CHADEMA KUMSHITAKI BAROZI WA CHINA NCHINI.

Dar es Salaam na Mbeya.Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kitamshitaki Balozi wa China nchini, Lu Younqing Umoja wa Mataifa (UN) kwa kukiuka Mkataba wa Vienna (Vienna Convention) wa mwaka 1964 ambao unaeleza uhusiano wa kibalozi kati ya nchi na nchi.
Aidha, kimesema kitaiandikia barua Serikali ya China ili kutaka ufafanuzi kama imemtuma Balozi wake kufanya kazi ya uenezi siasa kwenye vyama.
Tukio la Balozi huyo kuhudhuria mkutano wa hadhara wa CCM lilitokea Septemba tisa mwaka huu kwenye mkutano wa chama hicho uliofanyika Wilaya ya Kishapu Shinyanga, ambapo Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana alimtambushisha balozi huyo huku akiwa amevaa sare za chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri kivuli wa mambo ya nje ambaye pia ni Mbunge wa Nyamagana Jijini Mwanza, Ezekiel Wenje alisema Chadema wameamua kuchukua hatua hizo ili kukomesha vyama vya siasa kutumia mabalozi kama wawakilishi wa vyama vyao kwa kufanya uenezi kwenye mikutano ya siasa.
Wakati Wenje akisema hayo Katibu Mkuu Taifa wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema chama chake kinaangalia namna ya kumchukulia hatua za kumshtaki Balozi huyo akidai kuwa kitendo cha kushiriki siasa za CCM na kisha kuvalishwa kofia ya chama hicho ni kiunyume na taratibu za UN.
Kauli ya Dk Slaa aliitoa juzi jioni wakati akiwahutubia wakazi wa Jiji la Mbeya na vitongoji vyake kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Ruanda Nzovwe.
Kiongozi huyo yupo mkoani Mbeya akiwa ameambata na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ akifanya mikutano maeneo mbalimbali lengo likiwa kuwaeleza wananchi wa Mbeya kuhusiana na kitendo kilichomtokea Sugu na wabunge wengine bungeni hivi karibuni.
Kwa mujibu wa Dk Slaa, balozi huyo alikiuka sheria na taratibu za Umoja wa Mataifa kwa kitendo chake ambapo alionekana kupanda kwenye jukwaa la mkutano wa CCM na kuvalishwa kofia ya chama hicho.
Kwa upande wake, Wenje alidai kuwa kwa mujibu wa mkataba wa Vienna Convention wa mwaka 1964 ambao unaeleza mahusiano ya kibalozi unakataza mabalozi kujingiza kwenye mambo ya ndani ya nchi ikiwa pamoja na kushiriki kwenye siasa.
“Mkataba wa Vienna Convention wa mwaka 1964 Ibara ya 41 kifungu kidogo cha kwanza kinakataza mabalozi kujiingiza kwenye mambo ya ndani ya nchi ikiwa pamoja na kufanya siasa.” alisema Wenje na kuongeza;
“Kitendo alicho kifanya balozi wa China kufanya kazi ya uenezi wa chama kimevunja mkataba huo jambo ambalo hatuwezi kulivumilia hata kidogo,”alisema.
Alifafanua kuwa licha ya Ibara hiyo kukataza jambo hilo Ibara ya 3 ya mkataba huo inataja wazi kazi wanazotakiwa kufanya balozi pindi anapokwenda kuwakilisha nchi yake sehemu nyingine.”alisema.
Wenje alibainisha kwamba mwaka 2007 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alitoa tamko la kuwaonya mabalozi kuacha kujiingiza kwenye masuala ya siasa.

“Kumbukumbu zetu zinaonyesha kwamba Waziri Membe alishawahi kuonya mabalozi kuacha kujiingiza kwenye masuala ya kisiasa.Kitendo alichokifanya balozi wa China lazima tukishughulikie hatuwezi kukivumilia hata kidogo,”alisema.
Pia, Wenje alisema licha ya Membe kuonya jambo hilo mwaka 2011 alishawahi kuonya tena jambo hilo akiwa ndani ya Bunge jambo ambalo linasikitisha kuona kitendo hicho kinatokea hadharani
Naye Mkurugenzi wa masuala ya Bunge na Halmashauri wa Chadema, John Mrema alisema wataandika barua hizo kwa wakati ili kupewa ufafanuzi wa kitendo hicho.
Alisema kila hatua watakayopita wataambatanisha na ushahidi wao ili kuhakikisha hatua husika kwa balozi huyo zinachukuliwa.
“Tutaandika barua hizo kwa Serikali ya China, Serikali ya Tanzania pamoja na Umoja wa Mataifa (UN), kwani balozi wa nchi hiyo amevunja mkataba wa Vienna Convention na ni chanzo cha kuvunja mahusinao kati ya nchi hizi mbili,”alisema Mrema.
 -MWANANCHI

Post a Comment

Previous Post Next Post