha upatikanaji wa heroine
nchini maarufu ‘white sugar’ kama
inavyojulikana mitaani.
“Zamani ‘white sugar’ ikitoka shamba (nchi
inakotengenezwa yaani Pakistan na nchi
nyingine) ilikuwa inapelekwa Mombasa,
Kenya, ambako kuna mtambo wa
kuchanganya na dawa nyingine ili
iongezeke wingi wake, lakini kazi hiyo
inafanyika hapa hapa nchini kwa sasa,”
alisema.
Alipoulizwa kuhusu uwepo wa mtambo huo
hapa nchini, Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia
Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema
kuwa kuna taarifa alizonazo ambazo bado
anazifanyia kazi.
“Hata kama nikiwa nazo nazifanyia kazi,
za kwangu mimi nazifanyia kazi na hata za
kwako nazifanyia kazi,” alisema Nzowa.
Hata hivyo, Nzowa akizungumza katika
kipindi cha Malumbano ya Hoja
kilichorushwa na Televisheni ya ITV juzi,
alisema kuwa katika siku za hivi karibuni
wafanyabiashara wa heroine wamekuwa
wakiingiza nchini malighafi za dawa hizo,
tofauti na awali ambapo walikuwa
wakiingiza dawa hizo zikiwa tayari kwa
matumizi.
Akitoa mfano alisema kuna raia wa kigeni
alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam,
akiwa na malighafi hizo zilizokuwa
zikifanana na sukari na kwamba Mamlaka
ya Chakula na Dawa (TFDA) na Mkemia
Mkuu wa Serikali, ndiyo waliobaini kuwa
haikuwa sukari kama ilivyodhaniwa.
Alisema kutokana na uhaba wa dawa hizo
bei ya kete imepanda ambapo hivi sasa
hakuna kete ya gramu 0.11 inayouzwa
chini ya Sh 3,000.
Hii ni mara ya pili kubainika kuwepo kwa
mtambo wa kutengenezea dawa za kulevya
nchini. Miaka ya hivi karibuni jeshi la
polisi lilikamata mtambo wa kutengenezea
dawa za kulevya katika nyumba moja
iliyopo eneo la Mbezi Beach jijini Dar es
Salaam.
Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa
mbali ya kuwepo mtambo huo kuna
nyumba tano katika eneo la Tandika jijini
Dar es Salaam karibu na soko, ambazo
zinatumika kuuza dawa za kulevya huku
baadhi ya polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa
Temeke, wakiwalinda wauzaji wake kwa
kuwapa taarifa ya mipango inayopangwa
na jeshi la kuwatia mbaroni.Jf
Post a Comment