Kocha wa timu ya soka ya Mtibwa Sugar, Mecky Mexime amekubali kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Bara uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na mtandao huu mara baada ya mchezo huo, Mexime ambaye ni
nahodha wa zamani wa Taifa Stars amesema, timu yake ilicheza vizuri
lakini uwezo ulioonyeshwa na Simba uliwafanya wastahili kupata ushindi.
Alisema kikosi chake kilijitahidi kadiri ya uwezo wake kuweza kupata
ushindi lakini makosa mawili waliyofanya yaliiwezesha Simba kupata mabao
mawili na kuibuka na ushindi.
“Nimekubali kwamba nimefungwa na Simba kihalali kabisa katika hali ya
kawaida ya kimchezo, wenzetu walitumia vyema nafasi walizopata na
kuweza kufunga mabao mawili yaliyowawezesha kupata ushindi.
“Timu yangu haikucheza vibaya japokuwa tumefungwa mabao mawili,
kilichotokea ni hali ya mchezo ambayo inaweza kuikuta timu yoyote iliyo
imara na kutokana na matokeo haya tunajipanga kuhakikisha tunafanya
vizuri katika mchezo unaofuata ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi
kwenye ligi,” alisema Mexime.
Kwa upande wake, Kocha wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema kikosi
chake kimecheza vizuri hadi kikaibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya
Mtibwa hali inayompa faraja ya kuwa na kikosi bora msimu huu.
“Siyo siri nawashukuru vijana wangu kwamba wamejituma ipasavyo na
kuweza kupata ushindi huu mnono dhidi ya timu hodari kama Mtibwa. Kila
idara ilihakikisha inafanya kazi vizuri japokuwa kulikuwa na makosa
madogo madogo ambayo natakiwa kuyarekebisha kabla ya mchezo mwingine,”
alisema Kibadeni.
Post a Comment