MAKAMBA AZIPIGA TAFU SHULE YA MSINGI KWEMBALAZI NA KWEULASI


Mbunge  wa  Jimbo  la  Bumbuli  January  Makamba  amekabidhi  msaada  wa  mabati  80 na fedha taslimu laki tano kwenye  shule  ya  msingi  Kwembalazi  na Kweulasi  kwa  ajili  ya  kusaidia  ujenzi  wa  madarasa  katika shule  hizo ambazo  ziko  pembezoni  mwa  jimbo  hilo .

Pia  Wajumbe   wa  Kamati   ya  maendeleo  ya  kata  ya  Milingano wameeleza kufurahishwa kwao na juhudi za Mbunge wa Jimbo hilo, January Makamba katika kuendeleza elimu,afya  na  kuleta maendeleo ya jumla ya jimbo hilo.

Akizungumza  kwa  niaba  ya  January  Diwani  wa  kata  ya  Milingano  Hoza Mandia  ambae pia  ni  Katibu  wa  mbunge huyo  alisema  lengo  la kutoa  msaada  huo  ni  kuunga  mkono  juhudi  mbalimbali  zinazofanywa  na  wananchi  hao.

Akieleza  furaha  hiyo  kwa  niaba  ya  wajumbe  hao  Mwenyekiti  wa  kijiji  hicho Amiri Kaniki alisema  juhudi hizo za Mbunge huyo zinatakiwa kuungwa mkono na wakazi wote wa jimbo hilo ili  kuweza  kuharakisha  maendeleo  ya  haraka  na  kukuza uchumi  wa  bumbuli.

Katika  kumuunga  mkono  Mbunge  huyo  ambaye  ni  Naibu  Waziri  Mawasiliano  Sayansi  na  Teknolojia January  Makamba , Calorine  Johnstone ambaye  asili yake  ni  wingereza  alichangia  katika  sekta  ya  afya  kwenye  vijiji  vya  milingano  na Yamba  pamoja  na kujenga  vyumba  2  vya  madarasa  shule  ya  msingi  kweulasi  vyenye  thaman  ya  shilingi  mil. 50.
 
Wakati  huo huo  wakazi  wa vijiji vya Kwempunda na Manga vilivyopo  pembezoni mwa jimbo la  bumbuli wamemuomba ,Mbunge wa jimbo hilo,Januari Makamba kuwajengea vituo vya afya katika vijiji hivyo ili kuondokana na vifo vinavyoepukika.
 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya Mbunge huyo hivi karibuni wananchi hao walisema changamoto kubwa inayowakabili ni kukosekana kwa vituo vya afya katika vijiji vyao hali ambayo inawalazimu kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
 
Mwananchi wa kijiji cha Kwempunda Khamisi Shekigenda alisema wanatembea umbali mrefu kutafuta huduma ya afya katika vijiji vya jirani swala ambalo wakati mwingine limekuwa likiwaathiri wakinamama wajawazito na watoto.
 
Mbunge wa jimbo hilo,Januari Makamba akijibu hoja za wananchi hao aliwaambia atashirikiana nao bega kwa bega kuhakikisha wanaipata huduma hiyo na kuondokana na vifo ambavyo vinaweza kuepukika katika vijiji vyao.
 
Aliwaambia watenge maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo na kuonyesha mchango wao ili hatimaye waweze kuondokana na tatizo la muda mrefu la ukosefu wa vituo hivyo.
 
"Ndugu zangu wananchi niko tayari kushirikiana nanyi, ninachowaomba kuanzia sasa muanze kutenga eneo ,mchimbe msingi pamoja na kusombelea mawe na mchanga,a hapo mtakapofikia mimi nitawasaidia,"alisema Makamba.

Post a Comment

Previous Post Next Post