
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitembelea maendeleo
ya uzalishaji wa umeme kupitia miundo mbinu iliyopo hivi sasa kwenye
kituo kikuu cha umeme Mtoni. Kulia
kwa Balozi ni Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Madini Mh.
Ramadhan Abdulla Shaaban na kushoto yake ni Kaimu Meneja Mkuu wa Zeco
Thabit Salum Khamis.

Kaimu
Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) Thabit Salum Khamis
akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif mfumo
mpya wa huduma za umeme unaotumika katika kituo kikuu cha Umeme
kilichopo Mtoni wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya huduma
za umeme Nchini.

Mhandisi wa Vituo vya Umeme katika shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) Mohd Juma Othman akimfafanulia Balozi
Seif mfumo wa ugawaji wa laini za umeme mkubwa kwenda katika vituo
vipya vilivyojengwa kwa lengo la kutoa huduma za uhakika za Umeme maeneo
tofauti Nchini.Picha na Hassan Issa-
---
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji Nishati
na Madini imeombwa kufikiria njia muwafaka ya kuyauza Majanareta
yaliyopo katika kituo kikuu cha kupokelea Umeme Mtoni ili kuwepusha
hasara endapo yataendelea kuwepo eneo hilo bila ya matumizi.
Majanareta
hayo 30 yalikuwa yakitoa huduma za umeme wa dharura katika kipindi
ambacho Zanzibar ilikuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa huduma ya
nishati ya umeme kutokana na kinanzio chake ilichokuwa ikikitumia wakati
huo kutokidhi mahitaji halisi ya huduma hiyo Nchini.
Mhandisi
wa Maganareta katika Kituo Kikuu cha Umeme Mtoni Yussuf Reja alitoa
ushauri huo wakati wa ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi kuangalia maendeleo ya uzalishaji wa huduma ya umeme
Nchini kupitia miundo mbinu iliyopo katika kituo hicho.
Mhandisi
Yussuf Reja alimueleza Balozi Seif kwamba Majanareta hayo yako katika
kiwango bora lakini tatizo kubwa liliopo ni huduma ya mafuta ambayo ni
maalum { IDO } na yana hitaji gharama kubwa za uendeshaji.
Alisema
Shirika la Umeme lilikuwa likipata hasara ya zaidi ya shilingi Milioni
16,000,000/- kwa saa wakati maganareta hayo yalipokuwa yakiwashwa
kusaidia huduma za umeme katika kipindi cha mgao wa huduma hiyo muhimu.
Mhandisi
Yussuf Reja alifahamisha kwamba shirika la umeme lilikuwa likizalisha
umeme kupitia Maganareta hayo kwa uniti moja yenye thamani ya shilingi
500/- ambayo ingelazimika kuwauzia wateja wake uniti moja kwa shilingi
700/- gharama ambayo ni mzigo kwa mwananchi wa kawaida.
“
Ukweli uliowazi gharama ya kuyaendesha Maganareta hayo kupitia shirika
la Umeme ni kubwa mno na inaweza kuleta maafa kwa shirika hilo endapo
yataendelea kutumiwa “. Alitahadharisha Mhandisi Yussuf Reja.
Naye
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji, Nishati na Madini
Nd.Mustafa Aboud Jumbe alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
kwamba Wizara hiyo tayari imeshapokea mapendekezo ya Shirika hilo
kuhusiana na majanareta hayo ya Kituo cha Umeme Mtoni.
Naibu
Katibu Mkuu huyo wa Ardhi Mustafa Jumbe alisema Wizara hiyo inajipanga
kuyafanyia kazi mapendekezo hayo na baadaye kuyawasilisha Serikali kuu
kwa ajili ya kupatia ufumbuzi muwafaka.
Mapema
Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } Thabit Salum
Khamis alisema mfumo mpya wa kisasa wa huduma za umeme kwenye kituo
kikuu cha Umeme Mtoni uitwao { SCADA } umewawezesha watendaji wa shirika
hilo kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa.
Thabit
Salum alimfahamisha Balozi Seif kwamba mfumo huo umepunguza kero kubwa
ya kukatika katika kwa umeme kulikokuwa kukitoa usumbufu kwa wananchi
walio wengi kwenye maeneo mbali mbali wakati inapotokea hitilafu.
Alieleza
kwamba shirika la umeme limekuwa na vituo vikubwa vinavyosambaza umeme
kutoka kituo kikuu cha Mtoni kwenda Welezo na Fumba ambavyo vimepangwa
kusambaza huduma hiyo na kuacha mfumo wa zamani wa kutumia laini moja
tuu.
Kaimu
Meneja huyo wa Shirika la Umeme aliongeza kwamba matumizi zaidi
ya umeme huongezeka kutoka Mega walts 33.16 nyakati za asubuhi hadi
kufikia Mega Walts 48.1 kipindi cha jioni lakini huduma hiyo
kuongezeka zaidi katika kipindi cha siku kuu na kufikia hadi Mega Walts
52.
Uwezo
wa laini mpya ya umeme uliopo Zanzibar hivi sasa imefikia Mega Walts
mia moja ambapo shirika limekuwa na hakiba ya umeme kwa zaidi ya
asilimia 50% mbali ya ile laini ya zamani yenye uwezo wa mega walts 40
kutokana na kuchakaa kwake.
Akitoa
nasaha zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
aliwatanabahisha watendaji wa shirika la umeme kwamba huduma ya umeme
hivi sasa imekuwa nyenzo muhimu ya kiuchumi kwa vile inasaidia kipato
cha mwananchi.
Balozi
Seif alisema ni vyema kwa watendaji wa shirika la umeme kufanya kazi
zao katika mazingira ya ushindani mfano wa kuwepo mashirika mengine
yanayotoa huduma hizo hapa nchini kwa lengo la kupata ufanisi sambamba
na kutoa huduma bora kwa wateja wake.
“ Watendaji lazima mfanye kazi kama mko katika ushindani wa kibiashara na
mashirika mengine licha ya kwamba mpo peke yenu. Kila mkiamka lazima
mfikirie mtaongeza vipi wateja wengine wapya “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha wafanyakazi wa shirika hilo
kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya athari na hatari ya kutumia
mafundi wa mitaani katika kuungiwa huduma hiyo jambo ambalo mara nyingi
huleta hasara kutokana na hitilafu zinazojitokeza baadaye.
Post a Comment