MALKIA WA ZOUK NCHINI HAFSA KAZINJA AIBUKA NA WIMBO WA "NIMUOKOE NANI" KUMUENZI MUHIDIN MAALIM GURUMO ALIYESTAFU


Msanii Hafsa Kazinja akiimba wimbo wa Muhidin Maalim Gurumo wa "NIMUOKOE NANI" enzi hizo akiwa na NUTA jazz ikiwa ni mchango wake kumuenzi mwanamuziki huyo nguli ambaye amestaafu rasmi muziki baada ya kudumu katika fani tangu mwaka 1960. Hapa ni OM Records jijini Dar es salaam alikorekodia chini ya wanamuziki wakongwe Abdul "Key Devu" Salvado na Omari Mkali. 
Sikiliza maoni yao mwishoni mwa ngoma hii...

Baada ya ukimya wa muda mrefu, Malkia wa Zouk Tanzania, Hafsa Kazinja, anaibuka upya katika fani akiwa na ingizo lake la kwanza kati ya kumi aliyoandaa kwa kuimba wimbo maarufu wa NUTA Jazz Band uitwao “NIMUOKOE NANI” anauouleta hewani katika mahadhi ya Zouk.
 Hafsa Kazinja anasema ameamua kurudi ulingoni kwa kutoa wimbo huo ili kumuenzi Mzee Muhidin Maalim Gurumo ambaye amestaafu rasmi fani ya muziki baada ya kufanya kazi hiyo akiwa na bendi mbalimbali tokea mwaka wa 1960.
 “Nimeamua kuimba wimbo huu wa “NIMUOKOE NANI” ili kumuenzi gwiji huyu wa muziki kwani wakati yeye anastaafu na mimi ndiyo naibuka upya baada ya kukaa kimya kwa muda”, anasema Hafsa ambaye alitoka kwa wimbo wake wa “PRESHA” aliomshirikisha Banana Zorro.
 Hafsa ameandaa wimbo huo wa “NIMUOKOE NANI” katika studio za OM Productions ya jijini Dar es salaam chini ya wanamuziki nguli, Abdul Salvador na Omari Mkali.
 “Nafurahi kwamba wimbo wa NIMUOKOE NANI nimeuimba baada ya kupata Baraka zote toka kwa mtunzi na mwimbaji wake Mzee Gurumo mwenyewe.
 “Haikuwa rahisi kama inavyoweza kudhaniwa kwani baada ya kwenda kumuona nyumbani kwake alinifanyisha mtihani wa kuuimba wote kabla ya kuridhika maana alisema asingefurahi kuona wimbo wake unaimbwa hovyo hovyo na kuharibiwa radha yake”, anasema Hafsa, ambaye hivi sana anamalizia ngoma zake zingine tisa alizotunga mwenyewe, kabla ya kuvamia anga kwa mara ingine.
 Hafsa anasema katika ukimya wake amekuwa akifanya utafiti na kujifunza kwa undani zaidi fani ya muziki, akipata mawaidha maridhawa toka kwa wanamuziki nguli ndani nan je ya nchi wakiwemo Muhidin Maalim Gurumo, Omar Mkali, Abdul Salvador na Lokassa ya Mbongo wa Congo aliyekutana na kufanya naye kazi alipokuwa ziarani Marekani hivi karibuni.
 Msanii huyu wa kizazi kipya anasema ataitambulisha rasmi ngoma ya “NIMUOKOE NANI” katika tamasha la kumuenzi Mzee Gurumo lililopangwa kufanyika OKtoba 1, 2013 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.
 “Natumaini wapenzi wa muziki watafurika kwa wingi kwenye tamasha hilo name naahidi kuitendea haki ngoma ya “NIMUOKOE NANI” hivyo wasikose kuja kujionea wenyewe jinsi sie wa kizazi kipya tunavyoweza kufanya kazi na wakubwa wetu wa kazi, anaongezea Hafsa ambaye pia anaandaa video yake pamoja na ya ngoma zake zingine mpya.
 Mkongwe Abdul Salvador, ambaye alikuwa mmoja wa waanzilishi wa bendi ya TANCUT ALMASI YA Iringa iliyotamba na mtindo wake wa “FIMBO LUGODA”, anamtaja Hafsa kazinja mmoja wa wanamuziki wa kike waliojaaliwa sauti nzuri na kipaji cha hali ya juu hapa nchini. “
Kwa kuweza kuimba wimbo wa Mzee Gurumo na kuupatia kisawasawa inadhihirisha kwamba Hafsa ni mwanamuziki aliyekomaa maana si mchezo kuimba nyimbo ya wakongwe kwa ufasaha kama alivyofanya Hafsa. 
 “Na hii inadhihirisha kwamba uwezekano wa kizazi kipya na cha zamani kufanya kazi pamoja ni mkubwa sana na sioni kwa nini isiwe hivyo”, anasema Salvador.
 Omari Mkali, aliyetamba na bendi ya CHUCHU SOUNDS, chini ya marehemu Yusuf Chuchu, naye anamwelezea Hafsa Kazinja kama moja ya majembe ya muziki hapa nchini kwa upande wa kinamama, na kwamba anaweza kufika mbali endapo kama moto aliokuja nao upya atauendeleza. IMETOLEWA NA OM PRODUCTIONS NA HISIA SOUNDS

Post a Comment

Previous Post Next Post